Jumatano, 2 Septemba 2026

TMJA GEITA, BUKOBA WAIMARISHA UJIRANI MWEMA, USHIRIKIANO

Na MWANDISHI WETU-Mahakama, Geita

Tawi la Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Geita, tarehe 28 Agosti, 2026 lilipokea ugeni kutoka Tawi la TMJA Bukoba kwa lengo la kuimarisha ujirani mwema, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wanachama katika kutekeleza majukumu yao ya kimahakama na kijamii.

Ugeni huo uliwasili na kuongozwa na Mlezi wa Tawi la TMJA Bukoba, Jaji Mfawidhi, Mhe. David Patrick Ngunyale. Ugeni huo ulipokelewa na Mlezi wa Tawi la TMJA Geita, Jaji Mfawidhi, Mhe. Projestus Kahyoza.

Katika ziara hiyo, Majaji na Mahakimu kutoka matawi hayo walishiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na michezo, zikiwemo matendo ya huruma katika Hospitali ya Wilaya ya Geita, bonanza la michezo mbalimbali pamoja na chakula cha jioni.

Siku ya pili yake, yaani tarehe 29 Agosti, 2026 bonanza la michezo lilifanyika katika viwanja vya Geita Gold Mining Limited (GGML), likihusisha michezo mbalimbali, ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, mbio za yai na kijiko, kufukuza kuku  pamoja na mchezo wa karata.

Katika michezo hiyo, washiriki walionesha ushindani wa hali ya juu, huku wakidumisha mshikamano na urafiki. Bonanza hilo lililenga kutumia michezo kama fursa ya kujenga urafiki na mshikamano baina ya wanachama, kuimarisha afya na ustawi wa wanachama, pamoja na kuimarisha mahusiano ya kikazi na kikanda katika utendaji wa huduma za umma.

Baada ya kumalizika kwa shughuli za Bbonanza na kuagana na wageni kutoka Bukoba, tarehe 30 Agosti 2026, Tawi la TMJA Geita lilifanya Mkutano Mkuu wa Tawi katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Geita.

Mkutano huo ulilenga kujadili masuala mbalimbali yanayohusu utendaji wa chama, ustawi wa wanachama pamoja na namna ya kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli za kimahakama.

Akifungua Mkutano Mkuu huo, Mhe. Kahyoza alisisitiza umuhimu wa viongozi kuwa mstari wa mbele katika kuonesha mfano bora wa uongozi, ushirikiano na uwajibikaji.

Mhe. Kahyoza aliwataka viongozi kutanguliza maslahi ya chama na kuwa mfano katika kutekeleza majukumu yao, akieleza kuwa uongozi bora ni msingi wa kujenga chama imara chenye uwezo wa kuwahudumia wanachama wake kwa ufanisi.

Akitoa taarifa ya shughuli za chama, Katibu wa TMJA Geita, Mhe. Ally Mgomba, alisema kuwa tawi limeendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii kwa kushirikiana na Ofisi ya Mlezi wa Tawi.

Alisema TMJA Geita imekuwa ikitoa mchango na kuwafariji wanachama wakati wa misiba, kushiriki katika matukio ya furaha, pamoja na kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii zenye lengo la kuwasaidia watu wenye mahitaji.

Miongoni mwa shughuli hizo ni ziara katika Shule yenye Mahitaji Maalumu Bukoba, ziara katika Magereza ya Wilaya ya Chato, ziara za ujirani mwema kati ya matawi na kanda mbalimbali, ikiwemo Bukoba na Kigoma, pamoja na ziara ya utalii katika Mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML), iliyotanguliwa na shughuli za matendo ya huruma katika Hospitali ya Wilaya ya Geita.

Katika taarifa yake, Katibu huyo alieleza kuwa tawi limepata mafanikio mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa ushirikiano kati ya wanachama na uongozi wa tawi, pamoja na kuendelea kushirikiana katika kuwasaidia watu wenye changamoto na kushiriki katika matukio mbalimbali ya furaha ya wanachama.

Aidha, tawi limefanikiwa kuimarisha mfuko wake, kufanya ziara mbalimbali za kujenga mahusiano na ushirikiano na kupata tuzo mbalimbali kutokana na shughuli zake.

Pamoja na mafanikio hayo, Mhe. Mgomba alibainisha kuwa moja ya changamoto zinazolikabili tawi ni ushiriki mdogo wa wanachama katika mazoezi ya mwili. Alieleza kuwa hali hiyo inaweza kuathiri ushiriki wa wanachama katika shughuli za michezo na juhudi za kuimarisha afya na ustawi wao.

Kwa ujumla, ziara ya TMJA Bukoba pamoja na Mkutano Mkuu wa TMJA Geita imekuwa fursa muhimu ya kuimarisha ujirani mwema, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wanachama.

Aidha, shughuli hizo zimetoa nafasi kwa wanachama kubadilishana uzoefu, kujadili mafanikio na changamoto, pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha chama na ustawi wa wanachama wake.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Geita, Mhe. Projestus Kahyoza akiwakaribisha wageni kutoka Kanda ya Bukoba kushiriki hafla ya ujirani mwema.

Picha ya pamoja kati ya TMJA Geita na TMJA Bukoba baada ya kuwasili katika Mahakama Kuu Geita.


Wenyeviti wa TMJA Geita na Bukoba wakikabidhi baadhi ya sabuni na mafuta kwa Madakitari wa Hospitari ya Wilaya ya Geita.

Picha ya pamoja kati ya TMJA Geita na Bukoba katika mgodi wa madini wa Geita.

Timu ya mpira wa miguu ya Mahakama Kuu Geita (juu) ikiwa katika picha kabla ya kuanza mchuano na timu ya Mgodi wa Geita iliyopo hapo chini.


Timu ya kuvuta kamba kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo Bukoba ikivutana na Timu ya Mgodi wa Geita.


Uongozi wa TMJA Geita na Bukoba pamoja na Mgodi wa Geita ukiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Mahakama Kuu Bukoba baada ya kuwakabidhi kombe.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro.









Hakuna maoni:

Chapisha Maoni