Na
Mary Gwera, Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amezindua rasmi kitabu cha
Mkusanyiko wa Mashauri ya Watoto (Compendium of Child Justice Cases) huku
akitoa wito kwa Majaji, Mahakimu na wadau wa ‘Haki Mtoto’ nchini kuwezesha mashauri
ya Watoto kusikilizwa na kumalizwa kwa wakati.
Akizindua
rasmi kitabu hicho leo Julai 19, 2021 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere
jijini Dar es Salaam, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa maamuzi yanayotolewa na
Mahakama nchini yamebeba na kusheheni maelekezo, mafundisho na busara
zinazohitajika katika kulinda haki za mtoto na hivyo maamuzi yanayogusa haki na
maslahi ya mtoto ni lazima yapatikane kwa urahisi na yakatumiwa kama rejea na
wadau wote wa haki za mtoto.
“Sisi
sote tukumbuke kuwa, ‘Haki Mtoto’, kwa maana ya haki, ulinzi na ustawi wa
mtoto; haipatikani Mahakamani peke yake. Bali, inapatikana katika “Mfumo Jumuishi
wa Haki Mtoto” ambao ni mwavuli mpana zaidi ya mahakama, polisi au ustawi wa
jamii mmoja mmoja. Tukumbuke kuwa, katika Haki Mtoto, kila mmoja wetu atimize
wajibu wake,” alisisitiza.
Akitaja
faida kadhaa za kitabu hicho, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa kitabu hiki kinakumbusha
kuwa, zipo sheria nyingi zaidi ya Sheria ya Mtoto ya 2009 [Law of the Child Act
Na. 21 ya 2009], na kuwa Haki Mtoto haipatikani ndani ya Sheria moja tu bali kuna
vifungu vya Katiba, Sheria mbalimbali, Kanuni, Taratibu, Mazoea na vigezo vingi
ambazo kwa pamoja vinajenga mfumo wa kufahamu mapana na marefu ya Haki ya
Mtoto.
“Naweza
kusema kuwa mkusanyiko huu ni ‘One-Stop Centre’ kuhusu kesi za Haki mtoto na
muhimu katika kazi za polisi, wapelelezi, mahakimu, majaji, maafisa ustawi wa
jamii, magereza na hata kwa watunga sera wanaposhughulikia ‘HAKI MTOTO’,
alieleza Mhe. Jaji Mkuu.
Kwa
upande mwingine, Mhe. Jaji Prof. Juma alitoa wito kwa Waheshimiwa Majaji
Wafawidhi wa kanda zote, Mahakimu Wafawidhi wa Mikoa na Mahakama za Wilaya
kuhakikisha kuwa katika maeneo yenu ya kazi kuna nakala za kitabu hiki ili
kusaidia kufanya rejea pale inapobidi kufanya hivyo.
Kwa
upande wake Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaohudumia Watoto
(UNICEF), Bi. Sampathi Perera alieleza kuwa uzinduzi wa kitabu hicho ni fanikio
litakalowawezesha Majaji na Mahakimu kuendelea kutoa maamuzi sahihi kuhusu
mashauri ya Watoto.
Sambasamba
na hilo, katika hafla hiyo, Mhe. Jaji Mkuu alizindua pia Ripoti ya Tathmini ya
Mafunzo kwa Wadau wa Haki za Watoto Tanzania, Mafunzo hayo yaliendeshwa na Chuo
cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania
kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka 2020 chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa
Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF).
Ripoti
hiyo imeonyesha kuwa mafunzo yaliendeshwa kwa wadau wa haki za watoto Mia Saba
na Arobaini na Sita (746) katika kanda zote za Mahakama Kuu ya Tanzania ambayo
kupitia mafunzo hayo.
Uzinduzi
huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama
(IJA) 2018/2019-2022/2023 wa kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya sheria nchini.
Uzinduzi
huo umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya Sheria nchini wanaohusika na
haki za mtoto wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu,
Mahakimu wa ngazi mbalimbali, Wawakilishi wa Taasisi za Serikali, Wawakilishi
kutoka Mashirika yasiyo ya Serikali na Wawakilishi wa UNICEF.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akionyesha Kitabu cha
mkusanyiko wa kesi za watoto “Compendium
for Juvenile cases” mara baada ya kukizindua rasmi.Wengine ni Jaji wa Mahakama ya
Rufani ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mhe. Jaji Mkuu ya Utafiti na Mafunzo-Mahakama, Mhe. Augustine Mwarija (kushoto) na kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani
na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe.
Dkt. Gerald Ndika, uzinduzi huo umefanyika leo Julai 19, 2021 katika Ukumbi wa
Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Ripoti ya
tathmini ya mafunzo kwa Wadau wa Haki za watoto “Impact Assessment on trainings of Juvenile Justice Frontline workers” wanaoshuhudia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija
(kushoto) na kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la
Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe. Dkt. Gerald Ndika.
Wakionyesha vitabu vya ripoti hiyo mara baada ya kuzindua.
Mhe. Jaji Mkuu akimkabidhi Mwakilishi kutoka
Wizara ya Katiba na Sheria Kitabu cha Mkusanyiko wa Kesi za Watoto na Ripoti ya
Tathmini ya Mafunzo kwa Wadau wa Haki za Watoto mara baada ya uzinduzi.
Baadhi
ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji Wafawidhi, Mahakimu Wafawidhi wa
Mahakama za Hakimu Mkazi, Viongozi wa Mahakama na wadau mbalimbali
waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha mkusanyiko wa kesi za watoto na
Ripoti ya Tathmini ya Mafunzo kwa Wadau wa Haki za Watoto uliofanywa na Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Mwakilishi
wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), Bi. Sampathi
Perera akielezea jinsi Tanzania ilivyopiga hatua kubwa katika kushughulikia
masuala ya watoto, ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa uzinduzi wa kitabu hicho muhimu.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto ambaye pia ni Jaji
wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akitoa ufafanuzi wa namna ya uandaaji wa Kitabu cha
mkusanyiko wa kesi za watoto na Ripoti ya Tathmini ya Mafunzo kwa Wadau wa Haki
za Watoto ulivyotekelezwa kwa ushirikiano wa wadau.
(Picha na Innocent Kansha, Mahakama)