Alhamisi, 6 Agosti 2026

JAJI MAMBI ATETA NA KATIBU MKUU WA TUGHE TAIFA

Na CHRISTOPHER MSAGATI- Mahakama, Manyara

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi ametembelewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Bw. Henry Mkunda ofisini kwake jana tarehe 05 Agosti, 2026 mjini Babati.

Akimkaribisha Katibu Mkuu huyo wa TUGHE, Jaji Mfawidhi Mhe. Dkt. Mambi alimueleza Bw. Mkunda kuwa, ujio wake ni muhimu sana katika kujadili maslahi mapana ya ushirikiano miongoni mwa watumishi wa Umma wanaounda Shirikisho hilo la wafanyakazi kutoka Taasisi mbalimbali.

“Katibu Mkuu ninakukaribisha sana Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara na tumefurahi umefika kwa kuwa ujio wako ni chachu ya kuongeza ushirikiano ambao unapaswa kuwepo miongoni mwetu sisi watumishi wa Umma. Ninaomba pia muendelee kutoa elimu kwa watumishi kuhusu umuhimu wa kujiunga kwenye vyama vya wafanyakazi,” alisema Mhe. Dkt. Mambi.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora akitoa salamu alimshukuru Katibu huyo wa TUGHE kwa kufika mahakamani hapo na kumueleza kuwa, watumishi wa Mahakama wanapaswa kujua majukumu yanayofanywa na Vyama vya Wafanyakazi hivyo waendelee kufundishwa na kueleweshwa.

“Pamoja na jukumu kubwa tulilopewa la kusikiliza na kuamua mashauri, watumishi wetu wanastahili kupata nafasi ya kueleweshwa majukumu ya Vyama hivi vya wafanyakazi kwa sababu vyama hivi vinawasaidia sana kujua haki na wajibu wao wanapokuwa kazini kama watumishi wa umma,” ameongeza Mhe. Kamuzora.

Naye, Bw. Mkunda, aliushukuru Uongozi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara kwa ukaribisho aliopewa na kuahidi kuongeza ushirikiano miongoni mwa watumishi wa Mahakama katika kutekeleza majukumu yake ya kitaasisi kwani Chama kinategemea wanachama kwa kiasi kukubwa ili kuendesha programu zake.

“Mhe. Jaji Mfawidhi ninakushukuru sana kwa kunikaribisha ofisini kwako, nami ninaahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika ofisi yako ili kazi zetu tunazozifanya ziende kwa ufasaha lakini pia ili tuwawezeshe watumishi wote waweze kujua haki na wajibu wao wa kila siku wanapokuwa katika mazingira ya kazi,” alisema Bw. Mkunda.

Aidha, Bw. Mkunda aliipongeza Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara kwa kuweza kumpata na kuchaguliwa Bw. Shadrack Aron ambaye ni mtumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara ambaye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Manyara katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni.

Katika ziara hiyo, Mwenyekiti huyo Bw. Mkunda aliambatana na Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Manyara Bw. Shadrack Aron pamoja na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Manyara Bw. Maulidi Kasimba.

Viongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara wakiwa kwenye mazungumzo yaliyokuwa yanaendelea katika ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (kiti cha mbele) wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa Bw. Henry Mkunda (aliyevalia kofia).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi akifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea ofisini kwake mara baada ya kutembelewa na Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa Bw. Henry Mkunda.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wageni waliomtembelea ofisini kwake wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa Bw. Henry Mkunda. 

Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Manyara Bw. Shadrack Aron akifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea mara baada ya kutembelewa na Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa Bw. Henry Mkunda.

Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa Bw. Henry Mkunda akimsikiliza na kufuatilia ujumbe mahususi wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (hayupo pichani) wakati alipomtembelea ofisini kwake.


Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe. Devotha Kamuzora (kulia) na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu hiyo Mhe. Charles Mnzava (kushoto) wakifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea katika ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi walipotembelewa na Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa Bw. Henry Mkunda (hayupo pichani).

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni