Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya
Mahakama ya Rufani ya Tanzania inatarajia kuendesha Kikao cha usikilizaji wa mashauri 38 ya rufaa za Madai na Jinai katika kikao kitachoendeshwa Masjala Ndogo ya Mbeya kuanzia tarehe 05 Oktoba, 2026 hadi tarehe 30 Oktoba, 2026.
Kikao hicho kitaendeshwa na Jopo moja la Majaji watatu (3) wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Zephrine Nyahuganda Galeba, Majaji wengine katika Jopo hilo ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Amour Said Khamis na Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Rabia Hussein Mohamed.
Akiwasilisha taarifa katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Mbeya, ambacho ni kikao cha maandalizi (Pre- Session Meeting), Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Mhe. Abeesiza Kalegeya alieleza kuwa, jumla ya mashauri 38 ya Rufaa za madai na Jinai yamepangwa kusikilizwa katika Masjala Ndogo ya Mbeya, ambapo Rufaa za Madai ni 24, Rufaa za Jinai 13 na ombi ya Madai moja.
Aidha, Mhe. Kalegeya aliongeza kuwa, katika kuhakikisha ufanisi wa kikao hicho na kufikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa ratiba ya kikao ilitolewa kwa wakati na hati za kuitwa shaurini za wadaawa kwa ajili ya usikilizwaji wa mashauri zimesambazwa, na Mashauri 31 kati ya 38 yaliyopangwa wadaawa wote wameshapatikana.
Mhe. Kalegeya ameongeza kuwa, juhudi za kuwapata wadaawa ambao hawajapatikana zinaendelea ikiwa ni pamoja na kuwapigia simu wahusika ili kuhakikisha wanapata taarifa ya usikilizwaji wa mashauri yao kabla ya terehe ya usikilizwaji wa shauri husika, ambapo ni shauri moja (01) pekee ambalo wadaawa wote hawajapatikana na mashauri sita (06) amepatikana mdaawa mmoja mmoja kwa kila shauri.
Naye, Mwenyekiti wa kikao hicho, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Amour Said Khamis, alitoa pongezi kwa Mawakili kwa kufika kwa wingi katika kikao hicho na kuwaasa kuwatembelea wateja wao gerezani kabla ya mashauri kuanza kusikilizwa, huku akiwasisitiza kufika kwa wingi zaidi wakati wa usikilizwaji wa mashauri ya Rufaa kwa lengo la kujenga uzoefu juu ya mambo mbalimbali yanayoendelea wakati wa usikilizwaji wa mashauri mahakamani.
Aidha, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya, aliwasilisha ombi kwa Mwenyekiti wa kikao hicho Mhe. Khamis, kutoa ruhusa kwa Mahakimu na wale ambao wapo kwenye mafunzo kwa vitendo mahakamani na katika Ofisi Mbalimbali za Mawakili na Msaada wa kisheria kuingia mahakamani kwa lengo la kujiongezea ujuzi na maarifa zaidi.
Mwenyekiti wa kikao hicho aliridhia na kutoa ruhusa kwa watu hao kushiriki wakati wa usikilizwaji wa mashauri hayo, pia alitoa shukrani kwa wadau wote kwa kuitikia wito na kushiriki pamoja katika kikao hicho.
“Niwashukuru wadau wote kwa kuitikia wito na kushiriki nasi katika kikao
hiki, ni matarajio yetu kuwa, yale tuliyojadili na tunayokwenda kuyafanyia kazi
katika kikao hichi yatakuwa na tija kwetu sote na kutupa fursa ya kujijenga zaidi
katika utendaji kazi wa shughuli zetu za kila siku” Alisema Mhe. Khamis.
Kaimu Mwenyekiti wa Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Amour Said Khamis (kulia)
akiongoza kikao hicho cha awali cha maandalizi ya kikao cha Mahakama ya Rufani.
Kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Rabia Hussein Mohamed.
Naibu Msajili Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Abeesiza Kalegeya akiwasilisha taarifa ya Naibu Msajili
katika kikao hicho.
Sehemu ya wadau mbalimbali
walioshiriki katika kikao hicho
Sehemu ya wadau mbalimbali
walioshiriki katika kikao hicho
Mwenyekiti wa
Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Tanganyika (TLS) Chapta ya Mbeya Wakili Msomi
Philip Mwakilima akizungumza jambo katika kikao hicho.
Viongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya,
walishiriki kikao hicho ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya
Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (wa kwanza kulia), Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo
ya Mbeya Mhe. Angaza Mwipopo (wa pili kulia), Jaji wa Mahakama Kuu Masjala
Ndogo ya Mbeya Mhe. Said Kalunde (wa pili kushoto) na Jaji wa Mahakama Kuu
Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Mussa Pomo (wa kwanza kushoto).
Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania wakipokelewa na Waheshimiwa Majaji, Naibu Wasajili, Mahakimu na Watumishi wengine wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya mara baada ya kuwasili jijini Mbeya.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni