- Jaji Maghimbi aongoza sherehe hiyo
- Jaji Mstaafu Butamo akiri kuwa amejifunza mengi Mahakamani ikiwemo ushirikiano
- Awasisitiza Majaji, Mahakimu na Watumishi wote wa Mahakama kwa ujumla kuzingatia afya
Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi ameongoza sherehe ya kumuaga kitaaluma Mhe. Butamo Kasuka Phillip baada kustaafu utumishi wa Mahakama kwa mujibu wa sheria.
Sherehe hiyo ilifanyika tarehe 02 Oktoba, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Dar es Salaam ambapo Jaji Maghimbi aliambatana na Majaji wa Kanda hiyo pamoja na wa Mahakama Divisheni za Biashara, Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Kazi, Usuluhishi pamoja na Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia (IJC)-Temeke.
Akiongoza hafla hiyo ya Kitaaluma, Mhe. Maghimbi alirejea nukuu ya madai na. 01/2026 katika suala la kitaaluma la kumuaga Mhe. Butamo. Kwa kuanzisha nukuu hiyo alimtaka Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na wa Kujitegemea kuridhia kuanza kwa nukuu hiyo ambapo Wakili Mkuu alitoa hotuba yake na kisha kufuatiwa na Wakili wa Kujitegemea na baadaye hotuba ya Jaji Muagwa Mhe. Butamo ambapo baada ya hotuba hizo ilifuatia na hitimisho la hotuba ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Elizabeth Mkwizu.
Baada ya hotuba zote hizo Jaji Maghimbi aliwauliza kama wana pingamizi juu ya yote yaliyowasilishwa katika nukuu hiyo, na kuonekana kutokuwa na pingamizi kutoka pande zote. Ndipo Mhe. Maghimbi alitoa tamko la kuridhia kustaafu kwa Jaji Butamo.
Katika hotuba yake, Mhe. Butamo ambaye ameagwa kitaaluma alisema kuwa, aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu mnamo mwaka 2018 akitokea Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira alipokuwa Naibu Katibu Mkuu.
Baada ya kuteuliwa na kuapishwa kuwa Jaji kituo chake cha kwanza kilikuwa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara- Dar es Salaam na baadaye kuhamishiwa Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Arusha na mwaka 2023 alihamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambapo ametumika hapo mpaka muda wake wa kustaafu ulipofika.
Jaji Butamo amewashukuru Majaji aliofanya nao kazi kwa upendo waliomuonyesha kwa kipindi chote alipokuwa kazini.
Jaji Butamo amesema katika utumishi wake katika Mhimili wa Mahakama kuna mambo manne ambayo alijifunza ikiwa ni pamoja na kuwa kazi ya kutoa haki ni kazi muhimu sana na si kazi rahisi.
Amesema kwamba kazi hiyo ni kazi ya Mwenyezi Mungu, Majaji na Mahakimu katika ngazi mbalimbali wanakasimishwa tu na Mwenyezi Mungu ambaye ndiyo mwenye haki iliyokamilika.
“Ni kweli kwamba wadaawa na wateja wote wanaofika Mahakamani wanaujua ukweli kuliko Jaji au Hakimu hapo ndipo ugumu wa kazi hii ulipo kwa sababu wakati mwingine wadaawa wanakwepa kusema ukweli wanamuweka Jaji au Hakimu kwenye mtihani wa kung’amua ukweli,” alisema Mhe. Butamo.
Ameongeza kuwa, amejifunza uvumilivu na umakini katika kutekeleza jukumu la utoaji haki, amesema katika kusikiliza mashauri mbalimbali Jaji anapokea watu wa aina nyingi na tofauti kwa maana ya elimu zao, uwezo wao wa kujieleza, maisha yao, changamoto zao, umri na kadhalika, kwahiyo; Jaji au Hakimu anapaswa kuwa mvumilivu na makini kuwasikiliza wadaawa na asipofanya hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kutoa uamuzi usio wa haki.
Amesema pia, bidii katika kutekeleza majukumu ni moja ya funzo alilolipata akiwa Jaji amesema kazi ya Ujaji inahitaji bidii kubwa kwa sababu ni kazi ambayo inataka Jaji atumie asilimia kubwa ya muda wake kuifanya, ambapo ameeleza kuwa, “asilimia kubwa ya Majaji kama sio wote wanafanya kazi ofisini na wakitoka ofisini wanabadili tu eneo la kazi, wanakwenda kuendelea na kazi majumbani mwao.”
Kitu kingine Jaji Butamo alichojifunza ni ushirikiano
mzuri uliopo katika Mhimili wa Mahakama, ameeleza kuwa, Majaji na Mahakimu
wanashirikiana katika utendaji wa kazi Jaji au Hakimu akiuliza jambo lolote
anapewa msaada haraka na wenzake ili asikosee, amesema katika utumishi wake
hakuwahi kuomba msaada wa Majaji wenzake katika kutekeleza majukumu yake
akaachwa kupewa anaamini ushirikiano huo utaendelea.
Vilevile amewashauri na kuwakumbusha Majaji, Mahakimu na Watumishi wote wa Mahakama kujali na kuangalia sana afya zao, amesema mazoezi ni muhimu kwa afya ya mwili, akili na roho.
Amesisitiza kuwa, pamoja na kazi nyingi ni vema wajiwekee ratiba ya mazoezi binafsi au ya kikundi kama inawezekana, amesema uwepo wa michezo (bonanza) zinazoratibiwa na Mahakama ni jambo jema sana kwa afya ya watumishi wa Mahakama.
Amewaomba Mahakama iangalie uwezekano wa kuwa na utaratibu rasmi wa mazoezi katika kila Kanda ya Mahakama Kuu ambapo watumishi watakuwa huru kushiriki mazoezi hayo. Amesema utendaji bora wa kazi unaambatana na uwepo wa afya nzuri kwa watumishi husika.
Amekumbusha pia kwamba, umoja wa Mataifa umeweka tarehe 25 ya mwezi Julai ya kila mwaka kuwa ni Siku ya kukumbushana juu ya afya ya Majaji na Mahakimu (International day on Judicial Well-Being) na katika Mkutano wa mwaka huu wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Jumuiya ya Madola (CMJA) uliofanyika Kingston nchini Jamaica, kulikuwa na kipindi maalum juu ya mjadala wa afya za Majajai na Mahakimu (Judicial Wellness, Mental and Physical Health) hii inaonesha ni kwa kiasi gani suala la kuzingatia afya za Majaji na Mahakimu lilivyo muhimu.
Akizungumza katika sherehe hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ya Dar es Salaam, Mhe. Elizabeth Mkwizu amezungumzia urithi wa Jaji Mstaafu, Mhe. Phillip Kasuka Butamo ambao katika Mahakama hawezi kuacha kuutaja ni mchango wake katika maendeleo na ujenzi wa misingi ya sheria (jurisprudence) kupitia maamuzi yake, katika shauri la Josephat Muniko dhidi ya North Mara Gold Mine Ltd (Commercial Case 9 of 2019) [2020] TZHCCOMD 22(30 March 2020).
Mhe. Mkwizu amesema kuwa, Mhe. Butamo alitoa ufafanuzi muhimu kuhusu wakati ambao kiini cha kosa (cause of action) inaweza kuchukuliwa kuwa ime-‘accrue’, pale ambapo mkusanyiko wa mapato au gharama (accrual) ya madai inategemea taarifa ambayo mlalamikaji hakuwa nayo.
Mchango mwingine unaoonesha msisitizo wake katika kujenga misingi ya sheria unapatikana katika shauri la Thinamy Entertainment limited na wengine dhidi ya Dino Katsapas (Misc.Commercial Case No. 86 of 2018) [2019] TZHC 16415. (24Spril 2019) katika uamuzi huo Mhe. Butamo alieleza kuhusu uthibitisho wa malipo ya ada za uwakili kwa kutumia risiti za (Electronic Fiscal Device (EFD) akisisitiza umuhimu wa uthibitisho huo katika kuthibitisha madai ya gharama za uwakili.
Akionesha mifano mingi ambayo Jaji Butamo ameacha kama alama katika taaluma ya sheria, amesema pia ni Mwalimu hata kama hafundishi darasani lakini kila hukumu anayoandika ni somo kila hoja anayojadili ni somo kila uamuzi anaofanya ni somo kwa kizazi kinachofuata.
“Kwa hiyo tunaposema Jaji Butamo amestaafu, tunapaswa kutambua kwamba Mwalimu hajastaafu taaluma bado inamuhitaji vijana bado wanamuhitaji Mahakama bado inahitaji uzoefu wake na jamii bado inaweza kunufaika na busara yake,” alisema Jaji Mkwizu.
Mhe. Mkwizu aliongeza kuwa, wanamuaga Mhe. Butamo katika nafasi ya Ujaji lakini hawamuagi katika maisha yao, anatoka kwenye kiti cha Mahakama, lakini haondoki katika familia ya Mahakama kwa kuwa uzoefu wake ni hazina ambayo haiwezi kustaafu.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Madai ya Ndani (Assistant Domestic Litigation) kutoka katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Wakili Deodatus Nyoni katika nukuu ya Madai Na. 01/2026 katika suala la taaluma na kumuaga Mhe. Butamo alisema Jaji Mstaafu huyo atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa kupitia jukumu hilo ni wazi kuwa mchango wake hauwezi kuelezeka kwa mistari michache isipokuwa tu kuonesha baadhi ya mashauri ambayo ni mifano ya mashauri mengi aliyowahi kutolea maamuzi.
Katika shauri la Alnassir Rajabali dhidi ya Mathias Kanuti Lazaro (Civil Appeal No.28162 of 2025) [2026] TZHC 2929 (29 May 2026) uamuzi ya shauri hilo umetambua mawasiliano mbalimbali kama moja ya uthibitisho wa uwepo wa makubaliano baina ya wadaawa ambao hawana Mkataba wa kimaandishi. Mahakama ilitambua kwamba jumbe zinazotumwa katika simu au mitandao ya kijamii (WhatsApp) ni makubaliano halali. Maamuzi hayo yanaendana sambamba na maendeleo ya Kiteknolojia ambapo katika karne hii matumizi mbalimbali ya mawasiliano yamekua yakitumika katika kufikia makubaliano katika kazi na biashara mbalimbali.
Wakili Nyoni amesema pia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inatambua mchango mkubwa wa Mhe. Butamo katika kutenda haki kupitia maisha yake ambayo yanadhihirika hususan katika maamuzi na hukumu mbalimbali alizowahi kutoa.
Amesema, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inatambua na kuenzi mchango wake mkubwa katika kusimamia nidhamu za Mawakili kwa Mahakama na wateja wao. Na kila wakati alikuwa kinara katika kuhakikisha kuwa, Wakili akiwepo Mahakamani anatambua wajibu wake na kuzingatia misingi na taratibu za kimahakama.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Kanda ya Mzizima na Mjumbe wa Baraza la Uongozi TLS, Wakili Ipilinga Panya amemkaribisha Mhe. Butamo TLS baada ya kustaafu utumishi wa Mahakama kwa kusema anapofunga sura hiyo ya utumishi wa Mahakama anaamini kwamba kazi zake, michango yake na kumbukumbu ya huduma yake kwa Taifa vitaendelea kuwa sehemu ya historia ya mfumo wa haki nchini Tanzania.
Amemkaribisha katika Chama hicho ambapo amesema, atapata fursa ya kuendeleza elimu ya Mawakili vijana (Young Lawyers) kwa kushirikiana na Majaji Wastaafu, Wasajili wa Mahakama Wastaafu na Mahakimu Wastaafu ambao ni sehemu muhimu ya TLS.
Mhe. Butamo Kasuka Phillip, Jaji Mstaafu alizaliwa tarehe 10 Agosti, 1966 Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga na kupata elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi Town mkoani humo na elimu ya Sekondari aliipata katika Shule ya Sekondari Buluba iliyopo mkoani Shinyanga na baadae elimu ya Sekondari ya Juu aliipaata Shule ya Wasichana Tabora (Tabora Girls).
Mnamo mwaka 1992 alihitimu Shahada ya Sheria (Bachelor of Laws) na kufanya kazi mbalimbali katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano na baadaye mwaka 2018 aliteuliwa na kuapishwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Sherehe hiyo ilihudhuriwa na Naibu Wasajili, Watendaji, Mahakimu, Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea na Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Baadhi ya Mahakimu waliohudhuria Sherehe ya Kuagwa Kitaaluma kwa Mhe. Butamo Kasuka Phillip iliyofanyika tarehe 02 Oktoba, 2026 Mahakama Kuu Dar es Salaam.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji waliohudhuria Sherehe ya Kumuaga Kitaaluma Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Butamo Kasuka Philip (wa tatu kushoto). Wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga, wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma, wa kwanza kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Sharmillah Sarwatt, wa tatu kulia ni Jaji wa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo na wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Elizabeth Mkwizu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu waliohudhuria Sherehe ya Kumuaga Kitaaluma Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Butamo Kasuka Philip (wa tatu kushoto). Wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga, wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma, wa kwanza kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Sharmillah Sarwatt, wa tatu kulia ni Jaji wa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo na wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Elizabeth Mkwizu.
Meza Kuu pamoja na Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Wakili wa Kujitegemea kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) walioshiriki Sherehe ya Kuagwa Kitaaluma kwa Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Butamo Kasuka Philip iliyofanyika tarehe 02 Oktoba, 2026 Mahakama Kuu Dar es Salaam.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama waliohudhuria Sherehe ya Kumuaga Kitaaluma Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Butamo Kasuka Philip (wa tatu kushoto) iliyofanyika tarehe 02 Oktoba, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Dar es Salaam. Wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga, wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma, wa kwanza kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Sharmillah Sarwatt, wa tatu kulia ni Jaji wa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo na wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Elizabeth Mkwizu.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Zanzibar)













Hakuna maoni:
Chapisha Maoni