Alhamisi, 17 Septemba 2026

JAJI MRUMA AZITAKA TAASISI ZA MNYORORO WA HAKI KUZINGATIA KATIBA, SHERIA NA MAADILI

Na HALIMA MNETE, Mahakama-Dodoma

Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma ametoa rai kwa kila taasisi inayohusika katika mnyororo wa haki kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Katiba, sheria na maadili ya utumishi wa umma.

Mhe. Mruma ametoa rai hiyo leo tarehe 17 Septemba, 2026 alipokuwa akimkaribisha Mgeni Rasmi Jaji Mkuu kufungua Mkutano wa Mahakama na Wadau wa Haki Jinai kuhusu Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

“Kila Taasisi inayohusika katika mnyororo wa haki ina wajibu wa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Maadili ya utumishi wa umma” amesema Jaji Mruma.

Akifafanua nafasi ya Mahakama katika mnyororo wa haki amesema, “Ibara ya 107A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeelezwa kuwa, inaipa Mahakama nafasi ya kuwa mamlaka ya mwisho katika kuamua haki za wananchi, huku akisisitiza kuwa, utoaji wa haki si jukumu la Mahakama pekee, bali unahitaji ushirikiano wa taasisi zote zinazounda mnyororo wa haki.”

Kaimu Jaji Kiongozi huyo ambaye ameongeza kuwa, wajibu huo huanza tangu hatua za awali za utekelezaji wa sheria, ikiwemo ukamataji na upelelezi, uamuzi wa kuwasilisha mashtaka hadi shauri linapofikishwa Mahakamani na kuamuliwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Mhe. Mruma amesema kwamba, mkutano huo unalenga kufuatilia utekelezaji wa mikakati 10 iliyowekwa na Mahakama na wadau wa mnyororo wa haki katika vikao vilivyopita.

Aidha; ametaja mikakati iliyofikiwa na vikao Mahakama na Wadau hao, miongoni mwa mikakati hiyo ni kuhakikisha kila taasisi inatekeleza jukumu lake ipasavyo kwa kuzingatia Katiba, sheria na maadili ya utumishi wa umma; kuheshimu na kulinda hadhi na ukuu wa Mahakama; pamoja na kuimarisha mawasiliano miongoni mwa wadau ili changamoto za utoaji wa haki ziweze kushughulikiwa kwa haraka,” amesema Jaji Mruma.

"Mikakati hiyo pia inahusisha kuimarisha ufuatiliaji wa mashauri na uwajibikaji kupitia utoaji wa taarifa sahihi na za mara kwa mara, pamoja na matumizi ya mifumo inayoweza kuwasiliana ili kurahisisha mawasiliano baina ya taasisi," ameeleza.

Ametaja mkakati mwingine ni kuhakikisha vikao vya ushirikiano na mahusiano kati ya Mahakama na wadau vinafanyika angalau mara nne kwa mwaka, kwa lengo la kujadili changamoto na kufuatilia utekelezaji wa mikakati iliyowekwa.

Vilevile, kila taasisi inayoshiriki katika mnyororo wa haki imetakiwa kuweka utaratibu mahsusi na madhubuti wa ndani wa kuhakikisha mikakati hiyo inatekelezwa.

Kuhusu utatuzi wa migogoro, mkutano huo umeeleza umuhimu wa migogoro ambayo kwa mujibu wa sheria inapaswa kutatuliwa katika ngazi mbalimbali kwa njia ya madai au kiutawala kushughulikiwa kwanza katika ngazi husika badala ya kufunguliwa kama mashauri ya jinai moja kwa moja.

Hatua hiyo imehusishwa na dhana ya maridhiano, ambayo imeainishwa katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Criminal Procedure Act) kwa makosa yanayoweza kutatuliwa kwa njia hiyo.

Akielezea umuhimu wa mikakati hiyo, Mhe. Mruma amesema “jambo la msingi si idadi ya mikakati iliyowekwa, bali ni utekelezaji wake na matokeo yanayopatikana katika mnyororo wa haki jinai nchini.”

Mkutano huo unatoa fursa kwa Mahakama na wadau kutathmini walikotoka, walipo na wanakokwenda katika utekelezaji wa mikakati hiyo, sambamba na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na ushirikiano zaidi. Aidha, utekelezaji wa mikakati hiyo umehusishwa na Dira ya Taifa ya 2050, inayotambua haki kuwa msingi muhimu katika kujenga jamii yenye maendeleo na ustawi.

Kadhalika, Mkutano huo unatarajiwa kuendelea na majadiliano kuhusu changamoto mbalimbali zinazokabili mnyororo wa haki na namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama na wadau wake ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati, kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria.


Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma akitoa neno wakati wa Mkutano wa Mahakama na Wadau kuhusu Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani uliofanyika leo tarehe 17 Septemba, 2026 kwenye Ukumbi wa Mikutano Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza jambo wakati wa Mkutano wa Mahakama na Wadau kuhusu Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani uliofanyika leo tarehe 17 Septemba, 2026 kwenye Ukumbi wa Mikutano Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. 



Sehemu ya Wadau waliohudhuria 
Mkutano wa Mahakama na Wadau kuhusu Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani uliofanyika leo tarehe 17 Septemba, 2026 kwenye Ukumbi wa Mikutano Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. 

Sehemu ya Viongozi na Watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau wa Haki Jinai wakiwa katika picha ya pamoja. Katikati ni Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, aliyeketi kushoto ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma na kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)











 

 

JAJI MKUU AWAKUMBUSHA WADAU KUCHUKUA TAHADHARI MVUA ZA EL NINO

Na HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju ametoa rai kwa wadau wanaoshughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara kuchukua tahadhari na hatua madhubuti za kukabiliana na mvua za El nino kufuatia taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) juu ya uwepo wa mvua hizo kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu.

Mhe. Masaju ametoa ushauri huo tarehe 16 Septemba, 2026 alipokuwa akifunga Mkutano wa nne wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Akizungumza na Wadau hao, Mhe. Masaju amesema kuwa, Serikali inachukua hatua za kujikinga na kukabiliana na janga hilo hivyo, na wao wanapaswa kuchukua tahadhari kila mmoja na kutazama ni kwa namna gani wanaweza kuendeleza shughuli ikiwa mvua hizo zitakuwepo, pia kila mmoja kwa imani yake kumuomba Mwenyezi Mungu bila kusubiri kuambiwa na viongozi wa dini na pasipo kuringia kiburi cha uzima.

“Wadau wa haki mmejiandaa vipi, TLS mmeshaandaa namna gani ya kuendelea kusikiliza mashauri haya, wakati pengine njia barabarani hazifikiki, kwenye ‘Law fame’ zenu mna vyumba vya kutosha, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na wadau wengine humu tumejiandaa namna gani, hayo ndiyo ya kutafakari, sisi wenyewe kwenye sekta hii tuchukue hatua namna gani tutaendeleza shughuli zetu kama hilo janga litakuwepo, lakini pia na kumuomba Mwenyezi Mungu atukinge alitupilie mbali hilo janga, tusiwe na kiburi cha uzima, tuone kama Mungu yupo, maji yana nguvu Ghorofa hazisaidii kitu chochote,” amesema Jaji Mkuu.

Aidha, amesisitiza juu ya maombi huku akirejea Kitabu cha Zaburi 103, kama muongozo katika maombi ambayo itawawezesha wadau kuomba kwa yale ambayo yapo nje ya uwezo wao kuyadhibiti, basi Mwenyezi Mungu kwa rehema na fadhili zake aingilie kati na kuliepusha Taifa na janga hilo kwa sababu hakuna ambaye ana kinga ya uhakika ya kujiweka salama pindi janga hilo litakapotokea.

“Sisi wengine hatuna kinga ya kutofikiwa na hayo majanga ya elnino kama yatakuwepo, yapo mengine yapo nje ya uwezo wetu, na mimi naamini uwepo wa Mwenyezi Mungu, kila mmoja hapa hakuna ambaye anakinga ya kutokufa kwa majanga, kila mmoja achukue tahadhari na kumuomba Mwenyezi Mungu, lazima tuwe tayari kumuomba kwa rehema, neema na fadhili zake kwa mujibu wa Zaburi ya 103 ambayo tunaishi kwayo, anaweza kuingilia kati akatunusuru kwakuwa hata uwezo wetu wa kujikinga na hayo majanga ni mdogo,” ameongeza Mhe. Masaju.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amebainisha changamoto ambazo zinasababisha ucheleweshaji wa usikilizaji wa mashauri ya kiuchumi, ambazo amezitaja kuwa ni changamoto zinazotokana na Mahakama yenyewe, changamoto za kisheria na changamoto zinazotokana na wadau.

Amesema kuwa, changamoto zinazotokana na Mahakama yenyewe ni hasa zile za kisheria, ambazo zinaambatana na mfumo wa kitaasisi na kushauri kuwa wadau waendelee kubaini changamoto hizo na kuzijadili kwa pamoja ili kuzipatia ufumbuzi pale ambapo mhusika amekwama kuzitatua.

Amezitaja changamoto hizo kuwa ni ufunguaji wa mashauri kwa lengo la kuchelewesha ulipaji wa madeni, ambapo watu hufungua mashauri mahakamani ili wasiwajibike kulipa deni na kuongeza kuwa, kukiwa na riba rafiki na upatikanaji wa elimu hususan elimu ya mikopo na masuala ya bima watu watapata uelewa wa kutosha na kufahamu wajibu wao na namna gani wanawajibika.

Kadhalika, ameitaja changamoto nyingine kuwa, ni matumizi ya mbinu za kiufundi ili kuchelewesha usikilizaji na uamuzi wa mashauri, hali ya kuwa Katiba imetoa muongozo wa kutofungwa kupita kiasi na masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka akirejelea Ibara ya 107A(2)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, (1977).

“Matumizi ya mbinu za kiufundi ili kuchelewesha usikilizaji na uamuzi wa mashauri hizi (legal technicalities), wakati Katiba imetoa mwongozo kwamba tusifungwe kupita kiasi na masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka, hilo sharti limetajwa kwenye Ibara ya 107A(2)(e) haki inapaswa itendeke, tunapojiendekeza kwenye hizi hili tunaahirisha tu mgogoro hatuwezi kutatua mgogoro,” ameongeza Mhe. Masaju.

Pamoja na hayo, Jaji Mkuu amesema kwamba, wadau wanapaswa kuendelea kudhibiti hatua zinazochelewesha usikilizaji wa migogoro kwa kurahisisha matumizi ya notisi ya siku 90, kwa kuangalia wanaohusika kumfanya yule anayepewa notisi kutaka kushtakiwa, awajibike kuchukua hatua ambazo ni za kutatua na ikiwa ni hatua za usuluhishi wajadiliane ili kurahisisha usikilizaji wa migogoro na kuwataka wanaohusika na kuchakata notisi wawajibike ili kumaliza migogoro mapema ipasavyo.

“Wale wanaohusika na kuchakata hizo notisi zinazotolewa na watu wanaotaka kuishtaki Serikali na Taasisi zake, wawajibike kushughulikia hiyo changamoto inayopelekea watake kushtakiwa, kwa namna hiyo migogoro mingi itaisha,” amesema Mhe. Masaju.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu ameongeza kuwa, uwajibikaji ni moja ya nyenzo inayotajwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050 pia ni sharti la kikatiba kama Ibara ya 25 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyosisitiza juu ya uwajibikaji, kujituma na kuzingatia nidhamu ili kufikia malengo yaliyowekwa, hivyo ameipongeza Tume ya Taifa ya Mipango kwa mkakati wanaouweka ili kuleta uwajibikaji.

“Uwajibikaji ni sharti la kikatiba, kitu kikishawekwa kwenye sheria tunawajibika kukitekeleza kwa sababu huwa kuna adhabu usipokitekeleza kwa hiyo Ibara ya 25 ya Katiba inatusisitiza juu ya uwajibikaji lakini pia inasisitiza juu ya kujituma na inasisitiza juu ya kuzingatia nidhamu ya kazi ili kufikia malengo tuliyojiwekea,” amesema Mhe. Masaju.

Aidha, katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), amesema Mahakama imepiga hatua kubwa kwa kuweka mifumo mbalimbali ya matumizi ya TEHAMA huku mifumo mingine ikiendelezwa na kuwasisitiza  wadau hao kuendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA kama yanavyosisitizwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050. Ametaja manufaa ya kutumia TEHAMA katika utendaji kuwa ni pamoja na kupunguza matumizi ya karatasi ili kuimarisha mwenendo wa mashauri, kupunguza muda na gharama za kiutawala, kuongeza uwazi na uwajibikaji, kuwezesha upatikanaji wa taarifa mapema ipasavyo na kutoa takwimu zinazoweza kusaidia katika kupanga na kupima utendaji wa Mahakama.

Akihitimisha hotuba yake, Jaji Mkuu amemtaka kila mdau wa haki kujitathmini, kubaini changamoto zake za kiuwezo, kiutendaji na kimaadili na kuzifanyia kazi ili kwa pamoja kufikia matarajio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza wakati ya kufunga Mkutano wa nne wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Sehemu ya Viongozi wa Mahakama na Wadau wengine wakiwa katika 
Mkutano wa nne wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara tarehe 16 Septemba, 2026 uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Wajumbe wa Mkutano wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha) alipokuwa akifunga Mkutano wa nne wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara tarehe 16 Septemba, 2026 uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (kulia) akichangia jambo wakati wa Mkutano wa nne wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.



(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Jumatano, 16 Septemba 2026

MAHAKAMA YA TANZANIA YATAJA MAFANIKIO YA USIKILIZAJI MASHAURI YA KIUCHUMI

      Mahakama yasema ufanisi wa utoaji haki ni muhimu katika kukuza uchumi

      Yabainisha changamoto ya matumizi mabaya ya Akili Unde na nyingine zinazokwamisha utoaji haki ipasavyo 

Na HALIMA MNETE- Mahakama Dodoma

Mahakama ya Tanzania imeeleza mikakati mbalimbali inayochukua katika kuimarisha utoaji haki na kuongeza ufanisi wa kushughulikia mashauri, huku ikibainisha changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa mikakati ya kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini.

Akiwasilisha Taarifa ya Mahakama Kuhusu Utekelezaji wa Mikakati kwa Wadau wa Mashauri ya Ardhi, Kodi, Biashara, Mabenki, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji katika Mkutano wa Wadau hao uliofanyika leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, amesema Mahakama imeendelea kutekeleza mikakati iliyowekwa kwa mafanikio kwa kushirikiana na wadau wa mnyororo wa haki.

Mhe. Nkya amesema mikakati hiyo ambayo idadi yake imefikia 10, mikakati nane inahusu Mahakama na wadau kwa pamoja, huku miwili ikiwahusu wadau pekee.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika kipindi cha Januari hadi Juni, 2026 Mahakama imekamilisha utekelezaji wa hukumu katika mashauri 1,290, huku kati ya Juni na Agosti, mwaka huu kukiwa na maombi 207 ya utekelezaji katika ngazi mbalimbali za Mahakama.

Aidha, Msajili Mkuu amesema, Mahakama imeendelea kuimarisha mawasiliano na wadau kupitia vikao vya (Bench-Bar), ambapo mwaka huu vikao 17 vimefanyika katika Mahakama Kuu, 23 katika Mahakama za Hakimu Mkazi na 115 katika Mahakama za Wilaya.

Katika upande wa usikilizaji wa mashauri, Mhe. Nkya anabainisha kuwa, Mahakama katika ngazi zake mbalimbali ilisikiliza jumla ya mashauri 101,879 kati ya 170,059 yaliyofunguliwa katika kipindi husika. Amesema, uwezo wa Mahakama kumaliza mashauri umefikia asilimia 95 ya idadi ya mashauri yanayofunguliwa.

Kwa upande wa mashauri ya madai, Mhe. Nkya ameeleza kwamba, jumla ya 69,911 yalisikilizwa kati ya 74,514 yaliyofunguliwa, huku mashauri 23,850 yakiwa bado Mahakamani na 1,913 yakitajwa kuwa mlundikano.

Mhe. Nkya pia amesema kuwa, Mahakama imeendelea kuhimiza matumizi ya njia za usuluhishi katika kutatua migogoro. Katika kipindi cha Juni hadi Agosti, mashauri 151 yalifanyiwa usuluhishi katika ngazi mbalimbali za Mahakama.

“Kati ya Januari na Agosti, mwaka huu Mahakama Kuu ilimaliza mashauri 181 kwa njia ya usuluhishi, Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama Kuu kikamaliza 283, Mahakama za Hakimu Mkazi 141 na Mahakama za Wilaya 200,” ameeleza.

Msajili Mkuu huyo ameongeza kuwa, Mahakama imeweka mikakati maalum ya kushughulikia mashauri ya kimkakati ambapo Mahakama ya Rufani imepanga mashauri 300 kwa ajili ya kikao kijacho, wakati Mahakama ya Ardhi imeanza kikao maalum tangu Agosti 24 kinacholenga kumaliza mashauri 399.

Aidha, Mahakama ya Biashara imeanza kikao maalum kinacholenga kumaliza mashauri 88, huku wadau wakitakiwa kutoa ushirikiano ili mashauri hayo yakamilishwe kwa wakati.

Mhe. Nkya ameongeza kuwa, Mahakama imewezesha utekelezaji wa hukumu za mashauri 532 ya Ardhi,  Biashara, Kibenki, Hifadhi ya Jamii, Kazi na Madai.

Katika upande wa matumizi ya Akili Unde, Mhe. Nkya anasema miongoni mwa changamoto alizozitaja ni matumizi yasiyofaa ya Akili Bandia (AI) na baadhi ya Mawakili kutumia katika maandalizi ya nyaraka za mashauri.

“Tayari kumekuwa na matukio kadhaa ambapo kuna hukumu ambazo hazipo zimetengenezwa kwa kutumia Akili Unde na kuwasilishwa Mahakamani kama nyaraka halisi,” amesema Mhe. Nkya na kuongeza kuwa, baadhi ya waliohusika wamechukuliwa hatua wakiwemo waliopewa onyo.

Msajili Mkuu ametaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na matumizi mabaya ya  Kanuni 96 (7) inayoruhusu kurekebisha nyaraka za rufaa zikiwa na mapungufu, Mashauri ambayo yanatakiwa kuanza katika mamlaka nyingine kufunguliwa kwanza mahakamani, Mawakili kufungua  maombi rasmi hata katika masuala ambayo wangeweza kuomba wakati shauri linaendelea mfano application for dismissal of the pending case, Baadhi ya mabenki, yanapopokea amri ya kukamata fedha (Garnishee Order Nisi).

Aidha, Mhe. Nkya ameeleza kuwa, ufanisi wa utoaji haki ni sehemu muhimu ya maendeleo ya uchumi na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Maendeleo, 2050 huku akitoa wito kwa Mahakama na wadau wote wa mnyororo wa haki kuendelea kushirikiana katika kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya akiwasilisha Taarifa ya Mahakama Kuhusu Utekelezaji wa Mikakati kwa Wadau Wa Mashauri ya Ardhi, Kodi, Biashara, Mabenki, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji wakati wa Mkutano wa Wadau hao uliofanyika leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika Mkutano kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mikakati kwa Wadau wa Mashauri ya Ardhi, Kodi, Biashara, Mabenki, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji katika Mkutano wa Wadau hao uliofanyika leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Aliyeketi kushoto ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma na kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga.

Sehemu ya Majaji na Wadau wa Mahakama waliohudhuria katika Mkutano wa Wadau wa Mashauri ya Ardhi, Kodi, Biashara, Mabenki, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji uliofanyika leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Sehemu ya Wadau wa Mahakama wakiwasilisha taarifa za utekelezaji wa mikakati iliyowekwa kuhusu mashauri ya Ardhi, Kodi, Biashara, Mabenki, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)










 

TANZANIA JUDICIARY OBSERVES HYBRID MODEL OF JUDICIAL COMMUNICATION

From FAUSTINE KAPAMA-Judiciary, Cape Town

The Judiciary of Tanzania is using hybrid model of judicial communication, which is considered among the best way of communication within Africa.

This was revealed today, September 16, 2026 by Senior Resident Magistrate from the Institute of Judicial Administration (IJA) Lushoto, Hon. Husna Rweikiza, at the ongoing African Judicial Exchange Network Roundtable is being held at Pullman Hotel City Centre here, which has been organized by CEELI Institute.

She was contributing in a panel that discussed about Country Perspectives on Judicial Communication; Who speaks on behalf of the Judiciary. The discussion was moderated by District Judge from United States, Hon. John Tunheim.

Other Discussants were Justice Henry Adonyo from Judiciary of Uganda, Justice Fatimah Nadoma from Judiciary of Nigeria, Judge Jean Rosemary Kayira from Judiciary of Malawi and Judge Hellen Onkwani from Judiciary of Kenya.

Speaking on the matter, Hon. Husna stated that before enactment of the Judiciary Administration Act, the Registrar of the Court of Appeal was accounting officer, dealing with both case management as well as administration issues like human resources management, as well as estate management.

“Changes of circumstances came after the National Assembly of the United Republic of Tanzania enacted the Judiciary Administration Act in 2011 which introduced two important offices, that is the office of the Chief Court Administrator and the office of the Chief Registrar,” she said.

Hon. Husna pointed out that following such new shape, the Judiciary of Tanzania could no longer have only one Spokesperson, as it was in the past before the enactment of the Act in question and adopted a hybrid communication model.

“Institutional and administrative matters are generally communicated by the Chief Court Administrator or designated professional spokespersons, particularly through the Information, Education and Communication Unit…

“Matters relating to the administration of justice are communicated by the Chief Registrar, while broader institutional policy and justice dispensation matters are mainly communicated by the Chief Justice,” Hon. Husna told the participants.

She also explained that, although the Judiciary had a dedicated Information, Education and Communication Unit, comprising trained professionals, judicial communication is not limited to the Unit. Senior judicial leaders also communicated on institutional matters while working closely with the communication professionals.

She expounded that the Judiciary of Tanzania use various communication channels, including press releases, media briefings, updating website, social media platforms, public outreach programmes, stakeholder consultations, Law Week celebrations, exhibitions, radio and television interviews and educational forums.

As a notable example, Hon. Husna highlighted the “Sema na Mahakama” live television programme conducted in 2023 and 2024.

She explained that judges responsible for various High Court registries and directors of different functional directorates participated in live television programmes, responded to questions from the public and provided information on judicial services through television stations with nationwide coverage.

Hon. Husna noted further that the Judiciary of Tanzania also coordinates its communication with other justice sector institutions, including the Ministry responsible for Constitutional and Legal Affairs, the National Prosecutions Service, Law Enforcement Agencies, the Tanganyika Law Society, the National Bar Association and development partners.

Such coordination, she explained, supported coherent public messaging while respecting the distinct mandates of each institution.

She also cited the Judiciary’s digital transformation initiatives, including electronic filing and virtual court proceedings, as an example of how coordinated communication had supported institutional reforms, increased public understanding and encouraged adoption of new systems.

Effective judicial communication contributed to public trust in the rule of law by enabling citizens to understand court procedures, judicial decisions and institutional reforms. Public confidence depended not only on the quality of judicial decisions but also on the clarity, accessibility and credibility of institutional communication.

Judicial communication has become an essential component of modern judicial administration in Tanzania. By combining transparency, professionalism, ethical restraint and strategic public engagement, the Judiciary could strengthen public confidence while maintaining its constitutional independence.

Judicial communication in the Judiciary of Tanzania had undergone significant transformation over the past decade, moving from a traditionally reserved approach towards a more proactive strategy in response to increasing public demand for transparency, accountability and accessibility.

Through the Judiciary’s Five-Year Strategic Plan, particularly Pillar Three on Stakeholder Engagement, communication had been recognised as a strategic function supporting the delivery of justice.

It was intended to educate the public, improve understanding of judicial processes, address misinformation, communicate reforms and demonstrate accountability, while complementing and not compromising judicial independence.

The main objectives of judicial communication were to enhance public trust and confidence, improve access to justice through legal awareness, promote transparency in judicial administration, communicate reforms and innovations, facilitate stakeholder engagement and protect the integrity and independence of the courts through accurate and authoritative information.

Senior Resident Magistrate from the Institute of Judicial Administration (IJA) Lushoto, Hon. Husna Rweikiza, stressing a point during a panel discussion about Country Perspectives on Judicial Communication.

Senior Resident Magistrate from the Institute of Judicial Administration (IJA) Lushoto, Hon. Husna Rweikiza, listening to other Discussants during the session.


A section of participants to the African Judicial Exchange Network Roundtable (above and belwo) following what was going on during the discussion.



Another section of participants to the African Judicial Exchange Network Roundtable (above and belwo) following what was going on during the discussion.







 

MAHAKAMA, WADAU WAKUTANA KUTATHMINI UTEKELEZAJI WA MIKAKATI YA MASHAURI YA KIUCHUMI

·       Jaji Mkuu awataka Wadau kuwa huru kutoa maoni na michango ya kuboresha utoaji haki

·       Asema kipimo cha Kiongozi bora kinapatikana kwa huduma yake katika jamii

·       Asisitiza utatuzi wa migogoro kwa njia ya Usuluhishi

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Mahakama ya Tanzania pamoja na Wadau wa Sekta ya Sheria na Uchumi wamekutana kufanya Tathmini ya Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara lengo likiwa ni kuboresha ufanisi katika mnyororo wa haki za kiuchumi sambamba na kuoanisha utendaji kazi na Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.

Akifungua Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano- Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amewasisitiza wajumbe wa Mkutano huo kuwa huru kutoa maoni na changamoto zilizopo zikiwemo zinazoigusa Mahakama ili kuboresha uwazi na uwajibikaji katika utoaji haki nchini.

“Mkutano huu una mambo mazuri tu yanayotusaidia kuboresha ufanisi katika maeneo yetu ya kazi kwa jinsi yanavyohusiana na kuuwiana na mnyororo wa haki jinai, haki inaweza kuwa ni haki jinai au katika muktadha wa kikao hiki cha mashauri ya kiuchumi. Kwahiyo nawashauri kwamba muwe huru kabisa mnavyoshiriki mkutano huu. Wengi wenu nawafahamu ninyi tu si kwamba ni viongozi lakini ni wataalamu mahiri katika maeneo yenu, hivyo tunategemea kupata ushirikiano wenye tija kwa sababu ya uwepo wenu,” amesema Mhe. Masaju.

Aidha, Jaji Mkuu amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, umuhimu wa kiongozi haupatikani kwa Kiongozi kuwa ofisini pekee bali umuhimu wake unapatikana kwa huduma yake anayotoa katika jamii.

Mhe. Masaju amesema, nafasi na mchango wa Mahakama na Wadau katika utekelezaji wa majukumu ya kikatiba na kisheria katika muktadha wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni muhimu.

“Msingi Mkuu wa Dira hii ni Taifa Jumuishi lenye Ustawi, Haki na Linalojitegemea.Kwahiyo tunavyokaa hapa sasa pamoja na Mikakati hii tuliyokwishajiwekea tuweke au tupendekeze mikakati ya kutekeleza majukumu yetu ya kikatiba na kisheria katika muktadha wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo inamhususu kila mmoja wetu hapa. Kwa hiyo hiki kikiwa ni kikao cha tatu tunakutana ili kutathmini utekelezaji wa mikakati ya pamoja ya kushughulikia mashauri ya kodi, biashara, ardhi, mabenki na ushindani wa kibiashara,” ameeleza Jaji Mkuu.

Ameongeza kuwa, pamoja na kutathmini utekelezaji wa mikakati waliyojiwekea, Mkutano huo pia ni fursa ya kujadili masuala mengine yanayoweza kujitokeza baada ya kikao kilichopita na yale yanayoweza kujitokeza siku za mbeleni ambayo yanaweza kuathiri utekelezaji wa mikakati iliyowekwa katika utekelezaji wa majukumu ya Mahakama na Wadau.

“Mnapokuwa mmerejea katika Ofisi zenu muende mkayatekeleze haya lakini pia muwashauri viongozi wenu umuhimu wa kuyatekeleza hayo,” amesisitiza Mhe. Masaju huku akigusia juu ya umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi akirejea Ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Mahakama inahimizwa kukuza usuluhishi na kuzikumbusha Taasisi nyingine kuwa, zinapaswa kwanza kutatua migogoro kabla ya kufikisha mashauri mahakamani.

“Naomba niwarejeshe katika mkakati wa sita na wa kumi katika mikakati yetu inayohusu utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi. Lakini pia kwa njia za kiutawala katika maeneo yetu ya kazi. Na hili sharti ni sharti la kikatiba linatokana na ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo Mahakama inapotekeleza jukumu lake la kutoa maamuzi katika mashauri ya madai na jinai inatakiwa pia kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya watu wanaohusika katika migogoro,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Kadhalika, Jaji Mkuu amekitaka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kupitia Mawakili wake kuwasimamia wateja wao kwa maadili na kuwashauri kutumia mifumo ya usuluhishi na mamlaka za udhibiti badala ya kukimbilia mahakamani. Hatua hiyo inalenga kuepuka gharama zisizo za lazima na mapingamizi ya kisheria (preliminary objections) lakini vilevile ni utekelezaji wa Kanuni ya 59 ya Kanuni za Maadili ya Mawakili, 2018 Tangazo la Serikali Na. 118 la 2018 inayoelekeza Mawakili kuwataarifu Wateja wao kuhusu uwezekano na faida za kumaliza mashauri kwa mfumo wa usuluhishi

Akizungumzia kuhusu Uhuru wa Mahakama na Usimamizi wa Sheria; Mhe. Masaju amesema, kwa mujibu wa Ibara ya 107B ya Katiba, Mahakama itaendelea kuwa huru na kusimamia sheria huku akibainisha kuwa, mashauri ambayo hayakufuata taratibu za awali za kupatiwa ufumbuzi kwanza katika mamlaka husika kabla ya kuzihusisha Mahakama yatarejeshwa kwenye mamlaka husika.

“Na sisi huku mahakamani tutaendelea kusimamia sheria kwa ufanisi ipasavyo. Kwa sababu hata hivyo ni sharti letu la jukumu letu la kikatiba katika ibara ya 107B kwamba katika kutekeleza majukumu yetu Mahakama itakuwa huru isipokuwa itazingatia tu masharti ya Katiba na Sheria za Nchi,” ameeleza Jaji Mkuu.

Kupitia mkutano huo, Mahakama na Wadau hao wataendelea kubainisha changamoto zilizosababisha ucheleweshaji au zinazosababisha ucheleweshaji wa usikilizaji wa mashauri ya kiuchumi na kuendelea kutekeleza ipasavyo mikakati iliyowekwa na mingine itakayokubalika katika Mkutano huo.

Mkutano huo umehudhuriwa na Amidi wa Mahakama Kuu na Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Amir Mruma, Majaji Wafawidhi kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, Jaji Mfawidhi Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Elinaza Luvanda, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Kevin Mhina, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Wasajili wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu pamoja na baadhi ya Naibu Wasajili kutoka Mahakama Kuu Masjala Kuu, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi na Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara.

Wadau wengine waliohudhuria Mkutano huo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Shekalaghe na wengine kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wizara ya Fedha, Tume ya Taifa ya Mipango, Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Msajili wa Baraza la Ushindani.

Wengine ni kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Umoja wa Mabenki (TBA), Chama cha Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama, Baraza la Ushindani, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiongoza Mkutano kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara uliofanyika leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Kushoto ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma na kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga. 


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akitoa hotuba ya ufunguzi wa
Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Picha za Wadau mbalimbali za Wadau wa Mkutano kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo iliyokuwa ikitolewa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma akitoa neno la utangulizi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya akitoa taarifa ya utekelezaji wa mikakati kwa upande wa Mahakama ya Tanzania wakati wa Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu akichangia jambo wakati wa Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Shekalaghe akichangia jambo wakati wa Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.