Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji wa Mahakama
ya Rufani Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe.
Dkt. Paul Faustine Kihwelo amesema Mafunzo Elekezi kwa Naibu Wasajili wa Mahakama ni
muhimu kwa mustakabali wa uendeshaji wa Mahakama na utoaji wa haki nchini.
Mhe. Dkt. Kihwelo ameeleza
hayo leo tarehe 31 Agosti, 2026 wakati akitoa neno la utangulizi wakati wa
hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo hayo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Makao
Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
“"Mhe. Jaji Mkuu,
kama nilivyosema awali, mafunzo haya yameandaliwa ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa Mpango Mkakati. Na moja ya eneo muhimu sana ni kujengea uwezo
watumishi wa Mahakama ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi. Na mafunzo
elekezi haya yanakusudia kulifikia huko,” amesema Jaji Kihwelo.
Mkuu huyo cha Chuo cha
IJA amesema kuwa, mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa
Mahakama na Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya mwaka 2019, lakini pia ni sehemu ya
Sera ya Mafunzo ya Taifa ambayo inataka Viongozi wote katika ngazi mbalimbali
pamoja na watumishi waweze kupata mafunzo elekezi kabla ya kuanza kutumikia
nyadhifa mpya.
Aidha, Mhe. Dkt. Kihwelo amemshukuru
Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwa kukubali kuwa Mgeni Rasmi na kuona umuhimu wa
kufanyika kwa mafunzo hayo na kuweza kuja kufungua mafunzo hayo yeye mwenyewe
bila kutuma Mwakilishi. kutumikia nafasi hizo."
Kadhalika, Jaji Kihwelo
amewapongeza Naibu Wasajili hao ambao wamepata nafasi hizo kwa imani ambayo Uongozi
wa Mahakama umeonesha kwao. Hivyo, amewatakia kila la heri katika utumishi wao
wakitumikia nafasi hiyo ya muhimu sana ambapo amesisitiza kuwa siku zote anaamini
kuwa, injini ya Mahakama ni Wasajili pamoja na Watendaji.
Kuhusu ratiba ya mafunzo hayo
kwa Naibu Wasajili, Mhe. Dkt. Kihwelo amesema kwamba, ratiba hiyo imeandaliwa
kwa umakini sana. Lakini pia uteuzi au uchaguzi wa Wawezeshaji umefanyika kwa
umakini ili kuhakikisha kwamba Wasajili hao watapitishwa kwa muda muda mdogo wa
siku tano, lakini kile watakachokipata ni kikubwa.
“Wawezeshaji wengi ni
wabobezi kama nilivyosema, walio wengi kwa kweli wamekuwa na uzoefu wa kufanya
kazi katika maeneo yao. Kwa hiyo naamini waheshimiwa watapata fursa nzuri sana,”
ameeleza Jaji Kihwelo.
Ameongeza kuwa, ratiba
hiyo imejikita kwenye kutatua au kwenye maeneo ambayo ni changamoto za Mahakama
kwa sasa na baadaye.
“Mara nyingi tukisema
mafunzo lazima yajikite kwenye kuhakikisha tuna tunatibu changamoto zilizopo na
changamoto za baadaye. Ndio maana kwa mara ya kwanza, kwa kweli, naona kuna
mafunzo kabisa maalum kwa ajili ya Waendeshaji wa Masjala ya Mahakama ya Rufani
katika Masjala ndogo za Mahakama ya Rufani katika ngazi tofauti,” amesema Jaji Kihwelo.
Katika hatua nyingine,
Mhe. Dkt. Kihwelo amewapongeza washiriki hao kushiriki mafunzo kwa mara
ya kwanza katika ukumbi mpya wa Mahakama uliopo ndani ya jengo la Makao Makuu
ya Mahakama ya Tanzania na kuchukua fursa hiyo kumpongeza Jaji Mkuu na Menejimenti
ya Mahakama ya Tanzania kwa ujumla.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo akitoa neno la utangulizi leo tarehe 31 Agosti, 2026 wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo hayo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni