Jumatano, 12 Agosti 2026

JAJI MFAWIDHI MBEYA ATETA NA KAMATI YA UTATU YASISITIZA KUIMARISHA UTOAJI HAKI

Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Kamati ya Utatu inayojumuisha Jeshi la Polisi Tanzania (PT), Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imefanya ziara Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi za haki jinai.

Kamati hiyo iliongozwa na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) Bw. Basilius Namkambe ilikutana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya ofisini kwake jana tarehe 11 Agust 2026, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kufanya ukaguzi wa utendaji kazi wa vyombo hivyo na kukutana na wadau wanaoshirikiana navyo katika kutekeleza majukumu ya haki jinai.

Ziara hiyo imelenga kupata maoni, kubaini changamoto na kupokea mapendekezo kutoka kwa wadau wa mfumo wa haki jinai, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kuboresha namna vyombo hivyo vinavyotekeleza majukumu yao kwa pamoja.

Akizungumza wakati wa kukutana na Kamati hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya amesisitiza kuwa ushirikiano wa karibu miongoni mwa vyombo vya haki jinai ni msingi muhimu katika kulinda haki, usalama na ustawi wa jamii.

“Vyombo vyote vya haki jinai vikishirikiana kwa pamoja itasaidia kurahisisha kulinda usalama na haki kwa jamii. Nashukuru sana kwa ujio wenu na tunaahidi kama Mahakama tutatoa ushirikiano wa kutosha kila itakapohitajika kufanya hivyo,” alisema Mhe. Mtulya.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mhe. Zawadi Laizer, amesema kuwa, Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya imeendelea kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa wadau hao katika uendeshaji wa mashauri na utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya kimahakama yanayohitaji ushirikiano wa vyombo vya haki jinai.

Mhe. Laizer aliongeza kuwa, ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha mnyororo wa utoaji haki jinai unafanya kazi kwa ufanisi, huku kila chombo kikitekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Ziara ya Kamati ya Utatu Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya ni miongoni mwa hatua zinazolenga kuimarisha uratibu na mahusiano ya kikazi baina ya Mahakama na wadau wake, hususan katika masuala yanayohusu utekelezaji wa haki jinai.

Aidha, ziara hiyo inaendana na utekelezaji wa Nguzo ya Tatu ya Mahakama ya Tanzania, inayolenga kujenga na kuboresha mahusiano mazuri na wadau pamoja na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama.

Kwa mantiki hiyo, Mahakama ya Tanzania imeendelea kutambua kuwa ufanisi katika utoaji wa haki unahitaji ushirikiano wa karibu na endelevu kati ya Mahakama na wadau wote wa mfumo wa haki, kwa lengo la kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati, kwa usawa mapema ipasavyo na kwa kuzingatia sheria.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (katikati waliosimama mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na Moafisa wa Taasisi zinazounda Utatu waliomtembelea ofisini kwake, pamoja na sehemu ya Viongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya mara baada ya mazungumzo yanayohusu Taasisi hizo. Wengine ni (kushoto) Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer, (wa pili kushoto) ni Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma kutoka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Bw. Joseph Kasongwa Mwaiswelo, (wa kwanza kulia) ni Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mbeya, Bw. Jasper Luoga na (wa pili kulia) ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) Bw. Basilius Namkambe.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya, akiwa ofisini kwake akizungumza na Wageni ambao ni Kamati ya Utatu inayojumuisha Jeshi la Polisi Tanzania (PT), Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), walipomtembelea ofisini kwake (hawapo pichani) jana tarehe 11 Agosti, 2026.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni