Jumanne, 1 Septemba 2026

MWAKA MMOJA WA MAHAKAMA YA MWANZO TERRAT; WAJA NA MAFANIKIO KIUTENDAJI

  • Kiwango cha Uondoshaji mashauri chafurahisha

 Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha

Mahakama ya Mwanzo Terrat ni miongoni mwa Mahakama za Mwanzo mpya katika Wilaya ya Arusha na miongoni mwa mafanikio makubwa katika juhudi za kuboresha huduma za Mahakama ili kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi. 

Mahakama hii imekuwa chachu muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za haki kwa urahisi, ufanisi na mapema ipasavyo.

Mahakama ya Mwanzo Terrat ilianza rasmi kutoa huduma tarehe 20 Agosti, 2025, na sasa imetimiza mwaka mmoja tangu kuanza kwa safari yake ya kuhudumia wananchi.

Katika kipindi hicho, Mahakama imeendelea kutekeleza wajibu wake kwa uadilifu na weledi, huku ikiwa sehemu muhimu ya mageuzi na maboresho yanayoendelea kufanywa na Mahakama ya Tanzania.

Akizungumza na Mwandishi wetu, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Terrat, Mhe. Salma Mwamende amesema kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuanza, Mahakama ya Mwanzo Terrat imepokea jumla ya mashauri 974. Kati ya mashauri hayo, mashauri 954 yamesikilizwa na kutolewa uamuzi, huku mashauri 20 yakiendelea.

“Kwa mwaka huu wa 2026, kwa kipindi cha Januari hadi Agosti, tumepokea jumla ya mashauri 604 na tayari tumemaliza mashauri 604 na mashauri 20 yanaendelea kusikilizwa, Mahakama yetu ina Mahakimu wawili lakini tunachapa kazi kuhakikisha tunaendana na wingi wa mashauri yanayokuja katika Mahakama yetu,” alisema Mhe. Mwamende.

Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Arusha, Mhe. Sheila Manento alieleza kuwa, takwimu hizo za mashauri ya Mahakama ya Terrat zinaonesha kiwango cha juu cha ufanisi katika utoaji wa huduma za haki, ambapo Mahakama hiyo imeweza kumaliza zaidi ya asilimia 97.9 ya mashauri yote yaliyopokelewa, na kubakiza takribani asilimia 2.1 ya mashauri yanayoendelea.

“Mahakama hiyo imeweza kusikiliza na kumaliza mashauri ndani ya wastani wa wiki tatu, muda ambao ni mfupi ikilinganishwa na muda wa miezi mitatu unaotajwa katika miongozo kwa mashauri ya Mahakama za Mwanzo kwa shauri kusajiliwa hadi kuamuliwa. Mafanikio haya yanaonesha jitihada za Mahakama katika kuhakikisha mashauri yanashughulikiwa kwa wakati na wananchi wanapata haki kwa haraka,” alisema Mhe. Manento.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa, katika mwaka wake wa kwanza, Mahakama ya Mwanzo Terrat yenye Mahakimu wawili tu, imeweza kutekeleza kwa ufanisi jukumu lake la msingi la kutoa haki kwa wananchi mapema ipasavyo, huku ikidhibiti mlundikano wa mashauri na kuhakikisha muda wa usikilizwaji wa mashauri unapungua.

Mwaka mmoja wa Terat ni zaidi ya kumbukumbu kwani umekuwa mwaka wa mafanikio, huduma na matumaini mapya hasa kwa wananchi wa Kata za Terrat, Muriet, Elerai na Sokoni 1.

Mafanikio hayo ni matokeo ya maono na juhudi za Uongozi wa Mahakama ya Tanzania wakishirikiana na wadau wake wote katika kuhakikisha kuwa huduma za haki zinasogezwa karibu na wananchi na hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.


Jengo la Mahakama ya Mwanzo Terrat ambalo limetimiza mwaka mmoja tangu lianze kutumika kutoa huduma.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Arusha, Mhe. Sheila Manento alipotembelewa na Mwandishi wetu ofisini kwake tarehe 31 Agosti, 2026 kuzungumzia kuhusu Mahakama ya Mwanzo Terrat kutimiza mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Terrat, Mhe. Salma Mwamende alipotembelewa na Mwandishi wetu ofisini kwake tarehe 31 Agosti, 2026 kuzungumzia Mahakama hiyo kutimiza mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Arusha, Mhe. Sheila Manento (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo Terrat; Mhe. Salma Mwamende (kushoto) na Mohamed Nyenye (kulia).

Picha ya pamoja; Wa kwanza kushoto ni Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Arusha, Mhe. Sheila Manento katikati ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Terrat, Salma Mwamende, wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Terrat, Mohamed Nyenye, wa pili kushoto ni Kaimu Ofisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya Arusha, Bw. Sunday Kilimba pamoja na Watumishi wengine wa Mahakama hiyo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


 



 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

                            

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni