Jumatano, 2 Septemba 2026

MAHAKAMA KUU NJOMBE YAMUAGA BI. GRACE MTEMELA ALIYESTAAFU UTUMISHA WA UMMA

  •  Adumu katika Utumishi wa Umma kwa miaka 42 

 Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe imefanya hafla fupi ya kumuaga aliyekuwa Mtumishi wa Mahakama hiyo, wake, Bi. Grace Mtemela, aliyestaafu utumishi wa umma.

Hafla ya kumuaga Mtumishi huyo aliyekuwa akihudumu katika Kada ya Msaidizi wa Ofisi ilifanyika tarehe 31 Agosti, 2026 iliandaliwa na Ofisi ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe.

Bi. Mtemela alianza kuhudumu Mahakama ya Tanzania mwaka 1984, katika kipindi cha miaka 42 ya utumishi wake, amewahudumia Viongozi na Maofisa mbalimbali wa Mahakama, wakiwemo Mahakimu Wafawidhi wa Wilaya mkoani Njombe. Aidha, amestaafu akiwa anahudumu katika Ofisi ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, Bw. Richard Mbambe, aliwakaribisha watumishi wa Mahakama na kutoa neno la shukrani kwa mstaafu huyo kwa utumishi wake na mchango wake katika Mahakama.

Naye, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa, alimpongeza Bi. Mtemela kwa kumaliza salama kipindi chake cha utumishi wa umma.

“Tunashukuru kwa huduma yako katika kipindi cha miaka 42 katika utumishi wa Mahakama. Wewe utabaki kuwa sehemu ya familia ya Mahakama.Tutakapokuhitaji, usisite kutusikiliza, na pia kama utatuhitaji, usisite kuja. Wewe bado ni mtumishi wa Mahakama,” alisema Mhe. Nongwa.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano, alimshukuru Bi. Mtemela kwa kipindi chote alichohudumu katika ofisi yake. Pia aliwataka watumishi wengine kujifunza kutokana na nidhamu, kujituma na uzoefu aliouonesha katika kipindi cha utumishi wake. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Bi. Mtemela aliwashukuru Viongozi na Watumishi wa Mahakama kwa kujitolea kufika katika hafla hiyo na kwa kumuandalia tukio hilo pamoja na kumpatia zawadi mbalimbali. Alieleza kuwa hakutarajia kuandaliwa hafla hiyo kwa namna hiyo.

Mstaafu huyo alionesha kufurahishwa na tukio hilo na kuwaomba radhi viongozi na watumishi wenzake endapo kuna wakati aliwahi kutenda jambo kinyume na taratibu au kusababisha usumbufu katika kipindi cha utumishi wake. Aidha, aliwatakia kila la heri watumishi wote wanaoendelea na utumishi wa Mahakama.

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, imemtakia Bi. Grace Mtemela afya njema na maisha mema katika kipindi chake kipya cha kustaafu.


Mtumishi Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Njombe, Bi.Grace Mtemela (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili Mhe.Joseph Luambano (wa pili kulia) pamoja na Watumishi wengine wa Mahakama hiyo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Morogoro)

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni