· Awakumbusha kutunza Siri na Vifaa vya Ofisi
· Awasisitiza kushirikiana, kuheshimiana, kupendana na kuthaminiana katika nyakati mbalimbali za maisha
Na MARY GWERA,
Mahakama-Dodoma
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu ametoa rai kwa Waandishi Waendesha Ofisi na
Wasaidizi wa Ofisi wa Mahakama kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kujituma
huku wakizingatia taratibu zilizopo zinazowaongoza kutekeleza ipasavyo majukumu
ya kada zao.
Dkt. Jingu ametoa rai hiyo leo tarehe 12
Agosti, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania
jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Waandishi Waendesha Ofisi na
Wasaidizi wa Ofisi wanaohudumu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Mahakama ya
Rufani, Mahakama Kuu Masjala Kuu na Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma.
“Mnafanya kazi nzuri,
niwaombe tu muendelee kufanya vizuri, tunakumbushana tu sio kwamba kuna
changamoto kubwa, nyie wote mnafanya kazi vizuri, lakini nawaomba tuendelee
kufanya hivyo kufanya kazi kwa weledi, kujituma lakini kwa kuzingatia maadili
ya kazi zilizopo,” amesema Dkt. Jingu.
Kadhalika, Mtendaji Mkuu
amewataka watumishi hao kuendeleza ushirikiano, kuheshimiana, kupendana na kuthaminiana
katika nyakati mbalimbali za kimaisha.
Aidha, amewaeleza
Watumishi hao kuwa, wao ni miongoni mwa kada muhimu katika maendeleo ya Taasisi
kwakuwa kazi zao ambazo mara nyingi wanafanya kazi nyuma ya pazia zina mchango
mkubwa katika ustawi wa Taasisi.
Katika hatua nyingine,
Dkt. Jingu amewakumbusha watumishi hao kutunza siri za ofisi pamoja na vifaa
vyote vya Ofisi na kusisitiza kuwa, kutofanya hivyo, kunahatarisha usalama wa
Ofisi.
Mtendaji Mkuu ameitisha kikao hicho na watumishi hao ikiwa ni mara yake ya kwanza kuanza kukutana na watumishi wa Mahakama wa Kada mbalimbali tangu aapishwe kushika nafasi hiyo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 19 Juni, 2026.
Katika kikao hicho
kililenga kusikiliza na kupokea masuala na changamoto mbalimbali zinazowakabili
watumishi hao ili kuona namna ya kuzifanyia kazi ili kuboresha utendaji kazi.
Miongoni mwa masuala
mbalimbali ambayo watumishi hao wameomba kuboreshewa ni pamoja na huduma ya
usafiri, semina/mafunzo, maslahi na mengine.
Aidha, Mtendaji Mkuu amewahakikishia watumishi hao kuwa, Mahakama itafanyia kazi yaliyowasilishwa na kwamba milango ya ofisi yake iko wazi kukaribisha ushauri na maoni mbalimbali ili mambo yaende vizuri.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu-Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo-Mahakama, Bi. Patricia Ngungulu, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala-Mahakama, Bw. Stephen, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimaliwatu, Bi. Sharifa Mbaraka pamoja na baadhi ya Maofisa wengine wa Mahakama. 
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu na Waandishi Waendesha Ofisi na Wasaidizi wa Ofisi wa Makao Makuu ya Mahakama, Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu Masjala Kuu na Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma leo tarehe 12 Agosti, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick (aliyesimama mbele) akizungumza jambo wakati wa Kikao kati ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Waandishi Waendesha Ofisi na Wasaidizi wa Ofisi kilichofanyika leo tarehe 12 Agosti, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
(Picha na JEREMIA LUBANGO, Mahakama)















Hakuna maoni:
Chapisha Maoni