Jumatano, 28 Oktoba 2026

MAHAKAMA KUU YA TANZANIA, MASJALA NDOGO SINGIDA YAENDELEA KUIMARISHA UTOAJI HAKI

  • Mahakimu waaswa kulinda viapo vyao
  • Mahakimu, madalali na wasambaza nyaraka wa Mahakama wabadilishana uzoefu.

Na EVA LESHANGE & AMIRI BAKARI, Mahakama – Singida

Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma za haki kwa kuwakutanisha Mahakimu, Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama katika vikao vya kitaaluma vinavyolenga kuongeza weledi, uwajibikaji na uzingatiaji wa sheria katika utendaji wa kazi.

Katika mwendelezo wa juhudi hizo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Mhe. Ayoub Mwenda amewataka Mahakimu mkoani Singida kusimamia ipasavyo viapo vyao vya kazi, kuzingatia maadili ya taaluma na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu wa hali ya juu ili kuendelea kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama.

Akizungumza na Mahakimu wa Singida wakati wa kikao hicho kilichofanyika tarehe 23 Oktoba, 2026, Mhe. Mwenda alisema kuwa, kila Hakimu anapaswa kuthamini na kulinda kiapo alichopata wakati wa kuapishwa na kuhakikisha kuwa, hakuna mazingira yanayoweza kuathiri misingi ya taaluma, maadili na utoaji haki.

Aidha, amewakumbusha kuwa, yapo mambo yanayoonekana kuwa madogo katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku, lakini yanaweza kuathiri taswira ya Mahakama na kupunguza imani ya wananchi kwa mfumo wa utoaji haki. Kutokana na hali hiyo, aliwasisitiza kujiepusha na vitendo vyovyote vinayoweza kuibua shaka kuhusu uadilifu, weledi na kutokuwa na upendeleo katika utendaji wao.

"Tunapaswa kushirikiana na jamii tunayoihudumia, lakini katika kufanya hivyo ni lazima tuheshimu viapo vyetu vya kazi na kuzingatia maadili ya taaluma ya sheria ili kulinda hadhi ya Mahakama na kuimarisha imani ya wananchi," alisisitiza.

Vilevile, aliwataka Mahakimu hao kuepuka kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kuhakikisha kuwa, kila jukumu linatekelezwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

 Alibainisha kwamba, utoaji wa huduma bora kwa watumiaji wa huduma za Mahakama ni nguzo muhimu katika kujenga imani ya wananchi na kuhakikisha upatikanaji haki kwa wote na mapema ipasavyo.

Sambamba na msisitizo huo wa kuzingatia maadili na weledi wa kazi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Singida, imeendesha kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu utekelezaji wa hukumu, wajibu wa Madalali wa Mahakama na usambazaji wa nyaraka za Mahakama.

Kikao hicho kiliwakutanisha Mahakimu, Madalali wa Mahakama pamoja na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa hukumu na usambazaji wa nyaraka za Mahakama sambamba na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bora za utekelezaji wa majukumu hayo.

Akifungua kikao hicho, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Mhe. Evodia Kyaruzi alisema kuwa, kubadilishana uzoefu ni fursa muhimu inayowezesha washiriki kujifunza kutoka kwa wenzao, kubaini changamoto zilizopo na kupata suluhisho litakalosaidia kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Alisisitiza kuwa, utekelezaji wa hukumu ni moja ya hatua muhimu katika mchakato wa utoaji haki na unahitaji umakini mkubwa kwa kuwa una athari ya moja kwa moja katika imani ya wananchi kwa Mahakama.

"Sehemu mojawapo inayotakiwa kufanyika kwa umakini mkubwa ni utekelezaji wa hukumu. Tusipokuwa makini kwenye utekelezaji wa hukumu tunaweza kupoteza imani ya wananchi kwa Mahakama," alisema.

Washiriki wa kikao hicho walijadiliana pia juu ya changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa hukumu na usambazaji wa nyaraka za Mahakama huku wakishauriana kuhusu namna bora ya kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakimu, Madalali wa Mahakama pamoja na Wasambaza Nyaraka ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akifunga kikao hicho, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Singida, Mhe. Fadhili Luvinga aliwashukuru washiriki wote kwa kujitokeza na kushiriki kikamilifu, huku akieleza kuwa, ushiriki wao umeonesha dhamira ya kujifunza, kujiongezea maarifa na kuboresha utendaji kazi.

"Ushiriki wenu umeonesha kwamba tunapenda kujua na kujifunza zaidi. Ni muhimu kuendelea kuwa na vikao vya aina hii mara kwa mara ili kutukumbusha wajibu wetu na kuongeza uelewa wa masuala mbalimbali," alisema Mhe. Luvinga.

Alisisitiza juu ya umuhimu wa kuendelea kusoma sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayosimamia utekelezaji wa majukumu ya Mahakama ili kuongeza maarifa, kuimarisha utendaji kazi na kuhakikisha utoaji bora wa huduma za haki kwa wananchi.

Kwa ujumla, kikao hicho kimetoa fursa kwa washiriki kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu bora za kazi na kuimarisha uelewa kuhusu wajibu wao katika kuhakikisha hukumu za Mahakama zinatekelezwa kwa usahihi, ufanisi na kwa kuzingatia sheria, hatua ambayo ni muhimu katika kuendelea kujenga na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama.


Mahakimu, Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa Kikao cha Kubadilishana Uzoefu Kuhusu Utekelezaji wa Hukumu, Wajibu wa Madalali wa Mahakama na usambazaji wa nyaraka za Mahakama kilichofanyika tarehe 23 Oktoba, 2026 katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Singida.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Singida, Mhe. Jaji Ayoub Mwenda (kushoto), pamoja na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Singida, Mhe. Evodia Kyaruzi (kulia) wakishiriki katika kikao cha kubadilishana uzoefu. Kikao hicho kiliwakutanisha Mahakimu, Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama wa mkoani Singida.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, akichangia mada katika kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu utekelezaji wa hukumu, wajibu wa Madalali wa Mahakama na usambazaji wa nyaraka za Mahakama, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Singida.

Dalali wa Mahakama, Bw.William Mirumbe akichangia mada na kushiriki majadiliano kuhusu utekelezaji wa hukumu, wajibu wa Madalali wa Mahakama na usambazaji wa nyaraka za Mahakama wakati wa kikao cha kubadilishana uzoefu kilichofanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Singida.

Baadhi ya Washiriki wa Kikao cha Kubadilishana Uzoefu kuhusu Utekelezaji wa Hukumu, Wajibu wa Madalali wa Mahakama na usambazaji wa nyaraka za Mahakama wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuhitimika kwa kikao hicho kilichofanyika kwenye moja ya kumbi za Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Singida. 

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



 



 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni