Ijumaa, 18 Septemba 2026

JAJI AWAMU MBAGWA AFANYA UKAGUZI MAHAKAMA KIBAHA

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Kibaha

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Awamu Mbagwa amefanya ukaguzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha na Mahakama ya Wilaya Kibaha ili kuangalia mwenendo wa mashauri na masuala ya utawala.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo tarehe 17 Septemba, 2026, Mhe. Mbagwa alisema ukaguzi huo ni wa kawaida unaofanyika kila baada ya robo mwaka.

Akitoa taarifa ya utekelezaji ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani, Naibu Msajili na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi alisema Mahakama mkoani humo ina jumla ya Mahakama za Wilaya saba na Mahakama za Mwanzo 40.

Amesema, katika utekelezaji wa maagizo ya Viongozi Wakuu wa Mahakama Mkoa wa Pwani umejitahidi kupanga mashauri kwa kuzingatia muda, pia uondoshaji wa mashauri ya mlundikano inaridhisha kwa kuzingatia maelekezo, wananchi wanapata huduma katika Mhakama ya Hakimu Mkazi kulingana na taratibu.

“Wananchi wanapata huduma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kulingana na taratibu zilizopangwa na pia usikilizwaji wa mashauri kupitia Mahakama Mtandao (Virtual Court) unaendelea kuzingatiwa kipindi cha Julai-Septemba, 2026 yamesikilizwa mashauri saba kwa njia ya mtandao (VC)” amesema Mhe. Mkhoi.

Akizungumzia kuhusu uelewa wa watumishi juu ya Mpango Mkakati  na Programu ya Maboresho ya Mahakama, Naibu Msajili huyo amesema  elimu inatolewa kupitia  vikao vya kila wiki ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya kazi zillizofanyika ndani ya wiki na kuelimishana.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai amesema Mahakama pamoja na Wadau wa Haki wamekuwa na vikao vya mara kwa mara vya kujadiliana namna bora ya uendeshaji wa mashauri na kuondokana na mashauri ya mlundikano ambapo wameweza kuondoa mlundikano wa mashauri mahakamani na vikao hivyo vimekuwa vikizaa matunda.

Mhe Lukumai amesema pia, elimu kwa umma imekuwa ikitolewa kwa ajili ya ufafanuzi wa taratibu za Mahakama na sheria mbalimbali, ambapo Mahakama ya Wilaya Kibaha na Mahakama zake za Mwanzo wametenga muda wa siku moja kwa juma muda wa nusu saa kabla ya kuanza kwa mashauri  kwa kuweka ratiba maalum ambayo kila Idara ndani ya Mahakama inakuwa na siku ambayo inatoa elimu kwa wananchi.

Kadhalika, Mfawidhi huyo ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi ya Julai mpaka Septemba ambapo ni pamoja na kutoa huduma kwa wakati na kutoa nakala za hukumu mara baada ya kumaliza kusikiliza shauri, kumaliza na kuzuia mashauri mlundikano, kutoa elimu na mengine.

Katika ziara hiyo, Jaji Mhe. Mbagwa aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hussein Mushi, Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Bitulo Magafu na Ofisa Utumishi wa Kanda hiyo, Bi. Winifrida Shirima.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Awamu Mbagwa akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili kwenye Ofisi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani tarehe 17 Septemba, 2026 kwa lengo la kufanya ukaguzi wa Mahakama hiyo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Awamu Mbagwa (aliyeketi mbele) akiwa katika Kikao pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya Kibaha wakati wa ukaguzi wa Mahakama uliofanyika tarehe 17 Septemba, 2026.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hussein Mushi akitambulisha msafara wa Jaji Awamu Mbagwa baada ya kuwasili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani na Mahakama ya Wilaya Kibaha kwa ajili ya ukaguzi. Aliyeketi kulia ni Msaidizi wa Sheria, Mhe. Bitulo Magafu.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mahakama hiyo mbele ya Jaji Awamu Mbagwa (hayupo katika picha). Aliyeketi kulia ni Naibu Msajili na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Awamu Mbagwa akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hussein Mushi (kushoto), Naibu Msajili na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwana, Mhe. Joyce Mkhoi (kulia). Waliosimama nyuma, wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani, Bw. Nestory Mujunangoma, wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha Mhe. Emmael Lukumai, wa pili kushoto ni Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe Bitulo Magafu na wa pili kulia ni Ofisa Utumishi wa Mahakama Kuu ya  Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Bi.Winifrida Shirima.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Awamu Mbagwa (wa pili kushoto) akiagana na Mtendaji wa Mahakama Pwani, Bw. Nestory Mujunangoma (wa kwanza kushoto) baada ya kumaliza ziara ya ukaguzi Mahakamani hapo. Wanaoshuhudia wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani ambaye pia ni Naibu Msajili, Mhe. Joyce Mkhoi na wa pili kulia ni Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Bitulo Magafu.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


 


 


 


 


 


 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni