Jumapili, 4 Oktoba 2026

MAHAKAMA YA NJOMBE YAKETI KUJADILI UBORESHAJI WA HUDUMA ZA HAKI KWA WANANCHI

  • Yajadili mikakati ya kukabiliana na athari za Mvua za El Nino

Mahakama ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe imefanya Kikao cha Menejimenti tarehe 01 Oktoba, 2026 kwa lengo la kujadili namna ya kuboresha utoaji wa huduma za haki kwa wananchi, kupitia utekelezaji wa majukumu yake pamoja na kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utoaji wa huduma za kimahakama kwa ujumla.

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Njombe, kiliongozwa na Jaji Mfawidhi wake, Mhe. Victoria Nongwa.

Katika kikao hicho, wajumbe walipitia taarifa mbalimbali za kiutendaji, ikiwemo mwenendo wa mashauri, utekelezaji wa mipango kazi, matumizi ya rasilimali pamoja na changamoto zinazohitaji hatua za pamoja ili kuendelea kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Nongwa aliwataka Mahakimu Wafawidhi wa Wilaya zote kuwasimamia kikamilifu Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na Maofisa mbalimbali wa Mahakama ili waendelee kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Aidha, aliwahimiza watumishi kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika uendeshaji wa mashauri, hususan pale ambapo mashahidi wanapatikana maeneo ya mbali na vituo vya Mahakama. Pia alisisitiza umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi za mashauri kupitia mfumo wa kuhifadhi Takwimu (Datahub), unaotumika katika usimamizi wa takwimu za mashauri Mahakamani.

Mhe. Nongwa pia alizungumzia hali ya baadhi ya Mahakama za Mwanzo ambazo hazitoi huduma licha ya kuwepo katika Wilaya husika. Alitaja Mahakama za Mwanzo za Igominyi na Mtwango zilizopo Wilaya ya Njombe pamoja na Mahakama ya Mwanzo ya Mavanga iliyopo Wilaya ya Ludewa. Aliwaagiza Viongozi wa Mahakama Njombe kuchukua hatua za kuhakikisha vituo hivyo vinawezeshwa na kuanza kutoa huduma, kwa lengo la kusogeza huduma za haki karibu zaidi na wananchi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Nongwa alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na umoja miongoni mwa watumishi wa Mahakama, pamoja na matumizi sahihi ya rasilimali zilizopo ili kufikia malengo yaliyowekwa katika Mpango Mkakati wa Mahakama.

Alisisitiza pia umuhimu wa ushirikishwaji wa Wadau pamoja na utoaji wa elimu ya sheria kwa wananchi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kutumia kumbi za Mahakama na vipindi vya redio ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Naye, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano alitoa mwongozo kuhusu usimamizi wa mashauri ya mlundikano (case backlog).

Mhe. Luambano alielekeza kuwa; kila shauri linaloingia katika kundi la mashauri ya mlundikano liwe na maelezo yanayoeleza sababu ya kuchelewa kwake, kwa mfano shauri kurejeshwa katika Mahakama ya chini kwa ajili ya kusikilizwa upya au Mahakama kutokuwa na mamlaka ya kulisikiliza.

Aidha, Mhe. Luambano alitoa maelekezo mbalimbali kuhusu utekelezaji wa mrejesho uliotokana na ukaguzi uliofanyika hivi karibuni chini ya Uongozi wa Jaji Mfawidhi, Mhe. Nongwa. Alisistiza kuwa; tayari yameshaandaliwa mafunzo kwa Maofisa wa Mahakama katika maeneo yenye changamoto ikiwemo utoaji adhabu mbadala, huduma kwa mteja, pamoja na uendeshaji wa mashauri ya utekelezaji.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, Bw. Richard Mbambe ambaye pia alikuwa Katibu wa kikao hicho, aliwataka Maofisa wa Mahakama katika Wilaya mbalimbali kuhakikisha wanatafuta maeneo/viwanja na hati miliki kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo.

Bw. Mbambe alisema kwamba; maandalizi hayo ni muhimu kwa kuwa Mahakama inaweza kupata wadau au wafadhili watakaosaidia katika ujenzi wa miundombinu ya Mahakama hizo. Hivyo, upatikanaji wa viwanja vyenye hati unapaswa kupewa kipaumbele.

Aidha, Bw. Mbambe alizipongeza Mahakama zinazoendelea kununua na kuboresha vifaa vya TEHAMA, huku akisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za Mahakama.

Katika kikao hicho pia, Bw. Mbambe alijadiliana na wajumbe kuhusu namna ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za   El Nino katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Alisisitiza umuhimu wa kuanza maandalizi mapema, hususan katika kulinda miundombinu ya Mahakama pamoja na makazi ya watumishi, kutokana na uwezekano wa mvua kubwa zinazoweza kusababisha uharibifu wa miundombinu na mali.

Wajumbe wa kikao hicho walijadili pia mikakati mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za Mahakama, ikiwemo kuhakikisha mashauri yanashughulikiwa mapema ipasavyo na wananchi wanapata huduma kwa haki, usawa na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Kikao hicho ni sehemu ya utaratibu wa menejimenti wa kufuatilia utekelezaji wa majukumu na mipango ya Mahakama, kutathmini mafanikio na changamoto zilizopo, pamoja na kuweka hatua stahiki za kuboresha utendaji katika kipindi kijacho.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa, Naibu Msajili, Mhe. Joseph Luambano, Mtendaji wa Mahakama Kuu Njombe, Bw. Richard Mbambe, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama, Mahakimu Wafawidhi/Wawakilishi wa Wilaya za Ludewa, Makete na Wanging’ombe, pamoja na Maofisa mbalimbali wa Mahakama Njombe.


Meza kuu ikiongozwa na Jaji   Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa (katikati) wakiwa katika Kikao cha Menejimenti kilichofanyika tarehe 01 Oktoba, 2026. Aliyeketi kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama   Kuu   Njombe,   Mhe. Joseph Luambano na kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Njombe, Bw. Richard Mbambe. Mbele yao ni sehemu ya wajumbe wa kikao hicho wakimsikiliza kwa makini  Ofisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya Njombe, Bw.Barnaba Fussi    (aliyesimama wa kwanza kushoto) alipokuwa akisoma taarifa. Anayefata ni Ofisa TEHAMA, Bw.Fadhili Lwena.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano akitoa mada mbele ya wajumbe wakati wa Kikao cha Menejimenti kilichofanyika tarehe 01 Oktoba, 2026.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Liadi Chamshama (aliyeketi mbele) akichangia jambo wakati wa kikao hicho. Aliyeketi kiti cha nyuma yake wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ludewa, Mhe. Isack  Ayengo na anayefuata ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Makete, Mhe. Irvan Msacky na wa mwisho kiti cha nyuma ni Ofisa Fundi Sanifu kwa pamoja wakisikiliza kwa makini mada iliyokuwa inachangiwa.

  Ofisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe, Bw. Riziki Sanga akichangia mada wakati wa kikao hicho. Wengine walioketi ni sehemu ya Wajumbe wa Kikao cha Menejimenti cha Mahakama Njombe wakimsikiliza kwa umakini.
 


 Aliyesimama ni Kaimu Ofisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya ya  Ludewa, Mhe.Bornfast Humbo akisoma moja ya ajenda ya kikao hicho mbele ya Viongozi wa Mahakama Kuu Njombe ambao wanafuatilia kwa umakini wengine nyuma yake ni sehemu ya wajumbe wa kikao hicho cha Menejimenti. 


 Ofisa Bajeti  wa Mahakama wa Kuu Masjala Ndogo ya Njombe, Bw. Juma Nyenzi  akisoma   akiwasilisha taarifa ya bajeti  mbele ya Viongozi wa Mahakama Kuu Njombe (hawapo katika picha) wengine wakimsikiliza ni sehemu ya Wajumbe wa Kikao cha Menejimenti wakifuatilia kwa umakini.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Zanzibar)

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni