·
Kamishna Mkuu wa Magereza asema
umepunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya malalamiko ya Wafungwa, Mahabusu
·
Waipongeza Mahakama kwa kuondoa zaidi
ya asilimia 80 ya changamoto zilizokuwa zikiwakabili Wafungwa na Mahabusu
·
Asema idadi ya Mahabusu yapungua na
hakuna Mahabusu wa Mahakama za Mwanzo gerezani
·
Wapongeza matumizi ya Mahakama
Mtandao ambapo zaidi ya mashauri 10,000 yamesikilizwa kwa njia hiyo
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Kamishna Mkuu wa Jeshi la
Magereza nchini, (CGP) Jeremia Yorum Katungu ameipongeza Mahakama ya Tanzania
kwa ushirikiano mkubwa inaoupatia Jeshi hilo ambao umewezesha kupatikana kwa
mafanikio lukuki ikiwemo kupungua kwa idadi ya malalamiko ya Wafungwa na
Mahabusu.
CGP Katungu alieleza hayo
jana tarehe 19 Septemba, 2025 alipomtembelea Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Mhe. George Masaju ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma lengo likiwa
ni kusalimiana na kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali kwa ustawi wa utendaji
kazi wa vyombo hivyo.
“Matokeo ya ushirikiano
huu Mhe. Jaji Mkuu, kwanza magerezani kumekuwa na kupungua kwa malalamiko ya
wafungwa na mahabusu kuhusiana na changamoto za mashauri, miaka ya nyuma
ilikuwa ukiingia gerezani unaweza kusikiliza malalamiko kuanzia asubuhi mpaka
jioni malalamiko yalikuwa mengi sana, lakini sasa hivi nikuhakikishie
malalamiko sio kwamba tumeyamaliza yote lakini yamepungua kwa kiasi kikubwa
sana na tafsiri yake ni kwamba ni ushirikiano uliopo katika utatuzi wa
malalamiko hayo ambayo yamefanya wafungwa na mahabusu kuridhika na hivyo
kusababisha utulivu gerezani,” alisema Kamishna Mkuu huyo wa Jeshi la Magereza.
CGP Katungu alishukuru kwa
dhati ushirikiano huo ambao umekuwepo kati ya Mahakama pamoja na Jeshi la
Magereza na kukiri kuwa, kumekuwa na ziara za mara kwa mara za Majaji na
Mahakimu akiwemo Jaji Mkuu ambaye alifanya ziara yake ya kwanza katika Gereza
la Isanga tarehe 10 Julai, 2025.
Kamishna Mkuu huyo alikiri
kwamba, ziara hizo zimekuwa na manufaa mengi ikiwemo ushughulikiaji wa mashauri
ya wafungwa na mahabusu.
“Usikilizaji wa mashauri
ya wafungwa na mahabusu kupitia Mahakama Mtandao ni eneo ambalo pia tumekuwa
tukishirikiana vizuri, kama utakumbuka miezi kadhaa iliyopita mlitusaidia
kutupa makasha 10 ambayo yanatumika kama vyumba vya Mahakama mtandao lakini pia
mmeendelea kutusaidia vifaa vya TEHAMA ambavyo vinatumika kwenye Mahakama
mtandao kwakweli tunashukuru katika eneo hilo na tumeendelea kuona ufanisi
katika usikilizaji wa mashauri kupitia Mahakama mtandao,” alieleza CGP Katungu.
Kamishna Mkuu huyo wa
Magereza alisema kwamba, kuanzia mwaka 2021 ndipo ulianza ushirikiano wa huduma
ya wafungwa na mahabusu kusikiliza mashauri yao kwa njia ya Mahakama Mtandao
ambapo kufikia Septemba, 2025 huduma ya Mahakama mtandao imeendelea kutolewa
katika vituo 97 na mpango uliopo ni kuwa na huduma hiyo katika Magereza yote
nchini.
“Katika kipindi cha mwaka
2021 mpaka sasa, zaidi ya mashauri 10,000 yamesikilizwa kwa njia ya huduma ya
Mahakama Mtandao katika Vituo hivyo 97 na baadhi maamuzi yamefanyika kwa
utaratibu wa Mahakama mtandao na hii kwakweli imekuwa na manufaa sana
kuondokana na changamoto za ucheleweshaji wa mashauri,” alisema CGP Katungu.
Aliongeza huku akirejea
maelekezo ya Jaji Mkuu alipofanya ziara katika Gereza la Isanga tarehe 10 Julai
mwaka huu kuhusu kuondoa mahabusu wa Mahakama za Mwanzo gerezani kwamba
maelekezo hayo yamefanikiwa kwa ufanisi mkubwa na sasa.
“Nikupongeze kwa dhati
kabisa, maelekezo hayo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa, tumekuwa na mawasiliano
ya karibu sana na watendaji wako kuhusu
suala hili na matokeo yanaonekana, sasa ulipokuja Gereza la Isanga kulikuwa na
Mahabusu 6, 415 lakini kwa tarehe 18 Septemba, 2025 idadi ya mahabusu waliopo
ni 4,658, utaona kuna idadi ya zaidi ya mahabusu 1,757 wamepungua na hayo ni
matokeo ya ziara ambayo ulifanya na maelekezo uliyotupa ambayo utekelezaji wa
maelekezo yako umeanza kuzaa matunda, na kitu cha kujivunia sana ni kwamba,
tunavyozungumza sasa Mahabusu wa Mahakama za Mwanzo hatuna magerezani,”
alieleza.
Aliongeza kuwa, Mahakama na
Magereza inashirikiana pia ni katika eneo la kubadilishana taarifa ambapo
alirejea maelekezo ya Jaji Mkuu alipofanya ziara katika Gereza la Isanga ambapo
pamoja na mambo mengine aliomba kupatiwa taarifa za kila siku za idadi za
Wafungwa na Mahabusu waliopo katika magereza mbalimbali nchini, amesema kazi
hiyo wanaitekeleza kwa dhati kwa kuwa manufaa yake wameanza kuyaona ikiwemo
kupungua kwa mashauri pengine hayakuwa na ulazima wa kukaa kwa muda mrefu.
“Lakini kuna kupungua kwa
idadi ya waliopo gerezani hususani Mahabusu, Mhe. Jaji Mkuu nitoe tu takwimu
kidogo ulifanya ziara tarehe 10 Julai, 2025, maelekezo uliotoa tunaendelea kuyatekeleza,
lakini wakati unafanya ziara ile idadi ya wafungwa na mahabusu ilikuwa 25,784
lakini hadi kufikia tarehe 18 Julai mwaka huu idadi ilikuwa 24,761 kwahiyo
idadi imepungua hususani ya mahabusu na kwamba Serikali imepunguza gharama
kubwa ya kuwahudumia mahabusu na wafungwa,” alisema CGP Katungu.
Aidha, alizungumzia
kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na vikao vya Mahakama Kuu
kuchukua muda mrefu kufanyika, changamoto ya kupatikana kwa mtandao kwenye
Mahakama mtandao, mahitaji ya vifaa vya TEHAMA,
“Magereza mengi hayana
miundombinu inayowezesha urekebishaji wa wafungwa, kuna haja ya kuwa na viwanja
vya michezo na burudani ndani ya viwanja vya Magereza, kuna haja pia ya kuwa na
vyumba maalum vya kutumika kama madarasa. Kwahiyo sasa hivi magereza nyingi
tunazojenga tunajitahidi kuweka miundombinu muhimu itakayowezesha urekebishaji,”
alisema.
Kamishna Mkuu huyo
alieleza kuwa, kuna changamoto ya baadhi ya Wilaya kukosa Magereza na kwamba
lengo ni Wilaya zote ziwe na Magereza ili kurahisisha usafirishaji wa wafungwa
na mahabusu. Ameongeza kwamba kwa sasa kuna ujenzi unaendelea wa jumla ya
magereza 12.
Aliongeza kwamba vitendea
kazi bado ni changamoto hasa magari, Serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili
ya kununua magari na hivi karibuni wamepokea jumla ya magari 10 aina Land
Cruiser pick up 10.
Naye, Kamishna wa Sheria
na Uendeshaji wa Magereza kutoka Jeshi Magereza nchini (CP) Nicodemus Tenga
alisema kuwa, kwa sasa Jeshi hilo lina Wanasheria zaidi ya 264 na wamesambazwa
kwenye vituo mbalimbali vya Magereza ikiwemo Magereza ya mikoani na wilayani.
Aidha, CP Tenga
ameishukuru Mahakama kwa kuwafundisha wanasheria hao jinsi ya kutumia Mfumo wa
Kieletroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) na kuwezesha magereza zote nchini
kutumia mfumo huo na kuondokana na matumizi ya karatasi na imesaidia kupungua
zaidi ya asilimia 80 ya changamoto kufuatia matumizi ya mfumo.
Akizungumza mara baada ya
kupokea taarifa kutoka kwa Kamishna Mkuu wa Magereza nchini, naye Jaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju alimpongeza Kamishna huyo kwa kazi
nzuri ambayo amekuwa akifanya ambayo matokeo yanaonekana.
“Niwapongeze kwa haya
mambo makubwa ambayo mmekuwa mkiyafanya naona unayatekeleza kwa kiwango kikubwa
sana licha ya changamoto, nashukuru sana kwa hii taarifa ambayo umetupatia ni
taarifa ambayo imejitosheleza ambayo itatusaidia sisi kuboresha huduma zetu ili kuhakikisha kwamba wajibu wetu
katika utekelezaji wa haki jinai unatekelezwa kwa ufanisi ipasavyo,” alisema
Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu alisema kwamba,
kuna umuhimu mkubwa wa kuwa ushirikiano na uhusiano mzuri baina ya Wadau wa
Haki Jinai wakiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi, TAKUKURU,
Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Madawa ya Kulevya, Jeshi la Uhamiaji na wananchi
ambalo lengo lake ni kupata na kuboresha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi
kila sehemu ili lengo lililokusudiwa lifanikiwe.
Aidha, Mhe. Masaju
amemtaka Kamishna huyo kuwa kama kuna changamoto zozote zinazohusu Mahakama
ambazo zitaendelea kujitokeza asisite kuijulisha Mahakama na kwamba kwa sasa
hatatembelea Magereza hadi atakapohakikisha kuwa changamoto zilizopokelewa
wakati wa ziara yake katika Gereza la Isanga zifanyiwe kazi/ziishe.
“Nawashukuru kwa
ushirikiano mkubwa ambao mmeendelea kutupatia hususani utoaji taarifa, na
kwamba kuna taarifa au changamoto zaidi msisubiri tuwaombe nyie andikeni tuyafanyie
kazi,” alisisitiza Jaji Mkuu.
Aidha, amewashauri
Viongozi hao wa Jeshi la Magereza kushughulikia mapema mapema maombi ya
wafungwa wanaosubiri msamaha wa Rais kwa sababu kuna Kamati mahsusi ya
kumshauri Rais kuhusu msamaha kwa wafungwa wanaosubiri adhabu ya kifo kwa
kufuata utaratibu husika, kwa sababu itasaidia kupungua idadi ya wafungwa.
Aidha, Mhe. Masaju
amemuomba Kiongozi huyo wa Jeshi la Magereza kuandaa taarifa kuhusu utekelezaji
wa Kifungu cha 134 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, ili kujua kama
kweli mashauri hayo yanamalizika ndani ya miezi sita.
“Tunatengeneza pia Kanuni
ambazo zitawezesha katika mashauri yanayosikilizwa na Mahakama za Hakimu Mkazi
na Mahakama za Wilaya wao nao Mahakama na washtakiwa wawe nao sasa wanapata ushahidi
wa upande wa kesi za mashtaka ili iwasaidie na wao kujitetea kwa ufanisi
ipasavyo, haitoshi tu kwamba kumpa haki ya kusikilizwa lakini akiwa hana
taarifa za tuhuma na ushahidi uliopo dhidi yake hapo hakutakuwa na haki ya
kusikilizwa aliyopewa itakuwa imenyofolewa kwa kiasi fulani na itakuwa inakiuka
Ibara ya 13 ya Katiba inayotaka usawa mbele ya sheria,” alisisitiza Jaji Mkuu.
Kadhalika, Mhe. Masaju alilipongeza Jeshi la Magereza kwa kazi kubwa ya urekebishaji wanaofanya na kulishauri Jeshi hilo kuangalia uwezekano wa kuwarudisha hadi mipakani wafungwa kutoka nchi za Jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao wanamaliza kutumikia mifungo vyao badala ya kuendelea kujaza idadi ya wafungwa magerezanina kuwa na wahamiaji haramu nchini.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (aliyeketi mbele) akizungumza na ujumbe kutoka Jeshi la Magereza nchini ulioongozwa na Mkuu wa Jeshi hilo, CGP Jeremia Yorum Katungu walipomtembelea Jaji Mkuu ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Walioketi kulia ni sehemu ya Viongozi wa Mahakama.
Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza kutoka Jeshi Magereza nchini (CP) Nicodemus Tenga akizungumza jambo wakati wa mazungumzo kati ya Jaji Mkuu na Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini yaliyofanyika jana tarehe 19 Septemba, 2025 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, (CGP) Jeremia Yorum Katungu (wa pili kushoto). Wa pili kulia ni Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza kutoka Jeshi Magereza nchini (CP) Nicodemus Tenga, wa kwanza kushoto ni Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Hubert.