Jumatatu, 29 Julai 2019

MAHAKAMA YA TANZANIA YAINGIA KWENYE MKONGO WA TAIFA WA MAWASILIANO

Na Magreth Kinabo na Lydia Churi-Mahakama
Mahakama ya Tanzania  leo imeingia Mkataba na Shirika la Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL) utakaowezesha Mahakama kuingizwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano  ambapo majengo 157 ya Mahakama nchini yataunganishwa. 

Akizungumza kabla ya kusainiwa kwa Mkataba huo, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock, alisema  mkataba huo wenye thamani ya Sh. bilioni 4.1 utawezesha kuunganishwa kwa majengo ya Mahakama kuanzia Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu,   Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya na baadhi ya Mahakama za Mwanzo zenye majengo ya kisasa.

Alizitaja Mahakama ambazo zitaunganishwa kwenye mtandao huo kuwa ni Mahakama ya Rufani 1, Mahakama Kuu  16, Mahakama Kuu Maalumu (Specialized Division 4, Mahakama za Mkoa 29, Mahakama za Wilaya 112 na Mahakama za Mwanzo 10.

‘Lengo kuu ni kuunda mtandao mpana wa Mahakama utakao unganisha Mahakama zote  nchini  pia kuunganishwa  pamoja na mtandao wa serikali yaani (Government Network (Gov Net) ili kuhakikisha huduma zote za serikali mtandao zinapatikana kwa urahisi pia kuiwezesha Mahakama kutoa huduma kwa wakati na wakati  umadhubuti,’ alisisitiza.

Bw. Enock  alisema  faida ya mkongo huo ni kurahisisha upatikanaji wa huduma za mahakama kwa kupitia mifumo yake ya  kielektroniki kama vile Mfumo wa kuendesha na kuratibu Mashauri (JSDS2) na Mfumo wa kuratibu Mawakili (TAMS), mazingira wezeshi ya kubadilishana taarifa kati ya Mahakama na Taasisi, wadau katika mfumo mzima wa utoaji haki nchini.

Aliwataja wadau hao kuwa Magereza, Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka, TAKUKURU, Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Chama cha Mawakili(TLS).

Faida nyingine ni kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi/haraka kupitia mifumo ya kielektroniki ya Mahakama wakati wote na kutoka mahali popote, kurahisisha upatikanaji wa taarifa mbalimbali hasa mwenendo wa mashauri na shughuli za Mahakama kwa wananchi na wadau wengine kwa ujumla.

Aliongeza kuwa faida nyingine ni kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za Mahakama, mfano, shahidi anaweza kuwasilisha ushahidi bila kulazimika kufika Mahakamani, wakili au wananchi anaweza kufungua shitaka au shauri kwa njia ya mtandao, na kuimarika kwa shughuli za kila siku za Mahakama kwa kuongeza ufanisi na weledi hivyo kuwezesha upatikanaji wa Haki kwa wakati.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw, Waziri Waziri Kindamba alisema Shirika lake litahakikisha wanafanya kazi kwa bidii ili kuwezesha Mahakama kuingia kwenye mtandao.

“Tutafanya kazi usiku na mchana ili tuweze kutekeleza hili kwa wakati, tena ikibidi kumaliza kabla ya muda uliopangwa katika mkataba wetu, alisisitiza Bw. huo.
Alisema tayari vifaa vimeshasambazwa katika baadhi ya Mahakama na ujenzi umeshaanza, hivyo watajitahidi kumaliza kazi kabla ya muda.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama  ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga alisema mkataba huo utakuwa ukiendeshwa kwa hatua, ambapo utaanza na wiki 14 za usambazaji wa vifaa na utakuwa endelevu kwa kipindi cha miaka miwili.

Mahakama ya Tanzania imesaini mkataba huo, ikiwa inatekeleza Mpango Mkakati wake wa Miaka Mitano ( Julai 2015 hadi Juni 2020), ambapo moja ya malengo  yake ni kuongeza ufanisi katika mtiririko mzima wa shughuli za Mahakama na hatua hii itafikiwa kwa kupanua matumizi ya Tehama katika ngazi zote za Mahakama ili kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wakati na pia kusogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi .
 Mahakama ya Tanzania leo imeingia mkataba na Shirika la Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL) utakaowezesha Mahakama kuingizwa kwenye mkongo wa Taifa. Pichani ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Hussein Kattanga (katikati) na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Waziri Kindamba (kulia)wakisaini Mkataba huo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Bw. Mohamed Mtonga.
 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Hussein Kattanga na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Waziri Kindamba wakikabidhiana Mkataba huo mara baada ya kuusaini.
 Wakionesha Mkataba huo kwa wajumbe wa kikao cha Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania mara baada ya kusaini.

 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Hussein Kattanga (katikati) na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Waziri Kindamba (wa pili kulia) wakionesha kwa furaha Mkataba huo mara baada ya kuusaini. Wa pili kushoto ni  Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Bw. Mohamed Mtonga. Wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mhe. Kifungo Kiriho Mrisho na wa kwanza kulia ni Mwanasheria wa TTCL.
 Wajumbe wa Kikao cha Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Hussein Kattanga (katikati waliokaa), Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Waziri Kindamba (kushoto) na Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Bw. Mohamed Mtonga (kulia) mara baada ya kusainiwa kwa Mkataba huo leo jijini Dar es salaam.
 Wajumbe wa Kikao cha Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wakiwa katika ukumbi wakisubiri kusainiwa kwa Mkataba kati Mahakama ya Tanzania na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL). 
Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama ya Tanzania Bw. Kalege Enock akielezea kuhusu Mahakama kuingia kwenye Mkongo wa Taifa wakati wa Hafla ya kusainiwa kwa Mkataba kati ya Mahakama ya Tanzania na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) leo jijini Dar es Salaam. 

Ijumaa, 26 Julai 2019

WAHITIMU CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM WAMTEMBELEA JAJI MKUU

Rais wa Jumuiya ya wahitimu wa chuo kikuu cha Dar es salaam Mhe. Balozi Mwanaidi Sinare Maajar amemtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake jijini Dar es Salaam

Rais huyo aliyeambatana na Afisa Mwandamizi wa Jumuiya hiyo Bw. Daniel Stephen alisema pamoja na mikakati mingi waliyonayo, hivi sasa wameanzisha ujenzi wa kituo cha wanafunzi (University Students Centre) ambapo pia yatakuwa ni makao makuu ya jumuiya hiyo.
Balozi Mhe. Maajar pia amewaomba wahitimu wote kusaidia jumuiya hiyo kwa hali na mali ili iweze kufanikisha malengo yake.

Awali akiwakaribisha wageni wake, Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni mhitimu wa chuo hicho alisema chuo kikuu cha Dar es Salaam ni mojawapo ya vyuo vikuu nchini kinachotoa wataalamu wa sheria wanaotumikia Mahakama ya Tanzania, hivyo aliishauri Jumuiya hiyo kushirikiana na wahitimu wa chuo hicho ili nao waweze kushiriki  katika kufanikisha maendeleo na malengo ya Jumuiya hiyo.
 Rais wa Jumuiya ya wahitimu wa chuo kikuu cha Dar es salaam Mhe. Balozi Mwanaidi Sinare Maajar akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

 Rais wa Jumuiya ya wahitimu wa chuo kikuu cha Dar es salaam Mhe. Balozi Mwanaidi Sinare Maajar akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma pamoja na Afisa Mwandamizi wa Jumuiya hiyo Bw. Daniel Stephen walipomtembelea Jaji Mkuu ofisini kwake.
 Rais wa Jumuiya ya wahitimu wa chuo kikuu cha Dar es salaam Mhe. Balozi Mwanaidi Sinare Maajar akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipomtembelea Jaji Mkuu ofisini kwake.






 

UHOLANZI KUISAIDIA MAHAKAMA YA TANZANIA

 Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Jeroen Verneul amesema uholanzi iko tayari kuisaidia Mahakama ya Tanzania katika nyanja za uwezeshaji kitaaluma ili haki iweze kupatikana kwa wakati na tayari imetenga fedha kwa ajili hiyo.
Balozi Verneul alisema hayo hivi karibuni alipofika ofisini kwa Jaji Mkuu kwa ajili ya kujitambulisha na kubadilishana mawazo na Kiongozi huyo wa Mhimili wa Mahakama.
Awali akielezea mikakati ya Mahakama, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alisema hivi sasa Mahakama inajipanga kuona uwezekano wa kuihuisha sheria ya Usuluhishi (Arbitration Act) na ile ya Kimataifa ili iwe na wigo mpana na rahisi katika Mahakama zetu.

“Hii itasaidia sana wakati Serikali yetu inaingia katika uchumi wa viwanda na  kuwa na wawekezaji wasiokuwa na mashaka juu ya uwekezaji wao endapo  mifumo ya usuluhishi  wa migogoro ya kibiashara ina utaratibu mzuri”, alisema Jaji Mkuu.

Alisema katika bara la Afrika zipo nchi zimefanya hivyo na sasa zina mafanikio makubwa katika utatuzi wa migogoro ya wawekezaji, hivyo yuko tayari kutumia vyombo vyote vinavyohusika kuona endapo sasa sheria iliyopo inahuishwa ili kuendana na matakwa ya karne hii.

 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Jeroen Verneul alipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es salaam.
 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi Balozi wa Uholanzi nchini Mhe Jeroen Verneul kitabu cha Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma pamoja na Balozi wa Uholanzi nchini  Mhe Jeroen Verneul wakibadilishana mawazo.




 

Ijumaa, 19 Julai 2019

MAHAKAMA YA TANZANIA KUSHIRIKIANA NA TAASISI YA KIMATAIFA YA UPATANISHI(ICC) KUWEZESHA MIGOGORO KUSIKILIZWA KWA NJIA YA UPATANISHI


 Na Magreth Kinabo

 Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma amesema Mahakama ya Tanzania iko tayari kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Upatanishi ‘International Chamber of Commerce’ (ICC) ili kuwezesha Mahakama kusikiliza migogoro kwa njia ya mfumo wa upatanishi( Abitration).

 Kauli hiyo imetolewa leo na Jaji Mkuu,  ofisini kwake  jijini Dar es Salaam ,wakati alipofanya mazungumzo na ujumbe watu watano kutoka taasisi hiyo, uliongozwa na Makamu wa Rais wa taasisi hiyo, Profesa . Dkt.  Mohamed Wahab.

 Awali Makamu huyo wa taasisi hiyo alisema wamefika hapa nchini ili kufanya mazungumzo na Jaji Mkuu, Profesa Juma kuhusu kushirikiana   na Mahakama ya Tanzania kuiwezesha kusikiliza migogoro kwa njia ya mfumo wa upatanishi.

Profesa, Dkt. Wahab aliongeza kwamba tayari   nchi nyingine zimeruhusu Mahakama,  kutumia mfumo huo wa upatanishi na umeonyesha kufanikiwa, ambapo alitolea mfano nchi ya Afrika Kusini na Mauritania, hivyo wangependa kuona na Tanzania inautumia  na taasisi hiyo itatoa mafunzo kwa majaji.

“Ni tunaiomba Tanzania kutengeneza kanuni ili kuwezesha mfumo huo   wa upatanishi kuweza kufanya kazi katika Mahakama za Tanzania,'' alisema Profesa.Dkt. Wahab.

Jaji Mkuu alisema yuko tayari kuwezesha mfumo huo kuanza kutumika  nchini kwa kuwa  ni muhimu  na utawezesha  migororo kusikilizwa haraka.

“Tuna Sheria ya Upatanishi, ni sheria ya zamani hivyo kuna haja ya kuihuisha ili iendane na mahitaji ya sasa,” alisema Profesa Juma.

 Alisema Mahakama inatumia njia ya upatanishi   ndani ya kesi za madai, lakini haujaweza kufanya kazi vizuri kwa sababu ya kutoeleweka ipasavyo miongoni mwa wadaawa.

Hivyo aliongeza  kwamba ni vizuri majaji na  mawakili wakapatiwa mafunzo juu ya masuala hayo. 

Profesa Juma aliutaka ujumbe huo kuandaa andiko na kuhusu mfumo huo na kuonyesha mapendekezo yao.

Ujumbe  huo umekuwepo nchini  tangu Julai 17 na Julai 19 , mwaka  huu na umefanya mazungumza  na ujumbe wa Tanzania kuhusu masuala  ya upatanishi ndani na nje ya nchi , ikiwemo Siku ya  Upatanishi  iliyofanyika kwenye  hoteli ya Slipway, Dar es Salaam Julai 18,mwaka huu na utakuja tena  mwakani,

 Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma,(katikati)  akiwa na ujumbe wa watu watano kutoka   Taasisi ya Kimataifa ya Upatanishi (ICC), ukiongozwa na Makamu Rais wa ICC, kwanza kushoto  Profesa . Dkt.  Mohamed Wahab anayesaini katika kitabu cha wageni.
 Makamu wa Rais wa Taasisi ya Kimataifa ya Upatanishi(ICC) wa kwanza kushoto  Profesa . Dkt.  Mohamed Wahab(aliyenyoosha mikono) akizungumza jambo na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma mara baada ya kumtembelea Ofisini kwake, akiwa na wajumbe wengine wa ICC.
 Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma,(katikati)  akizungumza  na ujumbe wa watu watano kutoka   Taasisi ya Kimataifa ya Upatanishi (ICC).
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma akimpatia, Makamu wa Rais wa   Taasisi ya Kimataifa ya Upatanishi (ICC)anayeshughulikia  masuala  ya  Mahakama ya Kimataifa ya Upatanishi, Ndanga  Kamau wa( pili kulia) nakala ya kitabu cha Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania.

Jaji  Mkuu wa  Mahakama ya Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa watu watano kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Upatanishi(ICC), (wa kwanza kulia) ni  Makamu Rais wa ICC, Profesa . Dkt. Mohamed Wahab, (wa pili kulia) ni Makamu wa Rais wa   Taasisi ya Kimataifa ya Upatanishi anayeshughulikia  masuala  ya Mahakama ya Kimataifa  ya Upatanishi, Ndanga  Kamau. (Kushoto) wa kwanza Madeline Kimei, wa pili ni Mshauri wa masuala ya Kisheria(ICC)  Leyou Tameru na wa tatu ni Mkurugenzi wa  ICC anayeshughulikia Usuluhishi wa Migogoro, Semi Houerb.

JAJI MKUU APENDEKEZA MAKOSA YOTE KUWA NA DHAMANA

Na Lydia Churi-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amependekeza makosa yote kuwa na dhamana kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa msongamano wa Mahabusu kwenye Magereza mbalimbali nchini.

Akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kuwakubali na kuwaapisha wanasheria waliomaliza mafunzo ya Sheria kwa vitendo kuwa Mawakili, jijini Dar es salaam leo, Jaji Mkuu ameyataja baadhi ya mapendekezo ya Mahakama yatakayosaidia kuondoa msongamano magerezani kuwa ni pamoja na upelelezi wa kesi kumalizika mapema.

Jaji Mkuu alisema Mahakama imekuwa ikilaumiwa kwa kuchelewesha kesi mahakamani lakini kinachosababisha kuchelewa kwa mashauri hayo ni upelelezi kutokukamilika kwa wakati.

“Kuchelewa kumalizika kwa shauri Mahakamani wa kulaumiwa ni wapelelezi na siyo Mahakama”, alisema Jaji Mkuu.

Alisema pendekezo jingine ni sheria kutamka wazi muda wa kufanya upelelezi yaani ikifika muda fulani upelelezi haujakamilika basi shauri hilo lifutwe mahakamani.

Alisema sheria zimeegemea zaidi kwenye adhabu kubwa huku akitolea mfano wa mashauri ya mauaji, matumizi ya dawa za kulevya, Uhujumu uchumi na ubakaji. Aliongeza kuwa mashauri haya yana adhabu kubwa na upelelezi wake huchukua muda mrefu.

Alisema ili kutatua changamoto ya msongamano wa mahabusu magerezani, Mahakama ya Tanzania pia inapendekeza masharti ya dhamana kulegezwa na kushauri kutumiwa kwa vitambulisho vya Taifa kwenye dhamana. 

“Hivi sasa wananchi wengi wana vitambulisho vya Taifa ambavyo vinaweza kutumika kama dhamana bila ya kumtaka mwananchi aonyeshe mali”, alisema Prof. Juma.
Jaji Mkuu alitoa mapendekezo hayo ya Mahakama alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na waandishi wa habari waliotaka kufahamu Mamlaka ya kutoa Mahabusu gerezani. Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama ndiyo yenye Mamlaka.

Hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza kufanyika kwa uhakiki ili kubaini mahabusu na wafungwa waliobambikiwa kesi hatimaye kuachiwa huru. Watakaonufaika na matokeo ya uhakiki huo ni mahabusu wenye kesi ndogondogo na wafungwa watoto, wazee, na makundi mengine yenye mahitaji maalum.

Jumla ya wanasheria 720 wamekubaliwa na kuapishwa kuwa Mawakili wakiwemo Majaji nane wa Mahakama ya Rufani, Majaji saba wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Majaji wastaafu watatu, Manaibu Wasajili kadhaa, Mahakimu pamoja na wanasheria wengine.

Hii ni mara ya 60 kwa Mahakama ya Tanzania kuwakubali na kuwaapisha Mawakili wapya. Kwa mara ya kwanza Mahakama ya Tanzania iliwakubali na kuwaapisha Mawakili wapya mwaka 1986.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) pamoja na baadhi ya Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu wakiongozwa na Mhe. Jaji Kiongozi (wa tatu kulia) wakiwa katika Sherehe ya 60 ya kuwakubali na kuwapokea Mawakili wapya 720  iliyofanyika mapema Julai 19, 2019 katika Viwanja vya Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (Law School of Tanzania). 
Picha mbalimbali za Mawakili wapya waliokubaliwa leo na Mhe. Jaji Mkuu. Miongoni mwa waliopata Uwakili katika sherehe hizi ni pamoja na baadhi ya Maafisa wa Mahakama wakiwemo, Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, Manaibu Wasajili na Mahakimu.


Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Adelardus Kilangi (wa pili kushoto) pamoja na baadhi ya Viongozi wa Serikali wakiwa katika Sherehe za 60 za kuwakubali na kuwapokea Mawakili wapya 720.






 Meza Kuu wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Mawakili wapya.
Meza Kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya maandalizi ya sherehe za kuwakubali na kuwapokea Mawakili wapya.
 
(Picha na Mary Gwera, Mahakama) 

Jumatatu, 15 Julai 2019

MAKAMISHNA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA WASTAAFU

Na Lydia Churi- Mahakama
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapongeza Makamishna wa Tume hiyo waliomaliza muda wao kisheria kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kipindi chao cha miaka sita walipotumikia Tume hiyo.

Akizungumza leo kwenye hafla ya kuwaaga Makamishna hao, Mwenyekiti wa Tume hiyo alisema kazi iliyofanywa na wastaafu hao ni kubwa, nzuri na ya mfano wa kuigwa kwa kuwa viongozi hao walijitoa kuhakikisha Tume inasonga mbele.

Alisema Mahakama bado inaweza kuwatumia viongozi hao kwa ushauri na kazi nyinginezo  kwa kuwa ni wanasheria wenye uzoefu mkubwa.

Makamishna waliomaliza muda wao na kustaafu rasmi ni Prof. Angelo Mapunda pamoja na Bibi Georgina Mulebya ambao kwa pamoja waliitumikia Tume hiyo kwa kipindi cha miaka sita iliyowekwa kisheria.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuagwa, Kamishna Mstaafu Bibi Georgina Mulebya aliwashukuru na kuwapongeza watumishi wa Tume hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii, kufuata Maadili na kuwataka kuendelea na moyo huo wakati wote wa utumishi wao.

Hata hivyo bibi Mulebya pia aliwapongeza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Katibu wa Tume hiyo Bwn. Hussein Kattanga pamoja na Naibu Katibu wa Tume hiyo Bibi Enziel Mtei kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwataka viongozi hao kuendeleza moyo huo wa kujitoa katika kulitumikia Taifa. 

Naye Prof. Mapunda alisema Tume ya Utumishi wa Mahakama ni nyeti na inafanya kazi bora licha ya kuwa na majukumu makubwa na watumishi wachache.  Alisema Tume hiyo ilipata hati safi kwa miaka mitano mfululizo hivyo watumishi wake hawana budi kuendeleza mazuri wanayoyafanya.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga Makamishna wawili wa Tume ya Utumishi wa Mahakama waliomaliza muda wao kisheria. Walioagwa ni Prof. Angelo Mapunda na Bibi Georgina Mulebya.  Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi na kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Stella Mugasha.    
 Aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ya Tanzania Bibi Georgina Mulebya akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga Makamishna iliyofanyika leo jijini Dar es salaam. Kulia ni Prof. Angelo Mapunda ambaye pia amemaliza muda wake kisheria kutumikia Tume ya Utumishi wa Mahakama.   

  Aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ya Tanzania Prof. Angelo Mapunda akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga Makamishna iliyofanyika leo jijini Dar es salaam. Kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revocati.
 Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akifuatilia jambo  wakati wa hafla ya kuwaaga Makamishna wawili wa Tume ya Utumishi wa Mahakama waliomaliza muda wao kisheria. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi na kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Stella Mugasha.   
 Aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ya Tanzania Prof. Angelo Mapunda akifurahia zawadi aliyokabidhiwa na Mwenyuekiti wa Tume hiyo. 
   Aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ya Tanzania Bibi  Georgina Mulebya akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo ambaye ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. 
 Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ya Tanzania pamoja na baadhi ya viongozi wa Tume hiyo wakiwa kwenye hafla ya kuwaaga Makamishna wawili wa Tume ya Utumishi wa Mahakama waliomaliza muda wao kisheria. Walioagwa ni Prof. Angelo Mapunda na Bibi Georgina Mulebya.
 Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Adeladius Kilangi akiwa kwenye hafla ya kuwaaga Makamishna wawili wa Tume ya Utumishi wa Mahakama waliomaliza muda wao kisheria. Walioagwa ni Prof. Angelo Mapunda na Bibi Georgina Mulebya.  Kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi na kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bwn. Hussein Kattanga. 

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Makamishna wawili wa Tume ya Utumishi wa Mahakama waliomaliza muda wao kisheria, Prof. Angelo Mapunda (wa pili kulia) na Bibi Georgina Mulebya (wa tatu kulia) pamoja na Watumishi wa Tume hiyo.

Jumapili, 14 Julai 2019

MAJENGO MAPYA YA MAHAKAMA GEITA NA CHATO YAKAGULIWA NA MENEJIMENTI YA MAHAKAMA YA TANZANIA


Pichani ni muonekano wa jengo jipya la Mahakama ya Wilaya Chato lililopo mkoani Geita, jengo hilo la kisasa lipo katika hatua za mwisho za ukamilishwaji wake kabla ya kuanza kutumika rasmi.
 Msajili Mkuu- Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati (wa kwanza kushoto), Mtendaji wa Mahakama ya Rufani (T), Bw. Sollanus Nyimbi (mbele kulia) pamoja na sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Chato wakiwa eneo la jengo hilo jipya tayari kwa ukaguzi. Lengo la ukaguzi ni kuhakikisha kuwa kila kitu kimekaa sawa kabla ya kuzinduliwa na kuanza kutumika rasmi kwa jengo hilo. Ukaguzi huo umefanyika mapema Julai 13, 2019.

Ukaguzi wa jengo ukiendelea katika sehemu mbalimbali za jengo hilo.
 Msajili Mkuu- Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita na Mahakama ya Wilaya Chato iliyopo mkoani Geita.

Picha ya pamoja, Watumishi wa Mahakama mkoani Geita pamoja na sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania walipotembelea eneo hilo kwa ajili ya ukaguzi wa majengo mapya ( Mahakama ya Wilaya Chato na Mahakama ya Hakimu Mkazi- Geita)

Muonekano wa jengo jipya la Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita lililopo katika hatua za mwisho za ukamilishwaji wake, jengo hili pia limekaguliwa na Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama.
 Sehemu ya Maafisa Wakuu wa Mahakama ya Tanzania wakiwa katika jengo jipya la Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita tayari kwa ukaguzi.
 Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Mahakama ya Tanzania, Bw. Edward Nkembo (aliyenyoosha kidole) akiwaonyesha kitu baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama pindi walipokuwa wakikagua jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita.

Mhandisi kutoka Kampuni ya MOLADI Tanzania ( Kampuni iliyojenga majengo ya Mahakama ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita na Mahakama ya Wilaya Chato) , Bw. Noel akieleza jambo kwa Wajumbe kuhusiana na jengo hilo ambapo kwa mujibu wake jengo hilo tayari limekamilika kwa asilimia kubwa na sasa wanaendelea kufanya marekebisho madogomadogo katika baadhi ya sehemu za jengo hilo.
 Muonekano wa jengo la sasa linalotumika kwa shughuli za Mahakama ya Hakimu Mkazi/Mkoa Geita, upatikanaji wa majengo mapya ya Mahakama katika mkoa huu utawezesha huduma ya utoaji haki kupatikana katika mazingira bora na rafiki zaidi kwa manufaa ya wananchi. Moja ya malengo ya Mahakama ya Tanzania ni pamoja na kuboresha na kujenga miundombinu ya majengo rafiki kwa manufaa ya utoaji wa huduma ya haki kwa wananchi.

(Picha na Mary Gwera-Mahakama, Geita)