Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Njombe, wamepatiwa mafunzo ya siku moja kuhusu namna ya kujikinga na majanga ya moto pamoja na kuchukua tahadhali dhidi ya moto mahali pa kazi na nyumbani.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Njombe yalifunguliwa na ASF. Bw. Bahati Mkutani tarehe 03 Septemba, 2026 na kuhudhuriwa na Viongozi pamoja na Watumishi wa Mahakama hiyo.
Akitoa mafunzo hayo, Ofisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ZMK-FC Bi. Blandina Kayuya, alieleza kuhusu vifaa vya awali vya kuzimia moto, ikiwemo (portable fire extinguishers) za aina mbalimbali kama vile poda, povu na gesi ya kaboni dioksidi, pamoja na (fire blanket).
Bi. Kayuya alisema kuwa, miongoni mwa mambo yanayoweza kumfanya mtu ashindwe kukabiliana na moto katika hatua za awali ni uwoga na kutokuwa na vifaa sahihi vya kuzimia moto.
Alisisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhali na kuwa na uelewa wa namna sahihi ya kutumia vifaa vya kuzimia moto ili kuhakikisha usalama wa watu na majengo dhidi ya majanga ya moto.
Akieleza hatua za kuchukua mtu anapogundua moto, Bi. Kayuya alisema; “moto unapotokea mtu hushindwa kuukabili kutokana na uwoga, unatakiwa ufanye yafuatayo pindi unapogundua moto: piga king’ora na yowe, piga simu ya bure Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kupitia namba 114, watu wasiojiweza wapewe kipaumbele kutoka eneo hatarishi, na jaribu kuzima moto bila kuhatarisha usalama wako na watu wengine.”
Aidha, alieleza kuwa vyanzo vikuu vinavyoweza kusababisha majanga ya moto ni pamoja na hitilafu za umeme, uzembe jikoni, uvutaji wa sigara, hujuma na uhalifu, pamoja na matukio ya asili kama vile radi.
Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Njombe, Mhe. Victoria Nongwa, baada ya kushiriki mafunzo ya nadharia na vitendo kuhusu namna ya kuzima moto, alilishukuru Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kutoa mafunzo katika Mahakama hiyo.
Mhe. Nongwa aliwaalika tena Maofisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufika katika Mahakama hiyo kutoa mafunzo zaidi watakapopata nafasi, huku akiwashukuru Viongozi na Watumishi wote walioshiriki katika mafunzo hayo.
Mafunzo hayo, yaliyotolewa kwa ushirikiano na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Njombe, yalihusisha vipindi vya nadharia na vitendo.
Mafunzo hayo yaliwajengea watumishi uelewa kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya kuzimia moto, namna ya kukabiliana na moto ukiwa katika hatua za awali, kutambua aina mbalimbali za moto na njia sahihi za kuukabili, pamoja na mbinu za kujiokoa pindi moto unapotokea.
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Njombe, wakishiriki mafunzo ya vitendo kuhusu namna ya kuzima moto na kujikinga na majanga ya moto. Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 03 Septemba, 2026.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni