Jumanne, 18 Agosti 2026

TMJA MTWARA WAVUKA BAHARI KUTALII URITHI WA DUNIA VISIWANI KILWA

Na SOJO MWAKOBA – Mahakama, Mtwara

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Katarina Mteule, ambaye pia ni Mlezi wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Mtwara, hivi karibuni aliwaongoza wanachama wao katika ziara ya siku mbili ya utalii iliyofanyika katika Visiwa vya Kilwa Masoko.

Katika ziara hiyo ya siku mbili ambayo Mhe. Mteule aliongozana na Mwenyekiti wa TMJA Tawi la Mtwara, Mhe. Aisha Ndossy, wanachama walitembelea magofu ya mali kale yaliyopo Kilwa Kisiwani, ikiwemo Msikiti Mkuu wa Malindi na makaburi ya kale (Malindi Gravestones), kabla ya kufanya utalii wa majini na kuvuka hadi Kisiwa cha Songo Mnara ambako walitembelea magofu ya Ikulu ya Kale ya Masultani (Sultan’s Palace Ruins).

Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni utalii, elimu pamoja na kuchangamsha na kuburudisha akili na mwili baada ya majukumu ya kazi. Wanachama walitembelea na kujionea mabaki ya mali kale zilizopo visiwani humo, kujua historia ya urithi huo, huku pia wakipata elimu ya uendeshaji wa mashauri yanayohusu uhifadhi wa wanyamapori kutoka kwa mwanasheria wa  Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA).

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Jaji Mfawidhi aliwapongeza wanachama kwa ushirikiano wao na moyo wa kupenda kujumuika pamoja katika matukio muhimu kama hayo, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza ipasavyo kauli mbiu ya Mahakama ya “Uadilifu, Weledi na Uwajibikaji.”

“Niwapongeze wanachama kwa umoja na ushirikiano wenu wa kupenda kujumuika katika shughuli kama hizi. Tuendelee kushirikiana na kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza ipasavyo kauli mbiu ya Mahakama yetu,” alisema Mhe. Mteule.

Miongoni mwa waliohudhuria ziara hiyo ni Mahakimu, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Mtwara, Mhe. Seraphine Nsana, wakiwa ni sehemu ya wanachama wa TMJA Tawi la Mtwara, pamoja na Mtendaji wa Mahakama Mtwara, Bw. Yusuph Msawanga.

Ziara hiyo imeongeza mshikamano miongoni mwa wanachama huku ikiwapa fursa ya kujifunza historia na urithi wa mali kale za Kilwa, historia ya urithi huo,  pamoja na umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mtwara, Mhe. Katarina Mteule (wapili kulia) akiwasili Kilwa Kisiwani kutembelea magofu ya Malindi.

Mwanasheria kutoka TAW A(kulia) akiwakaribisha wanachama wa TMJA Mtwara kabla ya kuanza kutembelea magofu ya Kilwa Kisiwani.

Wanachama wa TMJA Mtwara wakipata elimu ya historia ya urithi wa Dunia ulioachwa hapo Kilwa Kisiwani.

Mahakimu wakitembelea moja ya majumba la kale yaliyopo Kilwa Kisiwani.

Wanachama wa TMJA Mtwara wakiwa kwenye picha ya pamoja kama kumbukumbu ya ziara yao ya utalii visiwani Kilwa.

Wanachama wa TMJA Mtwara wakiwa kwenye boti katika utalii wa majini baada ya kutembelea magofu ya Kilwa Kisiwani.

Mahakimu wakisoma mchoro wa ramani mara baada ya kufika Kisiwa cha Songo Mnara ikiwa ni siku ya pili ya ziara yao.

Picha ya pamoja ya wanachama wa TMJA Tawi la Mtwara mbele ya Magofu yanayopatikana Songo Mnara (Kilwa).

Wanachama wa TMJA Mtwara wakifurahia mandhari tulivu na upepo wakiwa kwenye kibanda cha kitamaduni.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni