Jumatatu, 31 Agosti 2026

TEKELEZENI MAJUKUMU YENU IPASAVYO KWA KULINDA MASLAHI YA HAKI; JAJI MKUU

·       Jaji Mkuu Masaju awataka Naibu Wasajili hao kuwajibika ipasavyo kwa mujibu wa Katiba

·       Akemea vikali wanaoingilia Uhuru na Maamuzi ya Mahakama

·       Awaonya Maofisa Mahakama hao kutojihusisha na Uanaharakati

·       Awakumbusha kuzingatia Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050

·       Ahimiza ushirikiano na mahusiano mazuri kati ya Naibu Wasajili na Watendaji kwa utekelezaji fasaha wa majukumu

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amewataka Naibu Wasajili wa Mahakama nchini kuendelea kutekeleza majukumu yao ipasavyo huku wakilinda maslahi ya haki (Interest of Justice).

Mhe. Masaju ameyasema hayo leo tarehe 31 Agosti, 2026 alipokuwa akifungua Mafunzo Elekezi kwa Naibu Wasajili wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

“Tuna wajibu wa kuendelea kutekeleza majukumu yetu kwa kulinda maslahi ya haki, kwa kutokufungwa kwa masharti ya kiufundi kupita kiasi hadi kukwamisha upatikanaji haki,” amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amesema kuwa, Wasajili wa Mahakama ndio 'injini' ya Mahakama. Hivyo, wana nafasi kubwa katika maendeleo ya Mhimili huo ambao mamlaka yake kwa mujibu wa Ibara ya 4 ni kutekeleza jukumu la utoaji haki.

“Kwa mujibu wa Ibara ya 107A(1), Mahakama ndio yenye kauli ya mwisho kwenye masuala ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano. Na ukiwa unaongozwa na kanuni kadhaa: mojawapo, kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kiuchumi au kijamii, kutochelewesha haki bila kuwepo sababu ya msingi na kwamba itakuwa huru, italazimika tu kuzingatia sheria za nchi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama ambavyo Ibara ya 107A inavyoelekeza,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amesema, shughuli zote za umma huongozwa na kusimamiwa na sheria; hakuna shughuli yoyote ya umma ambayo haiongozwi na kusimamiwa na sheria. Na kwa sababu hiyo, Katiba inakuwa pia sheria, kwa mujibu wa ile Sheria ya Tafsiri za Sheria, sura ya kwanza ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Jaji Mkuu amewakumbusha Naibu Wasajili hao kuwa waadilifu ili wanapofanya maamuzi, watu waone kweli kwamba haki imetendeka. Amesisitiza, “Na katika hilo lazima tuwe waadilifu, tunapoacha kuwa waadilifu, tukiwa wazembe, tukiwa wavivu, uwezo wetu ukiwa mdogo, watu hawatatuheshimu.”

Vilevile, Mhe. Masaju amekemea vikali tabia ya baadhi ya watu kuingilia uhuru na maamuzi ya Mahakama huku akibainisha kuwa, Katiba imeiwekea ulinzi kwa Mahakama kupitia Ibara ya 30(2)(c) inayoelekeza kuhakikisha utekelezaji wa hukumu au amri ya Mahakama iliyotolewa katika shauri lolote la madai au la jinai.

Aidha, Ibara ya 30(2)(d) inatamka kulinda heshima, haki na uhuru wa watu wengine au faragha ya watu wanaohusika katika shauri lolote mahakamani, kuzuia kutoa habari za siri, au kulinda heshima na uhuru wa Mahakama.

“Ni lazima hukumu na amri za Mahakama zitekelezwe, ni Mahakama gani hiyo inaweza ikafanya maamuzi halafu yasitekelezwe, halafu ikabaki kuwa Mahakama?” amehoji Jaji Mkuu.

Ameongeza kuwa, Katiba hiyo pia inaelekeza kwamba lazima Mahakama iheshimike; uhuru wake, mamlaka, na hadhi yake lazima vilindwe na viheshimiwe. Kwa hiyo, lazima kulinda sifa na haki au uhuru wa watu wengine, au maisha binafsi ya watu wanaohusika katika mashauri mahakamani, kuzuia kutoa habari za siri, kutunza heshima, mamlaka, na uhuru wa Mahakama.

“Hivi karibuni tulivyotaka kusimamia suala hili kwenye Kanda zenu, tulikuwa na sababu za msingi. Hatutaruhusu watu kuidharau Mahakama au kuitisha hii Mahakama. Kwamba sasa nchi itatawaliwaje? Tunahitaji amani! Hivyo tunatakiwa kuwa makini kuliangalia suala hili, hatutaendekeza kitendo ambacho kitafanya Taifa hili liharibike, ni haki za binadamu gani ambazo haziwezi kujali hata hizo Taasisi za kikatiba zilizowekwa kwa ajili ya kutekeleza haki za binadamu?” ameeleza Mhe. Masaju.

Amewataka Naibu Wasajili hao kutotishwa kwa namna yoyote ile kwakuwa wamepewa madaraka hayo na Katiba hivyo wayatekeleze kwa ufanisi ipasavyo kama ilivyo kawaida ya viapo vyao.

Amerejea Ibara ya 30 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayosema:

"Haki na uhuru wa binadamu ambavyo misingi yake imeorodheshwa katika Katiba hii havitatumika na mtu mmoja kwa maana ambayo itasababisha kuingiliwa kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine au masahi ya umma."

Kadhalika, amewakumbusha Naibu Wasajili hao kuwa sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050, kwa kuwa haki ina nafasi kubwa sana.

“Tuna jukumu kubwa sana Mahakama. Na Dira yenyewe inasema: "Taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea." Kwa hiyo haki unaona imetajwa pale; ni muhimu, wanaohusika na kutenda haki kwa mujibu wa Ibara ya 4 ya Katiba ya Jamhuri ni kina nani? ni sisi Mahakama. Kwa hiyo, tunapojifunza nanyi mnaochukua nafasi za uongozi katika kipindi hiki, mjue kwamba tunao wajibu wa kutekeleza majukumu wetu lakini kwa kuzingatia yale matakwa ya Dira,” amesema Jaji Mkuu.

Ameongeza kwa kueleza kuwa, pamoja na mambo mengineyo, Dira hiyo inalenga kuwa na jamii yenye mshikamano na kutengamana, ambayo watu wake wanaishi kwa haki, amani, na kuheshimiana. Na msingi mkuu wa Dira hiyo ni utawala, amani, usalama, na utulivu. Ametaja maeneo matano ya kipaumbele ya Dira hiyo kuwa ni Utawala Bora na Haki, Serikali za Mitaa imara na zenye ufanisi.

Amesema kuwa, “Unapozungumzia masuala ya haki, unazungumza juu ya masuala ya sheria. Kwa hiyo, shughuli zote hata zinazoenda kutekelezwa chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 zinaongozwa na kusimamiwa na sheria. Na mimi na baadhi ya wasaidizi wangu tumesha 'map out' sheria zote zinazohusika katika utekelezaji wa Dira hii, kwa sababu Dira hii haikuacha kitu. Hapa tulipo, unaweza ukabainisha kwamba mbali na Katiba, swala kama hili, kwa mfano utawala bora, utatekelezwa kupitia sheria zipi. Kwa hiyo, hapo ndipo utakapona masuala ya haki. Na katika utekelezaji wa sheria hizi, kuna kuzivunja na kuzitekeleza.”

Mhe. Masaju ameeleza kwamba, muundo wa Dira hiyo umeweka mazingira ya kukuza uchumi na shughuli nyingine mbalimbali, ikiwemo za kibiashara, hivyo; hali hiyo inaweza kuja ongezeko la migogoro ikiwemo migogoro ya kibiashara, kiwekezaji na migogoro ya kijinai.

Kadhalika, Jaji Mkuu amewataka Maofisa Mahakama hao kuwajibika ipasavyo wanapotekeleza majukumu yao ambao amesema; “Sisi Mahakama tuna nafasi kubwa sana, tulipozungumza nanyi tarehe 17 Juni mwaka huu, tuliwaeleza wajibu wenu. Na mimi niwaombe Wasajili wote mlioko hapa, muendelee kuwajibika katika utekelezaji wa majukumu yenu, kuwajibika ipasavyo kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyoelekeza kwenye Ibara ya 25 ya Katiba hii. Ni suala la uwajibikaji, ni suala la kikatiba na wajibu wetu sisi wenyewe. Na ni vizuri mjifunze na kuielewa hii Dira. Tulitoa vitabu tukavisambaza kwenye kanda, lakini pia hii Dira inapatikana kwenye nakala laini (soft copies).”

Mhe. Masaju amerejea Ibara ya 146(2)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa moja ya majukumu ya Serikali za Mitaa ni kuhakikisha utekelezaji wa sheria na ulinzi wa wananchi kwenye maeneo hayo na ndio maana Mahakama inao mpango wa kujenga Mahakama za Mwanzo kila kata.

“Na tumeshawaomba mketi kwenye maeneo yenu, mhakikishe kwamba mnashirikiana na Serikali ngazi ile ya Mkoa na Wilaya kupata viwanja kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hizi,” amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju ameongeza kuwa, katika kutekeleza hayo, wanatekeleza Katiba, hivyo, ushirikiano ambao umeendelea kuwa nao watendaji kwenye Kanda na Naibu Wasajili, waudumishe utasaidia kufanikisha jambo hilo.

Amewasisitiza Naibu Wasajili hao kuwajibika ipasavyo huku akirejea kipaumbele cha tatu cha Dira cha utumishi wa umma unaowajibika. Ambapo amewashauri kuendelea kuwajibika kwakuwa ni swala la kisheria na ni wajibu wao.

“Lakini kipaumbele cha nne ni amani, usalama, na utulivu. Ukiangalia yote haya, unaona ni kwa namna gani Mahakama ya Tanzania itaendelea kuwa na mchango muhimu katika kuhakikisha ustawi na maendeleo ya Taifa hili kiuchumi, kijamii, na kisiasa,” amesema Jaji Mkuu.

Aidha, ameeleza kuwa, ili Mahakama iweze kutekeleza jukumu hilo, lazima moja iwe na uwezo wa kulitekeleza. Kuna suala la miundombinu, kuna suala la rasilimaliwatu.

Akizungumzia suala la Utu, Jaji Mkuu Mkuu amewataka Naibu Wasajili hao kuweka mbele suala la utu huku akiwakumbusha kuwazingatia pia Watu wenye mahitaji maalum.

Kadhalika amewakumbusha Watumishi wote wa Mahakama kwa ujumla kuwa watu wenye uwezo wa kutekeleza wajibu kwa ufanisi ipasavyo (the capacity to deliver, competence), kuwa waadilifu (integrity), kuwa wabunifu; kuwa watu wa kujiongeza, na kujiongeza pia kumeelezwa katika Ibara ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 25 kwenye uwajibikaji pale.

“Tunapaswa kuwa ni watu ambao ni 'sensitive to justice', mnao wivu wa kuona kutenda haki na kuitenda haki ipasavyo. Na haki nimeshasema ni maamuzi yanayofanywa na Mahakama huru kwa kuzingatia Katiba na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na kwenye viapo vyetu tunaapa kwamba tutatekeleza majukumu yetu kwa mujibu wa ile sheria ya viapo, kwa kuzingatia Katiba, sheria, mila, na desturi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tukiwa huru, bila hofu, woga, upendeleo, wala chuki. Kitu hicho lazima tukisimamie na kukitekeleza ipasavyo, bila kufanya hivyo, tunakosa sifa hiyo ya kuwa watu wa kutoa haki,” amesisitiza.

Mafunzo hayo muhimu yenye kulenga kutoa mwongozo wa utendaji wa Naibu Wasajili hao yamefanyika kwa mara ya kwanza kwenye ukumbi mpya wa mikutano uliopo ndani ya Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jambo ambalo limeonesha kufurahiwa na Viongozi pamoja na watumishi wengi walioshiriki katika ufunguzi wa Mafunzo hayo.

“Ninayo furaha kubwa kwa tukio hili muhimu. Na nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuliwezesha tukio hili. Lakini pia na kuiwezesha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuweza kutenda mambo haya makubwa. Na leo sisi, Mahakama ya Tanzania, tumekuwa na ukumbi huu muhimu sana. Mikutano yetu mingiambayo ilikuwa na sababu za msingitutakuwa tunaifanyia hapa. Ni ukumbi wa kisasa sana,” amesema Mhe. Masaju.

Aidha, Jaji Mkuu ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwezesha kutimia kwa ndoto ya kuwa jengo kubwa na la kisasa, vilevile amewashukuru na kutambua kazi kubwa iliyofanywa na Majaji Wakuu Watangulizi wake kuanzia mwaka 1920 mpaka sasa.

“Viongozi waliotangulia wamefanya kazi kubwa. Sisi ambao tunapata fursa ya kutumika katika Mahakama ya Tanzania kipindi hiki, tunakaa kwenye jengo ambalo lilianza kujengwa na wenzetu wakati huo, na linaendelea kujengwa na kuimarika. Kwa hiyo, niwashukuru sana hawa viongozi wote, Maofisa wa Mahakama (Judicial Officers) na hao ambao sio 'Judicial Officers' waliokuwepo kuanzia mwaka 1920 mpaka sasa hivi. Na kwa sababu hiyo, nikupongeze Mtendaji Mkuu na watangulizi wako kwa kufikia hatua hii. Na nanyi Mwenyezi Mungu aendelee kuwabariki sana,” ameeleza Mhe. Masaju.

Matukio katika picha Ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Naibu Wasajili wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania leo tarehe 31 Agosti, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akitoa hotuba ya Ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Naibu Wasajili wapya Mahakama Kuu ya Tanzania leo tarehe 31 Agosti, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili (waliosimama). Wa tatu kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo, wa tatu kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dodoma, Mhe. Fatma Khalfan, wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu na wa kwanza kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya.

Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Viongozi na Watumishi wengine wa Mahakama wakisikiliza hotuba ya Mgeni Rasmi Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Naibu Wasajili leo tarehe 31 Agosti, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza wakati wa ufunguzi Mafunzo Elekezi kwa Naibu Wasajili leo tarehe 31 Agosti, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.






 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni