Jumanne, 4 Agosti 2026

MAHAKAMA YA RUFANI KUENDESHA MASHAURI 38 YA MADAI, JINAI MASJALA NDOGO MBEYA

Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Mahakama ya Rufani ya Tanzania inayoketi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya imeanza kuendesha Kikao chake cha kusikiliza mashauri 38 ya rufaa za madai na jinai ambacho kimeanza jana tarehe 03 Agosti, 2026 na kinatarajiwa kuhitimishwa mnamo tarehe 29 Agosti, 2026.

Kikao hicho kinachoongozwa na Jopo moja la Majaji wa Mahakama ya Rufani ambalo Mwenyekiti wake ni Jaji wa Rufaa ya Tanzania ya Tanzania, Mhe. Dkt. Gerald A. M. Ndika, Majaji wengine katika Jopo hilo ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Benhajj Shaban Masoud na Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina.

Akiwasilisha taarifa katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Mbeya, ambacho ni kikao cha maandalizi ya uendeshaji wa kikao hicho (Pre- Session Meeting), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Bernad Mpepo alisema kuwa, jumla ya mashauri 38 ya rufaa za madai na jinai yamepangwa kusikilizwa katika Masjala Ndogo ya Mbeya ikiwa rufaa za madai ni 27 na rufaa za jinai 11.

Aidha, Mhe. Mpepo aliongeza kuwa, Katika kikao hicho kinachoketi Mbeya pia kuna mashauri kutoka Kanda za Songwe, Tabora na Iringa na katika kuhakikisha ufanisi wa kikao hicho na kufikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa ratiba ya kikao ilitolewa kwa wakati na hati za kuitwa shaurini za wadaawa kwa ajili ya usikilizwaji wa mashauri zimesambazwa na juhudi za kuwapata wadaawa amabao hawajapatikana zinaendelea.

Naye, Mwenyekiti wa kikao hicho, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald A. M. Ndika, alisisitiza kuhusu kuzingatia upachikaji wa nyaraka zote muhimu zinazohitajika hasa nyaraka zinazopandishwa kielektroniki kuhakikisha kuwa, zinaambatanishwa pia kama nyaraka ngumu kwenye vitabu na majalada husika.

Aidha, Mhe. Dkt. Ndika alihitimisha kwa kuomba ushirikiano baina ya wadau na kusisitiza kufuata kanuni na sheria ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Ninawashukuru sana kwa kuhudhuria kwenu, tufuate kanuni na tushirikiane ili tufikie mafanikio yaliyokusudiwa. Lengo letu ni kutafuta haki kwa pamoja na ni matarajio yetu kuwa, kutokana na kwamba mpango wa kusikiliza mashauri haya uliandaliwa mapema pamoja kwa ufuatiliaji wa karibu wa kila jalada, kikao hiki kitafikia malengo yaliyokusudiwa bila akukwama,” alisema Mhe. Dkt. Ndika.

Kwa upande wao Jeshi la Magereza kupitia mwakilishi wa Mkuu wa Gereza Ruanda Mbeya alisema kuwa, watahakikisha wafungwa wanafikishwa kwa wakati mahakamani na watahakikisha wanatoa kibali kwa mawakili kuwaona wateja wao walipo gerezani hata kwa siku za mapumziko ambazo ni jumamosi na jumapili ili kuweka utaratibu sawa.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Viongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya akiwemo Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya, Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Mussa Pomo, Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Angaza Mwipopo, Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Bw. Festo Chonya, Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Bernad Mpepo, Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer, Mawakili na Wadau wengine wa Haki Jinai na madai kutoka Mbeya, Songwe na Tabora.

Mwenyekiti wa jopo la Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Dkt. Gerald A. M. Ndika, (katikati) akiongoza kikao cha wadau cha uendeshaji wa shauri ya rufaa za Mahakama ya Rufani, kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina na kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Benhajj Shaban Masoud

Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Bernad Mpepo akiwasilisha taarifa ya mashauri yanayotarajiwa kusikilizwa katika kikao hicho.

Sehemu ya Viongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya wakiongozwa na (wa kwanza kulia) ambaye ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya, Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Angaza Mwipopo (aliyesimama katikati) na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Mussa Pomo (wa kwanza kushoto).

Sehemu ya wadau walioshiriki katika kikao hicho.

Sehemu ya wadau walioshiriki katika kikao hicho

Sehemu ya wadau walioshiriki katika kikao hicho

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Tanganyika (TLS) Chapta ya Mbeya wakili msomi Bw. Philip Mwakilima akizungumza jambo katika kikao hicho.

Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani Tanzania wakipokelewa na Waheshimiwa Majaji, Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya walipowasili katika viwanja vya Mahakama hiyo.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha- Mahakama)







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni