Na SETH KAZIMOTO – Mahakama Arusha
Kikao cha nne cha
Mahakama ya Rufani kwa mwaka, 2026 kilichoketi Arusha kuanzia tarehe 03 hadi 28
Agosti, 2026 kimefanikiwa kusikiliza jumla ya mashauri 31 kati ya 38
yaliyopangwa, sawa na asilimia 82 ya mashauri yote.
Jopo la
Majaji wa kikao hicho kiliongozwa na Mhe. Lilian Mashaka huku Majaji wengine wakiwa Mhe. Gerson Mdemu, na Mhe. Imani Aboud.
Akiwasilisha taarifa ya Tathmini ya Kikao hicho cha Mashauri ya Rufani hivi karibuni, Naibu Msajili wa Mahakama ya
Rufani Tanzania, Mhe. Flora Mtarania alisema kuwa, mashauri 38 yalipangwa kusikilizwa ambapo kati ya
hayo, 12 yalikuwa Rufaa za Jinai, 25
Rufaa za Madai, na moja ilikuwa Maombi ya Madai. Idadi ya mashauri yaliyosikilizwa ni 31 na mashauri yaliyoahirishwa ni 7.
Mhe. Mtarania ameongeza kwa
kusema kuwa, Mashauri saba yaliyoahirishwa ni kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kukosekana
kwa nyaraka muhimu za Baraza la Ardhi, Vifo kwa baadhi ya Wadaawa na Wasimamizi wa Mirathi
kutoongezwa shaurini, kukosekana kwa wadaawa katika anuani
zilizowekwa kwenye rekodi za rufaa na kutofautiana
kwa majina ya wadaawa kwenye nyaraka za Mahakama Kuu.
Naibu Msajili huyo aliyataja mafanikio kadhaa yaliyopatikana katika kikao
hicho kuwa ni pamoja na Mashauri yaliyopangwa kusikilizwa na kumalizika kwa
asilimia 82, Wadaawa wote
waliopata wito walihudhuria mahakamani kwa wakati, hivyo kuwezesha usikilizaji wa mashauri kwa wakati na Maamuzi yaliyosomwa kutolewa kwa wadaawa kwa wakati na kupandishwa katika Maktaba Mtandao ya Mahakama (TanzLII).
Kikao hicho cha Mashauri ya Mahakama ya Rufani Kanda ya Arusha kilifanyika sanjari na vikao vingine tisa katika
Kanda za Mwanza, Shinyanga, Moshi, Bukoba, Dar es Salaam, Iringa, Mbeya,
Sumbawanga na Dodoma.
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Jopo la Majaji, Mhe. Lillian Mashaka akiongoza Kikao cha Tathmini ya Usikilizaji Mashauri ya Mahakama ya Rufani mkoani Arusha. Aliyeketi kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Gerson Mdemu na kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Imani Aboud. Kikao hicho cha tathmini kilifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi (IJC) Arusha.
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Gerson Mdemu (kushoto) akifafanua mambo
kadhaa wakati wa Kikao cha Tathmini ya Usikilizaji wa Mashauri ya Mahakama ya
Rufani mkoani Arusha. Kikao hicho cha tathmini kilifanyika hivi karibuni katika
ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Arusha, Mhe. Frank Mahimbali
akichangia jambo wakati wa Kikao hicho. Aliyeketi upande wa kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Arusha,
Mhe. Aisha Bade. Kikao hicho cha tathmini kilifanyika hivi karibuni katika
ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi (IJC) Arusha.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Arusha, Mhe. Seif Kulita akichangia jambo wakati wa
Kikao cha Tathmini ya Usikilizaji wa Mashauri ya Mahakama ya Rufani. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Arusha, Mhe. Nyigulila Mwaseba. Kikao
hicho cha tathmini kilifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.
Wajumbe mbalimbali waliohudhuria Kikao cha Tathmini ya Usikilizaji wa Mashauri ya Mahakama ya Rufani mkoani Arusha. Kikao hicho cha tathmini kilifanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Morogoro)







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni