Jumatano, 19 Agosti 2026

JOPO LA MAJAJI WA RUFANI LAFANYA TATHMINI YA UENDESHAJI MASHAURI MASJALA MBEYA

Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Mahakama ya Rufani ya Tanzania hivi karibuni imefanya kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za usikilizaji wa mashauri ya rufaa za madai na jinai katika Masjala Ndogo ya Mbeya, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhitimisha rasmi kikao cha Mahakama hiyo kilichoanza tarehe 3 Agosti, 2026 na kinachotarajiwa kumalizika tarehe 28 Agosti, 2026.

Kikao hicho kiliongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, Mhe. Dkt. Gerald A. M. Ndika na kuhudhuriwa na Majaji wa Rufani walioambatana naye katika kikao hicho ambao ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Dkt. Benhajj Shaban Masoud na Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina na Viongozi wengine wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kikao hicho, Naibu Msajili Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Bernard Mpepo alisema kuwa, kati ya mashauri 38 yaliyopangwa kusikilizwa, mashauri 33 sawa na asilimia 87% yameshasikilizwa na kupatiwa maamuzi.

Aidha, alieleza kuwa, mashauri 05 ya rufaa za madai yameahirishwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuwapa warufani nafasi ya kuwafikishia wajibu rufaniwa hati za mashauri, kumpa nafasi mrufani kumteua wakili mwingine na kutoa nafasi ya kupatikana kwa mwakilishi wa kisheria wa mjibu rufani aliyefariki, hali iliyolazimu wahusika kuongezewa muda wa kufanya mabadiliko hayo.

Katika tathmini hiyo, ilibainika kuwa kumekuwa na changamoto kadhaa ikiwemo wadaawa kutokuleta taarifa za kuondoa mashauri mapema jambo ambalo lingesaidia kupanga mashauri mengine, kutokufuata taratibu za uendeshaji wa mwenendo kabidhi (committal proceedings), washtakiwa wengi wanaotajana kuwakilishwa na wakili mmoja, na kutokuzingatia kanuni inayotaka mdaawa akifariki ateuliwe msimamizi wa mirathi ndani ya miezi 12 kwa mujibu wa kanuni ya 105(2) ya kanuni za mahakama ya Rufani.

Aidha, pamoja na changamoto hizo, kikao kilieleza kuridhishwa na mafanikio yaliyopatikana, ikiwemo kusikilizwa kwa mashauri 33 kati ya 38 yaliyopangwa pamoja na ushirikiano mzuri uliooneshwa na Warufani kwenye rufaa za madai, Mawakili wa Serikali na wa kujitegemea waliohudhuria kwenye vikao hivyo kwa wakati.

Mafanikio hayo yameendelea kuimarisha juhudi za Mahakama ya Rufani ya Tanzania za kuongeza ufanisi katika usikilizaji wa mashauri na kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati mapema ipasavyo.

Viongozi wengine walishiriki kikao hicho ni kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya ambao ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya, Jaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Said Kalunde, Jaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Mussa Pomo.

Wengine ni Naibu Msajili Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Bernard Mpepo, Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer, Mahakimu mbalimbali wakiongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya wilaya Mbeya Mhe. Teddy Mlimba, Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Alintula Ngalile na wadau wengine wa haki Madai na Jinai Mawakili na wadau wengine wa Haki Jinai na madai kutoka Mbeya, Songwe na Tabora.

Mwenyekiti wa Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Dkt. Gerald A. M. Ndika, (katikati) akiongoza kikao cha kufanya tathmini ya uendeshaji wa mashauri ya Madai na Jinai Masjala Ndogo Mbeya, kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina na kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Benhajj Shaban Masoud.

Sehemu ya Viongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya waliohudhuria kikao cha tathmini (kulia) ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya, Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Said Kalunde (wa pili kulia), Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Mussa Pomo (wa pili kushoto) na Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer (kushoto)

Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Bernad Mpepo akiwasilisha taarifa ya Naibu Msajili ya tathmini kuhusu uendeshaji wa mashauri ya rufaa Masjala Ndogo Mbeya katika kikao hicho.

Sehemu ya wadau walioshiriki katika kikao hicho

Sehemu ya wadau walioshiriki katika kikao hicho.

Sehemu ya wadau walioshiriki katika kikao hicho.

Mwakilishi kutoka Gereza Kuu Ruanda Mbeya akitoa neno la shukurani kwa Jopo la Majaji wa Rufani katika kikao hicho.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)








Hakuna maoni:

Chapisha Maoni