Alhamisi, 3 Septemba 2026

WADAU WA MAHAKAMA MOSHI WAPATIWA MAFUNZO YA MFUMO WA e-CMS

 · Wafundishwa jinsi ya kupakua Nakala za Hukumu na mienendo ya mashauri kupitia mfumo huo

· Wasisitizwa juu ya matumizi ya TEHAMA

Na PAUL PASCHAL, Mahakama-Moshi

Wadau wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Moshi wamepatiwa Mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Ki-elektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) yaliyolenga kuwaelekeza juu ya upandishwaji wa mashauri, upakuaji wa taarifa mbalimbali za kimahakama kama upakuaji wa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri.

Mafunzo hayo ambayo yametolewa kwa Wadau kutoka Magereza, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Waendesha Mashtaka wa Serikali yamefanyika leo tarehe 03 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mdogo wa mikutano wa Mahakama Kuu Moshi.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Moshi, Mhe. Sekela Mwaiseje na mada kuu ikiwasilishwa na Ofisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Moshi, Bi Catherine Mugyabuso.

Akizungumza wakati ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Mwaiseje alisisitiza juu ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa ajili ya kusaidia uendeshaji wa shughuli za Kimahakama kwa haraka na weledi katika kurahisisha upatikanaji wa taarifa za mashauri kama vile upatikanaji wa nakala za hukumu na mienendo ya shauri kwa haraka na kwa unafuu kupitia Mfumo wa e-CMS ili kuepuka malalamiko yasiyo ya lazima kutoka kwa Mahabusu au Wafungwa.

“Ndugu washiriki tumewaita hapa leo ili kuwaongezea maarifa kidogo juu ya maboresho yaliofanyika na yanaoendelea kufanywa na Mahakama ya Tanzania katika kuhakikisha ufanisi na weledi katika jukumu zima la utoaji haki nchini kupitia mifumo yetu ya kimahakama huduma zetu zimeboreka na kurahisishwa ili kuondoa malalamiko kwa wote tunaowahudumia,” amesema Mhe. Mwaiseje.

Amewaeleza washiriki hao wa mafunzo kuwa, wao kama Wadau muhimu wa Mahakama katika kuwahudumia Watanzania ni vema nao wakapata ujuzi na kuwa na uelewa wa pamoja katika matumizi ya mfumo huo wa e-CMS.

Ameongeza kuwa, mfumo huo unaosimamia Mashauri Mahakamani    unalenga kuimarisha utoaji haki mapema ipasavyo na kwamba kupitia mfumo huo  kwa upande wa Mahakama Kuu Moshi kwa sasa  haitumii karatasi kupata nakala za hukumu na mwenendo wa shauri bali zinapatikana kupitia kwenye mfumo.

Mshiriki Suzan Kimaro ambaye ni Ofisa Mpelelezi Mkuu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kilimanjaro ameushukuru uongozi wa Mahakama Kuu Moshi kwa maandalizi mazuri ya mafunzo hayo yanayokwenda kuwajenga na kuwaongezea uwezo wa ufanisi katika kutimiza majukumu yao.

“Kwa niaba ya Washiriki wote nipende kuishukuru Mahakama kwa mafunzo haya kwani yametupa mwanga mzuri wa namna ambavyo tunaweza kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi na weledi kupitia mfumo huu wa e-CMS hii itatusaidia sana kuwahudumia wananchi kwa haraka na pasipo na malalamiko yasio ya msingi,” amesema Bi. Suzan.

Washiriki kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) Moshi, Magereza na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kilimanjaro kwa pamoja wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa wakati wa mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Moshi leo tarehe 03 Septemba, 2026.

Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Moshi, Mhe.Sekela Mwaiseje akieleza akifungua mafunzo hayo na kueleza lengo la kufanyika kwa mafunzo hao kwa washiriki walioalikwa (hawapo katika picha).

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Moshi, Mhe. Opportuna Kipeta (aliyevaa miwani) pamoja na Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Mhe. Herrieth Mhenga (kulia) wakifuatilia mafunzo hayo.

Ofisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Moshi, Bi. Catherine Mugyabuso akitoa Mada kwa washiriki wa Mafunzo kuhusu matumizi wa e-CMS (hawapo katika picha).


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Morogoro)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni