- Asema Mahakama ipo tayari kushirikiana ili kuimarisha matumizi ya usuluhishi
Na FAUSTINE KAPAMA na
HABIBA MBARUKU-Mahakama, Dodoma
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, leo tarehe 12 Agosti,
2026, amekutana na Wajumbe wa Baraza la Taasisi ya Wasuluhishi Tanzania (TIArb)
na kufanya nao mazungumzo yanayolenga kuimarisha ushirikiano na kukuza utatuzi
wa migogoro kwa njia ya mbadala (ADR).
Viongozi hao wakiongozwa
na Rais wa TIArb, Wakili Msomi Aderickson Njunwa, wamekutana na Jaji Kiongozi
kwenye ofisi yake iliyopo Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Wajumbe wengine
walioambatana na Rais wa TIArb, ni Wakili Nasra Songoro, Wakili Sultan Rajab,
Wakili Marydenisia Katemana na Bi. Mariam Mruma, ambaye ni Katibu wa Baraza
hilo.
Akizungumza na Wajumbe hao,
Mhe. Dkt. Siyani alieleza kuwa Mahakama ya Tanzania ipo tayari kushirikiana na TIArb
kuimarisha matumizi ya usuluhishi au upatanshi, kwani ndiyo mfumo ambao kwa
sasa unapewa uzito mkubwa duniani katika utatuzi wa migogoro, iwe ya kibiashara
kiuchumi na usalama.
“Mahakama itajitahidi
kadri inavyowezekana kuwa karibu na nyinyi, tushirikisheni tukutane katikati
pale ambapo mkono wetu na mkono wenu hauwezi kufika. Tumefungua milango, msione
shida kugonga pale ambapo mkono wenu unafika, tutawafungulia,” amesema.
Jaji Kiongozi amewaambia Wajumbe
hao kuwa Mahakama ya Tanzania ina wataalam wengi, ambao wana ujuzi wa masuala
ya usuluhishi, wanaoweza kusaidia pale kunapotokea changamoto kwenye masuala
hayo.
Aidha, Mhe. Dkt. Siyani
amewaeleza kuwa TIArb inachokifanya ni kitu kikubwa ambacho jamii ya Watanzania
bado haijapata elimu ya kutosha, hivyo wanayo kazi kubwa ya kuifanya Taasisi hiyo
inafahamika zaidi kwa wananchi ili wanaopaswa kuitumia wasiwe wageni pekee.
“Nchi yetu inakua
kiuchumi na uchumi unapokua kunakuwa na migogoro mingi ya kiuchumi. Ufanisi katika
eneo la usuluhishi ni jambo ambalo lina faida kubwa kwani njia hii imeonekana
kuokoa muda zaidi, tofauti na mchakato wa kimahakama,” amesema.
Jaji Kiongozi ametumia
fursa hiyo kuwakumbusha Wajumbe hao kuwa Tanzania imeanza kutekeleza Dira ya
Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo eneo kubwa linahusu haki, hivyo kila Taasisi, ikiwemo
TIArb ina mchango wa kutoa ili kuwa na jamii inayokusudia kufikia malengo ya
Dira hiyo.
Mhe. Dkt. Siyani amebainisha
kuwa Mahakama ya Tanzania inapoanda Mpango Mkakati wake, inajaribu kuamsha
ndoto hiyo namna gani inaweza kutoa mchango wake katika utekelezaji wa dira
hiyo.
“Ninyi kama TIArb hamtaweza
kama sheria hazitakuwa haziwapi fursa ya kujielekeza huko, ni wakati muafaka
sana wa kuishirikisha ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mkiwa na mawazo
yenu ya nini kitarahisisha kukuza usuluhishi katika nchi yetu. Hili ni jambo
muhimu sana na huu ndiyo wakati sahihi zaidi kuliko utekelezaji wa Dira
utakapokaposhika kasi,” amesema.
Awali, akizungumza baada
ya kukutana na Jaji Kiongozi, Wakili Njunwa alieleza malengo ya kufanya ziara
hiyo, ikiwemo kumshukuru kwa kuwafungulia Mkutanao wa nane wa Taasisi hiyo kwa niaba
ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George M. Masaju, uliofanyika
jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Rais wa TIArb alimweleza
Jaji Kiongozi kuwa lengo lingine ilikuwa kueleza namna Mkutano huo
ulivyofanyika hadi kumalizika kwake, maazimio yaliyofikiwa na kusikiliza
ushauri au malelekezo yake kwa Taasisi hiyo.
Aidha, Rais wa TIArb aliomba
Mahakama kushirikiana na Taasisi hiyo katika mambo mbalimbali, ikiwemo kupata
mwongozo wa namna bora ya utendaji kazi ambao utasaidia kufikia lengo kuu la
kuisaidia Serikali katika kuboresha mifumo ya haki.
Rais huyo alifafanua kuwa
majukumu ya TIArb, ni usimamizi wa mashauri ya usuluhishi na kujenga uwezo kwa
kuandaa vipindi mbalimbali vya mafunzo, yanayolenga kukuza matumizi ya njia
mbadala za utatuzi wa migogoro.










Hakuna maoni:
Chapisha Maoni