Na Faustine Kapama – Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 31 Januari, 2022 amefungua Kongamano la wadau wa
sheria na utoaji haki nchini ambapo amewahimiza washiriki wote kujadili jinsi
mfumo wa haki jinai uliopo unavyoathiri wahanga na washitakiwa wa makosa ya
jinai.
Amesema kuwa Kongamano hilo linalofanyika katika ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma ni fursa
muafaka kwa Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Uingereza kubadilishana
uzoefu katika masuala mbalimbali, hususani maeneo ya mfumo wa haki jinai
ambapo Mahakama zote mbili wanashiriki changamoto zinazofanana.
"Kwa mfano, hatua ya awali ya
shauri la kijinai (committal proceeding) ni eneo ambalo sisi sote tunashiriki.
Madhumuni ya msingi ya kuendesha mwenendo huu ni kuamua kama kuna ushahidi wa
kutosha kumruhusu mtu anayetuhumiwa kutenda kosa apelekwe mbele ya Jaji kusikilizwa. Kwa
nini mwenendo huu wenye nia njema ubadilike kuwa kichaka cha
ucheleweshaji uliopitiliza nchini Tanzania?” amehoji Mhe. Prof. Juma.
Jaji Mkuu amesema kuwa wamekuwa
wakikumbana na ucheleweshaji mkubwa wakati wa kuendesha hatua hizo za awali za
mashauri ya jinai yanayosikilizwa na Mahakama Kuu, hivyo katika Kongamano hilo
Mtaalamu kutoka Uingereza, Jaji Nic Madge ataweza kutoa uzoefu wake na namna
nchi yake inavyofanya ili kuepuka ucheleweshaji huo.
Wawezeshaji wengine katika Kongamano
hilo ni Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman, Majaji wengine
wabobezi kutoka nchini Uingereza, Jaji Lain Bonomy na Nicholas Blake, Majaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Awamu Mbangwa, Mhe. Edwin Kakolaki na Mhe. Dkt.
Zainab Mango pamoja na Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Bw.
Laurean Tibasana.
Jaji Mkuu ana imani kuwa washiriki
wa Kongamano hilo watanufaika vya kutosha kutokana na mada mbalimbali zitakazowasilishwa
na Majaji na wadau wengine ambao wamebobea
katika maeneno kadhaa yananyohusu haki jinai. Ametoa shukrani zake kwa Serikali
ya Uingereza kwa kuendelea kutoa mchango wa kifedha kupitia mpango endelevu wa
kupambana na rushwa (BSAAT).
"Kongamano la leo ni hatua
muhimu katika kuimarisha ushirikiano ulioanza tangu mwaka 2017 katika Mkutano
wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya Madola (CMJA). Licha ya janga la UVIKO-19,
tunatarajia kuendeleza shughuli mbalimbali, ikiwa pamoja na mafunzo, miaka
mingi zaidi ijayo,” Jaji Mkuu amesema.
Awali, akizungumza katika Kongamano
hilo, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA),
Mhe. Dkt. Gerald Ndika, ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani amesema kuwa Programu
hiyo iliyoandaliwa ni moja ya programu nyingi za maendeleo ya kitaaluma ambazo
zimeundwa na Chuo kwa kushirikiana na washirika wake.
Mhe. Dkt. Ndika amesema kuwa Kongamano
hilo ni ushuhuda wa wazi kwamba Chuo hicho kimekuwa kikijitahidi kutimiza
majukumu yake chini ya Sheria ili kuboresha utoaji wa haki nchini kwa kutoa mafunzo
yanayofaa kwa maafisa wa Mahakama na watumishi wengine.
Kongamano hilo limeandaliwa na Mahakama ya
Tanzania kwa kushirikiana na Mahakama ya Uingereza na kuratibiwa na Taasisi ya
Majaji Wastaafu nchini Uingereza iitwayo Slynn Foundation wakishirikiana na IJA
kupitia ufadhili wa Programu ya Kitaifa ya Kuzijengea Uwezo Taasisi za Umma
Tanzania zinazohusika na kuzuia na kupambana na Rushwa (BSAAT).
Kuandaliwa kwa Kongamano hilo ambalo
litafanyika kwa siku moja ni sehemu ya jitihada za Mahakama ya Tanzania katika
kuwajengea uwezo maafisa wa Mahakama na wadau wengine wa sheria ya haki nchini
katika kutekeleza majukumu yao hususani utoaji wa haki jinai.
Mbali na maafisa wa Mahakama
waliostaafu na walioko kazini pamoja na Mahakama ya Uingereza, washiriki wengine
katika Kongamano hilo ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria na
maafisa kutoka ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikjali,
ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na mwakilishi wa Mkurugenzi
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Kongamano hilo ambalo ni sehemu ya
maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini ambayo kilele chake ni tarehe 2 Februari,
2022, pamoja na mambo mengine, limelenga kujadili uboreshaji mbalimbali uliofikiwa
na Mahakama ya Tanzania katika utoaji wa haki jinai pamoja na kubadilishana
uzoefu wa namna haki jinai kwa wahanga na washitakiwa unavyofanyika kati ya
Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Uingereza.
Hii ni mara ya pili Kongamano hili
linafanyika baada ya lile la kwanza ambalo lilifanyika katika Wiki ya Sheria
mnamo mwezi Februari 2020 jijini Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akihutubia Kongamano linalojumuisha Majaji wa Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Uingereza kujadili, pamoja na mambo mengine, athari za mfumo uliopo wa haki jinai. Kongamano hilo limefanyika leo tarehe 31 Januari, 2022 katika ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Bw. David Concar akisisitiza jambo alipokuwa akiongea kwenye Kongamano hilo.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani akitoa neno la ukaribisho katika Kongamano linalowaleta pamoja Majaji kutoka Mahakama ya Tanzania na Uingereza.
Meza Kuu, ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Wandamizi wa Mahakama ya Tanzania waliohudhuria Kongamano hilo. Kutoka kushoto ni Msajili Mkuu, Mhe. Wilbert Martin Chuma, Mtendaji Mkuu, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Shamillah Sarwatt.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani (juu na chini) waliohudhuria Kongamano hilo wakifuatilia mada.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (juu na chini) waliohudhuria Kongamano hilo wakifuatilia mada mojawapo iliyokuwa inawasilishwa na wawezeshaji
Maafisa Wandamizi wa Mahakama ya Tanzania, ambao ni Msajili Mkuu, Mhe. Wilbert Martin Chuma (kushoto) na Mtendaji Mkuu, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kutoka kushoto) wakiwa na Majaji Wastaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Sauda Msafiri na Mhe. Januari Msoffe (kulia) wakifuatilia moja ya mada zilizokuwa zinawasilishwa kwenye Kongamano hilo.