·
Azindua pia Vifaa vya
TEHAMA awakabidhi Mahakimu na Watumishi wengine wa Mahakama
Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa amezindua Mahakama ya Mwanzo Lupembe katika Wilaya ya Njombe baada ya ujenzi wake kukamilika na shughuli zake zikiendelea.
Uzinduzi wa Mahakama hiyo ulifanyika hivi karibuni sambamba na uzinduzi wa vifaa vya Teknolojia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kugawa vishikwambi kwa Mahakimu na Maofisa wa Mahakama pamoja na kwa Watumishi mbalimbali.
Uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Lupembe lenye vifaa vya kisasa vya TEHAMA unalenga kuimarisha upatikanaji haki kwa wananchi mapema ipasavyo na kwa gharama nafuu.
Katika hafla hizo za uzinduzi wa jengo hilo pamoja na uzinduzi wa ugawaji wa Vifaa vya TEHAMA, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Njombe alizungumzia kuhusu dhima ya Mahakama katika kutoa haki kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji bila kuchelewesha huduma za msingi kwa Wananchi.
Mhe. Nongwa, aliwaasa Watumishi waweze kutumia vifaa vya TEHAMA pamoja na kuvitunza ambapo alizungumza na Wananchi wa Lupembe wa maeneo hayo kuhakikisha wanatunza jengo hilo na miundombinu yake ili liweze kudumu kwa muda mrefu kwa kuwa jengo hilo limetokana na kodi za wananchi wenyewe.
“Kuanzishwa kwa Mahakama hii kutasaidia kupunguza msongamano wa mashauri na kuharakisha utoaji haki, hatua hii ni sehemu ya juhudi za Mahakama ya Tanzania na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kila Mwananchi anapata haki kwa wakati na kwa gharama nafuu,” alisema Jaji Nongwa.
Mhe. Nongwa aliongeza kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, Msajili Mkuu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama Njombe kwa kuwezesha na kusimamia ujenzi wa jengo hilo.
Kwa upande wake, Mgeni Maalum katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma Swedi aliwaasa wananchi kushirikiana na Watumishi wa Mahakama kwa ajili ya kulinda msingi wa amani na kudumisha ustawi wa utoaji haki kwa wananchi.
“Hii Mahakama ni mali yetu, hivyo ni wajibu wetu sote kushirikiana na kutunza jengo la Mahakama hii kwa umoja na tutunze miundombinu yote ili Kazi ya Mahakama na Mahakimu ya kutafsiri sheria ifanyike kwa ufasaha” alisema Mhe. Swedi.
Naye, Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Njombe, Bw. Richard Mbambe, alipata wasaa wa kuwasilisha Taarifa fupi ya Mpango wa Ujenzi na Ukarabati wa Miradi ya Mahakama ya Mwanzo Lupembe lililopo Wilaya ya Njombe ambapo jengo hilo ambalo limejengwa kwa fedha za mradi zilizotolewa na Benki ya Dunia (WB) zilizotumika mpaka kukamilika kwa ujenzi wake.
Aidha, alisema Jengo la zamani la Mahakama ya Mwanzo Lupembe, lilikuwa kwenye hifadhi ya Barabara, hivyo hali hiyo ilisababisha utafutaji wa eneo jingine kwa ajili ya kujenga Mahakama mpya ikiwa ni moja ya mikakati ya Mahakama ya Tanzania na Serikali kwa ujumla kuboresha majengo ya Mahakama ambayo ni ya zamani ili yaweze kuwa ya kisasa zaidi.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama Kuu Njombe akiwemo Jaji wa Mahakama ya Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Njomba, Mhe. Obadia Bwegoge, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya za Njombe, Ludewa, Wanging’ombe na Makete pamoja na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Njombe, Mhe. Victoria Nongwa (aliyesimama mbele kushoto) akiwa tayari amekata utepe kuashiria uzinduzi wa Jengo la Mahakama ya Mwanzo Lupembe Wilaya ya Njombe.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Njombe, Mhe. Victoria Nongwa (aliyeketi katikati), Jaji wa Mahakama ya Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Njombe, Mhe.Obadia Bwegoge (kushoto) na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Njombe, Mhe. Joseph Luambano wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Mahakama ya Tanzania Njombe baadhi wakiwa wameshika vifaa vya TEHAMA ambavyo ni vishikwambi walivyokabidhiwa na Jaji Mfawidhi, Mhe. Nongwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Njombe, Mhe.Victoria Nongwa akipanda mti wa mparachichi kwa ajili ya kumbukumbu. Waliosimama ni Viongozi mbalimbali pamoja na wageni waalikwa waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Lupembe wilayani Njombe.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Njombe, Mhe.Matilda Kayombo (wa kwa kushoto) akimuonesha kitu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Njombe, Mhe.Victoria Nongwa (wa pili kushoto) wakiwa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma Swedi. Wengine wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Obadia Bwegoge, aliyesimama nyuma wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Njombe, Mhe. Joseph Luambano na viongozi wengine.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama mbalimbali kutoka Mahakama Njombe wakiwa katika picha ya pamoja.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama)






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni