Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya
Majaji,
Naibu Wasajili na Mahakimu wa Mahakama Masjala Ndogo ya Mbeya wametakiwa
kutambua, kudhibiti na kukabiliana na msongo wa mawazo kwa wakati, wakizingatia
kuwa afya njema ya akili ni msingi muhimu wa kufanya maamuzi yenye umakini,
weledi na ya haki katika utekelezaji wa majukumu yao.
Wito
huo umetolewa katika mafunzo maalumu yaliyowakutanisha Majaji na Mahakimu wa Masjala
Ndogo ya Mbeya, yaliyofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Lake Nyasa, iliyopo
katika fukwe za Ziwa Nyasa, Wilaya ya Kyela, ambapo washiriki walipata elimu
kuhusu chanzo, madhara na namna bora ya kukabiliana na msongo wa mawazo katika
maisha na mazingira ya kazi.
Mafunzo
hayo yaliendeshwa na mtaalamu wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Kilutheri ya
Matema, Wilaya ya Kyela, Dkt. Ebenezer Richard Minja, ambaye aliwaeleza
washiriki kuwa msongo wa mawazo ni hali inayoweza kumpata mtu kutokana na
changamoto mbalimbali za maisha na mabadiliko ya mazingira au mtindo wa maisha
na kwamba hali hiyo inapopuuzwa inaweza kuleta madhara makubwa kwa afya ya mtu.
Dkt.
Minja alisisitiza umuhimu wa mtu kutambua mambo yanayoweza kumletea msongo wa
mawazo na kuchukua hatua stahiki mapema, akiwataka washiriki kuzingatia ulaji
unaofaa, kufanya mazoezi mepesi mara kwa mara na kuepuka tabia ya
kujilinganisha na watu wengine.
Aidha,
alieleza kuwa kufanya ibada ni miongoni mwa njia zinazoweza kumsaidia mtu
kupata utulivu wa akili, kwa kuwa humwezesha mtu kujenga imani na kumweleza
Mungu changamoto anazokabiliana nazo.
Kwa
mujibu wa Dkt. Minja, msongo wa mawazo unapokomaa unaweza kuathiri kwa kiasi
kikubwa afya ya mtu na kusababisha matatizo mbalimbali, yakiwemo shinikizo la
juu la damu, magonjwa ya moyo, kupoteza kumbukumbu, kupungua uzito na kushuka
kwa kinga ya mwili, hali inayoweza kuongeza hatari ya kupata magonjwa mengine
kama kisukari.
“Ukihisi
mambo yanaenda mrama, tafuta msaada mapema. Njiti moja ya kiberiti inaweza
kuangamiza msitu mzima, hivyo chukua hatua mapema kupambana na msongo wa mawazo
kabla matatizo makubwa hayajajitokeza,” alisema Dkt. Minja, huku akisisitiza
umuhimu wa kutafuta msaada mapema pale mtu anapohisi kuzongwa na msongo wa
Mawazo.
Akizungumzia
suala hilo kwa mtazamo wa mazingira ya kazi za Mahakama, Mtendaji wa Mahakama
Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Festo Chonya alisema kuwa, majukumu ya
kimahakama yanaweza kuwa miongoni mwa vyanzo vya msongo wa mawazo kutokana na
mlundikano wa mashauri, uzito wa maamuzi yanayofanywa pamoja na mazingira
mbalimbali yanayowazunguka watendaji hao.
Bw.
Chonya aliongeza kuwa, changamoto hizo zinahitaji usimamizi mzuri wa muda,
kutenganisha majukumu ya kikazi na maisha ya nyumbani pamoja na kutafuta
ushauri wa kitaalamu pale mtu anapohisi amelemewa.
“Akili
iliyochoka inashindwa kuchuja ukweli na uwongo kwa wakati, hivyo tujitahidi
kudhibiti msongo wa mawazo. Kwani afya ya watendaji wa Mahakama ina uhusiano wa
moja kwa moja na uwezo wao wa kutekeleza wajibu wa kutoa haki kwa jamii,”
alisema Bw. Chonya.
“Ili
uweze kutoa haki kwa jamii ni lazima ujitendee haki mwenyewe kwa kulinda afya
ya mwili na akili. Jamii inatuhitaji tukiwa na afya njema na akili timamu,” alisema
Mtendaji Chonya
Katika
mafunzo hayo pia washiriki walijifunza umuhimu wa kuzuia changamoto kabla
hazijawa kubwa kwa kujadili umuhimu wa mpango wa malezi kwa mahakimu
“mentorship programe”
Akizungumzia
suala hilo, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya,
alisema ‘Mentorship Programme’
ni muhimu katika kuwasaidia Mahakimu kukua kitaaluma, kuboresha utendaji wao na
kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika safari yao ya
kiutumishi.
Mhe.
Mtulya alisema kuwa, malezi ya kitaaluma yanaweza kuwa nyenzo muhimu ya
kumsaidia Hakimu kupata ushauri mapema kabla changamoto anazokabiliana nazo
hazijawa kubwa na kuathiri utendaji wake au kufikia hatua ya kushughulikiwa na
Kamati za Maadili.
“Mahakimu
wengi wanaharibikiwa kwa kutopata mlezi wa kumsaidia kabla changamoto haijawa
kubwa hadi kufikia kwenye Kamati ya Maadili,” alisema Mhe. Mtulya.
Kwa
upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mbeya, Mhe. Teddy
Mlimba, alisisitiza umuhimu wa kuwa na viongozi, walezi na wasimamizi wanaoweza
kuwasaidia watendaji kukabiliana na changamoto za kazi na maisha kwa wakati.
“Kazi
zetu ni ngumu sana na ukipata mtu wa kumtolea mambo au changamoto zako ni jambo
kubwa sana, hivyo ni muhimu kupata kiongozi, mlezi na msimamizi wa kukusimamia,”
alisisitiza Mhe. Mlimba
Mafunzo
hayo yameweka wazi kuwa mjadala kuhusu afya ya akili kwa Majaji na Mahakimu
haupaswi kuangaliwa kama suala binafsi pekee, bali kama sehemu ya kujenga
mazingira bora ya utoaji wa haki.
Majukumu
ya kimahakama yanahitaji umakini mkubwa, uwezo wa kuchambua hoja kwa kina na
kufanya maamuzi kwa usawa na bila kuyumbishwa. Kwa msingi huo, kulinda afya ya
akili na mwili, kusimamia muda, kutafuta msaada pale inapohitajika na kuwa na
mfumo imara wa malezi na ushauri wa kitaaluma ni miongoni mwa hatua zinazoweza
kuimarisha ustawi wa watendaji na ufanisi wa kazi za Mahakama.
Hatua
hiyo pia inalinda dhamira ya kujenga Mahakama yenye watendaji wenye weledi,
maadili na utayari wa kutekeleza wajibu wao kwa uadilifu. Afya ya akili ya
watendaji wa Mahakama ni uwekezaji katika haki na kulinda akili iliyo imara ni
sehemu ya kulinda haki ya mwananchi.
.JPG)
Mtaalamu
wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Kilutheri ya Matema, Wilaya ya Kyela Dkt.
Ebenezer Richard Minja (aliyesimama) akitoa mafunzo ya kukabiliana na Msongo wa
Mawazo kwa Waheshimiwa Majaji na Mahakimu (hawapo pichani).
Sehemu ya Viongozi wa Mahakama na Mahakimu ambao walioshiriki katika mafunzo hayo ambao ni wananchama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (TMJA) Tawi la Masjala Ndogo ya Mbeya wakifanya zoezi kwa vitendo.
Sehemu
ya washiriki katika mafunzo hayo ambao ni Mahakamu wananchama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (TMJA) Tawi la Masjala Ndogo ya Mbeya wakifuatilia mafunzo hayo kwa makini.
Hakimu
Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kyela Mhe. Roster Mofuga akichangia jambo
katika mafunzo hayo, (katikati) ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya
Wilaya Mbeya Mhe. Tedy Mlimba na (kushoto) ni Naibu Msajili Mahakama ya
Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer.
Jaji wa
Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mbeya Mhe. Mussa Pomo (aliyesimama) akizungumza
jambo katika mafunzo hayo, kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya
Mbeya Mhe. Benard Mpepo.
Viongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya wakiwa
katika mafunzo hayo (wa kwanza kushoto) ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala
Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya, (katikati) ni Jaji wa Mahakama kuu masijala
Ndogo ya Mbeya Mhe. Angaza Mwipopo na Jaji wa Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya
Mbeya Mhe. Mussa Pomo (wa kwanza kulia)
(Habari Hii Imehaririwa na INNOCENT KANSHA - Mahakama)