Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe wameanza kufanya mazoezi ya pamoja ikiwa ni programu maalum ya kuimarisha afya ya mwili, kuimarisha mahusiano na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi kwa watumishi wa kada zote.
Programu hiyo ilianza tarehe 11 Agosti, 2026 ambapo Majaji, Mahakimu pamoja na Watumishi wengine wa Mahakama Kuu Njombe hukutana baada ya saa za kazi mara mbili kwa wiki kwa siku ya Jumanne na Ijumaa kwa ajili ya kushiriki kwenye mazoezi hayo.
Katika nyakati tofauti tofauti, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa amekuwa akiwasisitiza watumishi kufanya mazoezi mara kwa mara kwa ajili ya kulinda afya ya mwili hasa katika maeneo hayo yenye hali ya hewa ya baridi kali pamoja sambamba na kuimarisha mahusiano na mshikamano kwa watumishi wa kada zote.
Alisema kuwa, Majaji wa Mahakama hiyo wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mazoezi hayakwami bila sababu za msingi, huku na wao wakishiriki kikamilifu kwenye mazoezi hayo pamoja na kuwahamasisha watumishi wote kushiriki kwa wingi kwakuwa mazoezi ni kwa ajili ya kujenga afya imara pamoja na kukabiliana na hali ya hewa ya baridi iliyopo mkoani Njombe ili waweze kuendelea na majukumu yao bila kutetereka kiafya.
Naye, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano aliwasisitiza watumishi kuhakikisha mazoezi yanafanyika mara kwa mara na vifaa vyote vinavyohitajika katika mazoezi vinapatikana kwa wakati kama vile jezi, vibao vya mazoezi na mikeka kwa ajili ya mazoezi ya aina mbalimbali ili kuwapa watumishi hamasa ya kufanya mazoezi. Aidha, alieleza kuwa Taasisi nyingine kama Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) ya mkoani humo wameonesha nia ya kuungana na Mahakama katika program hiyo.
Kwa upande wa watumishi wa Mahakama Njombe wameonesha kufurahia programu hiyo ya mazoezi ambayo huwa yanaanza kwa kukimbia umbali wa kilomita tatu (3) yakifuatiwa na mazoezi ya kunyoosha viungo vya mwili ambapo mazoezi hayo yamewafanya watumishi wengi kushiriki bila kukosa kwa kuzingatia ratiba endelevu iliyotolewa na uongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Njombe.
Jaji wa Mahakama ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe.Obadia Bwegoge (mwenye jaketi la kijivu kushoto) akiwa sambamba na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe.Liadi Shamshama pamoja na watumishi wengine wakiendelea na mazoezi ya kukimbia.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe.Joseph Luambano (mwenye kofia nyeusi) akiwa mstari wa mbele kuhamasisha mazoezi ya mwili kwa watumishi wote wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Njombe.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe.Obadia Bwegoge, viongozi pamoja na watumishi mbalimbali wakifanya mazoezi ya viungo.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni