Na Innocent Kansha – Mahakama
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru amezindua Kamati mpya ya Ukaguzi wa
Mahakama ya Tanzania na kuwataka wajumbe kusimamia rasilimali nyingi ilizonazo
Mahakama ili iweze kufanya kazi katika ubora unaotakiwa.
Akizindua kamati hiyo leo
jijini Dar es salaam, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania amesema sheria ya
Fedha ya mwaka 2001 inampa mamlaka Mkuu wa Taasisi kuteua wajumbe wanne wa
kamati ya ukaguzi na pia inatoa fursa kwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha
kuteua mjumbe mmoja.
“Nina imani tutaichukulia
kamati yenu kama sehemu ya menejimenti, shabaha kubwa ikiwa ni kuhakikisha
usimamizi wa rasilimali za Taasisi na mali za Umma zinalindwa na kusimamiwa kwa
weledi mkubwa zinatumika vizuri na kudhibitiwa”, alisistiza Mtendaji Mkuu.
Alisema Kamati ya ukaguzi
ni chombo cha utawala (Management Control System) kinachopewa jukumu la
usimamizi wa Taasisi hasa kwenye mambo hatarishi, na kuhakikisha kuwa michakato
ya udhibiti imeundwa na inafanya kazi kama ilivyo kusudiwa ili kufikia malengo.
Mtendaji Mkuu alisema
kutokana na dhamana na umuhimu wa kamati hiyo, shughuli zake zinapwaswa
kujumuisha wajumbe wa nje ili kufanya wajumbe waweze kufanya maamuzi sahihi
yasiyokuwa na upendeleo.
“Kutokana na muundo huu
ni matarajio yangu kwamba kamati itatekeleza wajibu na majukumu yake kwa uwazi
na kuwezesha mamlaka ya ndani ya Mahakama kuchukua hatua stahiki kwa wakati
kabla madhara hayajatokea”, alisema Bw. Kabunduguru.
Bw. Kabunduguru amemtaka
Mkaguzi Mkuu wa ndani na timu yake kuhakikisha taarifa za ukaguzi wa ndani
zinapatikana kwa wakati ili kushirikisha wadau wengine kutenda kazi zao kwa
wepesi na uwazi zaidi kwakuwa wao ndiyo kioo cha Taasisi.
Mtendaji Mkuu aliainisha
baadhi ya majukumu ya kamati hiyo kuwa kuimarisha shughuli za ukaguzi wa ndani
na wa nje, ambapo ripoti zao kwa kamati ni chanzo kikuu cha mafanikio ya
Taasisi.
Kamati hiyo pia inalo
jukumu la kupitia na kupitisha mpango wa mwaka wa ukaguzi wa ndani pamoja na
kupitia ripoti za ukaguzi wa ndani wa kila robo mwaka ili kuona changamoto
zilizojitokeza na kuchukua hatua stahiki.
Majukumu mengine ya
kamati ya ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania ni kupitia mkakati wa wakaguzi wa nje
na ripoti zao ili kuzishughulikia na kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza na
kuiletea Taasisi hati chafu. Kamati hiyo pia inalo jukumu la kupitia taarifa ya
fedha ya mwaka ya uhasibu kabla ya kusainiwa na Afisa masuhuli ili kuona kama
kuna masuala yoyote yanayohitaji utatuzi na kuyatolea ushauri kabla ya kwenda
nje ya Taasisi.
Mtendaji Mkuu aliongeza
kuwa majukumu mengine ni kumshauri Afisa masuhuli wa Mahakama juu ya hatua za
kuchukua kwenye masuala yanayohitaji uamuzi kulingana na taarifa za ukaguzi wa
ndani na ule wa nje na taarifa za uwazi katika utawala, usimamizi wa fedha,
mifumo ya udhibiti wa ndani ya Taasisi, mienendo ya kisheria, maadili ya
usimamizi na wafanyakazi.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti mpya
wa Kamati ya Ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania Bw. Pius Maneno wakati wa uzinduzi
wa kamati hiyo ulifanyika Mahakama ya Rufani Jijini Dar es salaam leo.
Mwenyekiti mpya wa Kamati
ya Ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania Bw. Pius Maneno akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati
hiyo uliofanyika Mahakama ya Rufani Jijini Dar es salaam .
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru akiwa kwenye picha ya pamoja na Wajumbe wa
Kamati mpya ya Ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania mara baada ya uzinduzi wa kamati
hiyo uliofanyika Mahakama ya Rufani Jijini Dar es salaam, kushoto kwake
walioketi ni Mwenyekiti wa Kamati Bw. Pius Maneno na kulia ni Katibu wa Kamati
Bw. Bwai Biseko.
Wajumbe wa kamati mpya ya Ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa kamati hiyo uliofanyika Mahakama ya Rufani Jijini Dar es salaam.